Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wazuia msafara wa Lissu Ngorongoro, wafuasi waziba barabara

Viongozi na wafuasi wa Chadema wakiwa wamekaa katikati ya barabara baada ya kuzuiwa na polisi kuingia ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro leo Jumamosi Septema 9, 2023.

Arusha. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu pamoja na msafara wake wamezuiwa kuingia ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili kufanya mkutano wa hadhara leo.

Lissu pamoja na viongozi wengine wa chama hicho, walikuwa kufanya mkutano ndani ya eneo hilo ambalo kuna zoezi la watu kuhama kwa hiari kwa waliokuwa wakazi eneo hilo, kwenda Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, kwa lengo la kupisha shughuli za uhifadhi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi September 9,2023, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Chadema Wilaya ya Karatu, Joseph Mtui, amesema leo mchana wakiwa wameambatana na viongozi wa kitaifa kwenda Ngorongoro walizuiwa na polisi.

Mtui amesema kabla ya kuanza safari walipewa taarifa wanatakiwa kuwa na vibali vya kuingia hifadhini na kwamba walianza taratibu ya kuvipata lakini walikwama.

"Tulienda kulipia vibali lakini baadae tulipata taarifa ya kuzuiwa wakati tayari viongozi wakiwa eneo la kituo cha ukaguzi wa watalii," amesema.

Mtui ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, Kata ya Karatu mjini, amesema baada ya hali hiyo, ndipo Lissu na viongozi wengine, waliamua kufunga barabara ya kuingia hifadhini, hali liyozua tafrani.

"Polisi walikuwa wanatufukuza lakini tunashukuru Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karatu (OCD), alifanya mazungumzo na Lissu na ndipo Lissu akakubali turejee Karatu wakati suala hilo linafanyiwa kazi," amesema

Amesema hata hivyo wakati wanageuza magari na watu wakiwa wamekusanyika wameshangazwa na polisi kuanza kupiga mabomu kufukuzwa.

Aidha amesema mkutano wa Lissu katika wilaya ya Karatu utafanyika kesho.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa, amesema wanashangazwa na Polisi kuzuia mikutano yao wakati tangu wameanza hakuna “ukiukwaji wa amani."

"Tunaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa juu kuona jinsi ya kufanya mikutano na hatutasitisha," amesema.

Juzi Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro, ACP Peter Lusesa, alitoa barua ya kuzuiwa mikutano ya Lissu kutokana na sababu za kiusalama katika eneo la Loliondo na Ngorongoro.

Hata hivyo, jana Lissu akifanya mikutano tarafa ya Loliondo katika vijiji vya Ololosokwani na Wasso na leo alikuwa aendelee na mikutano Ngorongoro.

Taarifa zaidi kuhusu kuzuia Lissu kuingia hifadhini humo, zinaendela kuwajia kwani mwandishi wetu anaendelea kuwasiliana na viongozi wa mamlaka husika.