Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI MJEMA: ‘CCM itapata kipimo sahihi upinzani imara ukijitokeza uchaguzi’

Kuna kila dalili kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho chama Kikuu cha Upinzani nchini, hakitaweza kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa 2025 kwa sababu za kisiasa na kisheria.

Ukweli una sifa moja kuu, kwamba hata kama utaukataa namna gani, kamwe hauwezi kugeuka kuwa uongo, na ndivyo ambavyo ni ukweli kuwa Chadema kutoshiriki uchaguzi kutapunguza mzuka wa uchaguzi ambao tuliuzoea.

Lakini si hivyo tu, Chadema kutoshiriki uchaguzi huu kunakipunguzia CCM kipimo cha kujipima kwa sababu CCM imara inahitaji upinzani imara na katika uchaguzi huu, naamini ushiriki wa Chadema utakuwa kipimo sahihi cha CCM kujipima.

Japokuwa aliongea kimzaha mzaha bungeni, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku maarufu Musukuma naye aliona hili lisemwalo kwamba bila Chadema kushiriki uchaguzi mkuu kuna kitu fulani uchaguzi huu unapoteza ladha.

Akizungumza bungeni Aprili 2025, Musukuma alishauri hata kwa kuwapitishia mlango wa uani, Chadema wapewe kanuni wazisaini ili wakutane ulingoni kwa sababu kazi alizozifanya Rais Samia Suluhu Hassan zinajiuza zenyewe.

Inaweza kuongezewa hoja nyingine kwa Musukuma na kwa wana CCM kuwa, chama hicho kikongwe sasa hivi kina wanachama waliosajiliwa katika mfumo, wapatao milioni 13 na ndicho chama pekee kwa sasa kinachoongoza kwa kuwa na wanachama wengi nchini.

Ni kweli vyama vilivyosaini maadili ya uchaguzi mkuu ni 19 kikiwamo CCM, lakini tukiulizana mimi na wewe, ukiacha ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi CUF, hivi vingine mbona hatuoni uhai wao katika siasa za mageuzi?

Safari hii pengine tutaona vuguvugu fulani la Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), lakini pamoja na uwepo wa vyama hivyo bado haiondoi umuhimu na nafasi ya Chadema kama chama kikuu cha upinzani kwa takwimu sio blablaa.

Niambieni tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ni vyama vingapi vya upinzani huwa vinatoa ilani yake ya uchaguzi? Wananchi watavipima hivi vyama sio nyakati tu za uchaguzi, bali uhai wake.

Huku mitaani wapo wananchi tena wengi tu wanavifahamu vizuri baadhi ya vyama vya upinzani na bahati nzuri watanzania wa sasa wanajua kuchambua mambo kuliko ile miaka ya 70, wanajua vizuri maigizo ya baadhi ya vyama vya upinzani.

Ni ukweli ulio wazi kuna athari kubwa za kisiasa kwa chama kikuu cha upinzani kutoshiriki uchaguzi na baadhi ya matokeo yanaweza kufanya kukosekana kwa mitizamo tofauti na uwakilishi na kusababisha kuwa na bunge lisilo na uwiano.

Jambo lingine ni kuwa chama tawala kinaweza kushinda kwa hiyari kabisa ya wapiga kura, lakini ushindi wake ukaibua maswali kuhusu uhalali wa kisiasa na kukosa kipimo cha kupima uwajibikaji wake kwa sababu hakuna upinzani imara.

Lakini tusijidanganye kuwa kwa vile Chadema haitashiriki uchaguzi basi baada ya uchaguzi kumalizika nchi itatulia, mimi naona giza mbele kwa sababu siamini Chadema kitatulia tuli kama maji ya kwenye mtungi labda kiwe kimefutwa.

Tofauti na hivyo, ninaweza kuwa ninaota lakini ninaona jambo mbele kwamba Rais atakayepatikana anaweza asiongoze nchi kwa utulivu kwa miaka yake yote mitano, kukawa na kuzuiwa safari za viongozi na hata kunyimwa misaada. Kuna sababu mbili tu ambazo leo hii tunaona Chadema inawekwa pembeni kushiriki uchaguzi, moja ni ya kisiasa tu na nyingine ni za kisheria.

Ni sababu za kisiasa kwa sababu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeshikilia msimamo kuwa kwa vile hawakusaini kanuni za maadili ya uchaguzi huo za mwaka 2025 basi hawatashiriki, japo kuna utata wa kisheria juu ya hili.

Msimamo wa Chadema umejengwa katika msingi unaosukumwa na madai ya kutaka mabadiliko ya kimfumo ili kutoa hakikisho la chaguzi zinazofanyika nchini ziwe za haki, huru na zinazokubalika na wananchi na wadau wa siasa nchini.

Wanasheria wameshaweka msimamo kuwa Chadema kinaweza kuruhusiwa kusaini maadili hayo hata leo kwa sababu hakuna sheria inayowazuia, kwani kisheria wanatakiwa wasaini maadili hayo kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.

Huo ni upande mmoja wa shilingi, lakini kwa hali ilivyo sasa, hata kama INEC itaridhia Chadema kusaini maadili hayo, bado chama hicho hakitaweza kushiriki uchaguzi kutokana na zuio la mahakama la kukizuia kufanya shughuli za siasa.

Ni ukweli kuwa kwa muda tulionao, yapo mabadiliko ya msingi wanayoyadai Chadema kama Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi (sio jina) hayawezi kufanyika kwa sasa, lakini yapo mambo ambayo hayahitaji mabadiliko hayo.

Chadema walijishusha na kutaja mambo sita yarekebishwe ili washiriki na miongoni mwa mambo hayo ni kwamba hawataki taratibu zinazoruhusu wagombea wa upinzani pekee kuwa ndio wanaenguliwa na wasimamizi.

Lakini wanataka ambao hawana sifa za kupiga kura wasiwepo katika daftari la kupiga kura na kama hilo haliwezekani basi wasiruhusiwe kupiga kura lakini wanataka wasifanyiwe fujo na vyombo vya Dola katika mikutano ya kampeni.

Jambo lingine walililotaka ni kwamba mawakala wa vyama vyote wawe huru kufanya shughuli zao ikiwamo kujua kura zao na kama hakuna mawakala uchaguzi usifanyike, aliyeshinda ndiye atangazwe na uchaguzi usitumike kutoa kafara.

Ukiyatizama hayo mambo wala hayahitaji mabadiliko ya kisheria makubwa hivyo, mengine ni utashi tu wa kisiasa na uadilifu wa watendaji wa INEC na bahati nzuri CCM tayari kimeweka suala la Katiba mpya kwenye ilani yake 2025-2030 Mimi natamani tutafute muafaka na maridhiano ya kitaifa kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu na Chadema iruhusiwe kushiriki uchaguzi ili kuipa uhalali wa kisiasa CCM pale itakapopata ushindi wa kishindo wa haki kama inavyotamba.

Lakini CCM ijue upinzani imara ni kioo cha kujitizama na kujua wapi panapovuja ili wajirekebishe, tofauti na hivyo itakuwa sawa na hadithi ile ya kifalsafa ya mfalme aliyekuwa uchi lakini amezungukwa na chawa hawamwambii yuko uchi.