Polisi yazuia Chadema kufanya mikutano Tarafa ya Ngorongoro

Muktasari:
- Jeshi la Polisi wilayani Ngorongoro limesema taarifa za kiintelijensia zinaonyesha tarafa ya Ngorongoro si salama kwa sasa kufanya shughuli za kisiasa.
Arusha. Siku moja kabla ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanza operesheni ya kukijenga chama hicho Kanda ya Kaskazini, chama hicho kimesema hakitafika kwenye Tarafa ya Ngorongoro.
Uamuzi huo unafuatia zuio la Polisi Wilaya ya Ngorongoro la Juni 20, 2024 kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha eneo la tarafa hiyo si salama kwa sasa kufanyia shughuli za kisiasa.
Chadema inatarajia kufanya operesheni ya siku 21, kuanzia kesho Juni 22, 2024 kwenye majimbo 35 ya mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro, ikiongozwa na mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Juni 21, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema baada ya uongozi wa wilaya kupokea barua hiyo, wameshauriana na kuamua kuridhia suala hilo.
Amesema kutokana na sababu hiyo, mikutano iliyokuwa ifanyike katika Ngorongoro, itafanyika tarafa za Sale na Loliondo, ambazo pia zipo wilayani humo.
“Baada ya mashauriano hatujataka kuingia kwenye ugomvi au mabishano na Polisi, japo hatujaelewa “hali si salama” ni nini, wakati watu wanaishi na wanaendelea na shughuli kule. Tumesema tusiingie katika malumbano, tutapanga kwenda wakati mwingine,” amesema.
“Mikutano iliyokuwa ifanyike kwenye tarafa hiyo sasa itafanyika kwenye tarafa mbili zilizobaki. Na katika maeneo mengine yote tuliyooamba kufanya mikutano tumepata vibali,” ameongeza Golugwa.
Polisi wametoa zuio hilo kupitia barua yenye kichwa cha habari “kufanyika kwa mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya”, ambayo imerejea barua ya Chadema ya Juni 19, 2024.
“Ofisi yangu imepokea taarifa yako ya kutaka kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Ngorongoro, taarifa tumeipokea na tunakuhakikishia hali ya ulinzi na usalama katika maeneo uliyoomba kufanya mikutano hiyo.
“Aidha, kutokana na taarifa za kiintelijensia tulizonazo, eneo la tarafa ya Ngorongoro si salama kwa sasa kufanya shughuli za kisiasa,” imehitimisha barua hiyo.
Kwa mujibu wa Golugwa, kwa majimbo ya Ngorongoro na Karatu, Mbowe atakuwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na kwenye majimbo mengine, mwenyekiti huyo ataambatana na Godbless Lema, mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini na kote huo wanatarajia kuanza mikutano 105.