Lisu akerwa bei ndogo ya pamba, aipa ushauri bodi

Muktasari:
- Wakati bei ya zao la pamba likitajwa kuchochea maumivu kwa wakulima, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema ni vyema Bodi ya Pamba kuweka bei ya ukomo wa zao hilo huku akishauri hatua kali zichukuliwe kwa watumishi wa umma wanaojishughulisha na biashara ya kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 1995.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema njia pekee ya kukabiliana na bei ndogo ya pamba, ni Serikali kuondoa vizingiti kwa wanunuzi.
Amesema tabia ya kuwaachia watu wachache kuhodhi soko la pamba ndio matokeo ya bei hiyo kuporomoka kutoka Sh2,200 mwaka jana hadi Sh1,060 mwaka huu kwa kilo, akishauri hatua kali zichukuliwe kwa watumishi wa umma wanaofanya biashra zao hilo kinyume cha sheria.
Ameshauri hatua hiyo kuchukuliwa kwa watumishi hao, kutokana na mchango wao kudumaza bei ya pamba hutokana na mgongano wa maslahi waliyonayo.
Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani, aliyasema leo Septemba 2, 2023 mkoani Simiyu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zao la pamba na hifadhi za Taifa.
“Bei juu ya pamba mwaka jana kulikuwa na ushindani wanunuzi walikuwepo ambao walinunua kwa bei kubwa zaidi Sh2,200, mwaka huu wameambiwa wainunue zaidi ya Sh1,060 kwa hiyo hatua ya kufanya kwa haraka na muda mfupi ni kufungua biashara hii kwa watu wengi zaidi na kuondoa vizingiti.
Bodi ya Pamba iweke bei ya chini ili lakini bei ya juu iwe ya ushindani kati ya wanunuzi na hii ni hatua ya muda mfupi haziitaji mabadiliko ya sheria,”amesema.
Jambo lingine alilokemea ni viongozi wa umaa kujihusisha na biashara ya pamba kinyume na sheria sheria ya viongozi wa maadili ya umma ya mwaka 1995 ambayo inamkataza kiongozi wa umma kujiingiza kwenye biashara.
Pia Lissu alishauri hatua za muda mrefu ya kuinua bei ya zao hilo ni ujenzi upya wa uchumi wa pamba kwa kufufua viwanda vya pamba vya kufuma nyuzi na vitambaa.
“Hayati Mwalimu Julius Nyerere alituachia nchi yenye uchumi wa pamba kulikuwa na viwanda mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Musoma Arusha vyote vimekufa.
“Kwa hiyo hatua zitakazotatua hili tatizo ni kuhakikisha tunatengeneza upya uchumi wa pamba, mfuko wa kuendeleza pamba ni njia ya kuwanyonya wakulima,” amesema.
Pia mifuko ya kuendeleza mazao haiendeleze kitu chochote zaidi ya kutafuna fedha za wakulima, kinachotakiwa ni kuhakikisha tunarudisha utaratibu wa mkulima kuuza mazao yake anakotaka,”amesema.