Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wapaza sauti sakata la Loliondo

Askari polisi wakibeba mwili wa mwenzao, Garlus Mwita Garlus aliyeuawa Loliondo juzi. Picha na Mtandao

Muktasari:

Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea kutanda Loliondo mkoani Arusha kufutia taarifa za mapigano kati ya askari na wakazi wa eneo hilo, Serikali imetakiwa kusitisha shughuli ya uwekaji alama inayolalalmikiwa hadi mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu suala hilo.

Dar/mikoani. Wakati hali ya sintofahamu ikiendelea kutanda Loliondo mkoani Arusha kufutia taarifa za mapigano kati ya askari na wakazi wa eneo hilo, Serikali imetakiwa kusitisha shughuli ya uwekaji alama inayolalalmikiwa hadi mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu suala hilo.

Vilevile, Serikali imetakiwa kuunda tume huru itakayohusisha uwakilishi kutoka wakazi wa eneo husika, lakini imesisitiza iliwashirikisha kwa kiasi cha kutosha.

Jana Chama cha ACT Wazalendo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walitoa msimamo wao kuhusu sakata hilo ambalo tayari limegharimu maisha ya askari mmoja huku waanchi kadhaa wakidaiwa kujeruhiwa.

Juzi, Naibu katibu Mkuu Bara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Benson Kigaila alisema chama hicho kitasimama pamoja na watu wa Loliondo dhidi ya changamoto wanazozipitia katika siku hizi za karibuni.

Kigaila alisema watu wa hao wanayo haki ya kukaa katika ardhi ile kisheria, hivyo Serikali iache mara moja operesheni ya kuwaondoa katika maeno hayo.

“Sisi kama chama tutasimama na watu hao hivyo Serikali ya Samia inatakiwa itambue hilo na kutoa ufafanuzi wa kina na kuwajulisha Watanzani kuwa Loliondo kuna uwekezaji gani unaotaka kufanyika,” alisema Kigaila.

Kutokana na hilo, alisema ipo haja ya Bunge kuunda kamati ya kuchunguza madhara yaliyotokea huko na walioshiriki kuyaleta hayo madhara waadhibiwe.

Wakati huohuo, taarifa iliyotolewa na LHRC na kusainiwa na Fulgence Massawe, kaimu mkurugenzi mtendaji, iliitaka Serikali kusitisha mara moja shughuli ya kuweka mipaka kwa kuwa shirikishi, imekosa uwazi na inavuruga amani na usalama.

“Kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na zoezi zima limekosa ushirikishwaji wa jamii husika, kitu kinachopelekea misuguano na vyombo vya dola katika kutekeleza zoezi hilo la kuweka mipaka.

“Ni wazi kuwa, tukio hilo na matukio mengine ni uvunjifu wa haki ya kuishi kama ilivyoainishwa katika ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. LHRC imesikitishwa na mauaji haya.

Taarifa hiyo ya LHRC ilieleza kumekuwepo na taarifa zilizoporiwa na wananchi kuhusu watu waliokamatwa na jeshi la polisi katika kata saba na hawajulikana wapo katika kituo gani mpaka sasa.

Pamoja na taarifa za watu kukamatwa katika kata hizo, pia kuna taarifa kuwa mwenyekiti wa kijiji cha Oloirien, madiwani wawili (2) wa viti maalum na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ngorongoro hawajulikani walipo hadi sasa.

Suala hilo pia lilizungumziwa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alipendekeza kusitishwa kwa uwekaji alama katika eneo hilo hadi mahakama itakapotoa uamuzi huku akiitaka kuunda tume huru itakayohusisha uwakilishi kutoka wakazi wa eneo husika kubaini kinachoendelea na kama kuna ukiukaji wa taratibu maofisa wa Serikali wanaohusika wachukuliwe hatua.

Aliongeza kwamba Serikali inapaswa kutumia mbinu ya mazungumzo kumaliza mgogoro huo, badala ya nguvu huku akimtaka Rais Samia kusitisha mpango wa kupandisha hadhi mapori tegefu, jambo alilosema limekuwa likisababisha migogoro kati ya askari na wananchi.


Madai ya ACT

Dorothy akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema taarifa za uchunguzi wa chama hicho zimebaini pamoja na askari aliyeuawa, kuna wananchi 14 wamejeruhiwa.

Alidai kuwa kati ya hao, wanane ni wanawake na wawili ni wazee, taarifa alizosema zimepatikana kutoka katika vyanzo vya chama hicho katika eneo husika.

“Tunasikitishwa na kauli za Serikali na Bunge zinazosema hapakuwa na taarifa za uvunjifu wa amani. Tumefuatilia kujua athari halisi, tumebaini Juni 10, mwaka huu kijijini Loliondo kulitokea mapigano kati ya wananchi na polisi,” alidai Dorothy.

Dorothy alidai kuwa vikosi hivyo vya askari viliwasili Juni 7, mwaka huu na kuzua hofu na wananchi kuona kwamba kuna nia ya kuporwa ardhi yao.

Alidai wakati askari wanaweka vigingi katika eneo la pori tengefu la Loliondo, wananchi walizingira hatua ambayo ilifanya askari wawatawanye kwa mabomu ya machozi.

Hata hivyo, alisema uamuzi wa Serikali kuweka vigingi katika eneo hilo unakiuka sheria huku akidai kuwa tayari wananchi walishapeleka shauri mahakama ya Afrika Mashariki na inatarajia kutoa uamuzi Juni 22, mwaka huu.


THBUB yafuatilia

Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB, Dk Thomas Masanja alisema tayari tume hiyo imeanza kufanyia kazi suala hilo na wanajipanga kwenda eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Tuna mpango wa kwenda huko kuchunguza na kujua ukweli, sisi huwa hatuzungumzi kwa kusikia lazima tufike tujue nini kinaendelea. Tukishapata picha halisi ndio tutazungumza,” alisema Dk Masanja.


Kauli ya Serikali

Akizungumza jana Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema wananchi wa Loliondo wameshirikishwa kikamilifu kwenye uwekaji alama na kukanusha madai ya askari kuvamia maeneo ya wananchi huku akitetea uwekaji mipaka kushirikisha askari.

“Lile ni eneo la hifadhi, mnapokwenda kwenye eneo kama lile la hifadhi ambalo lina wanyama wakali, lazima mwende na askari wa usalama. Wananchi walitoka kwenye makazi yao wakaja kuwafuata askari waliokuwa kwenye zoezi (kazi) la uwekaji alama na ndugu zangu Watanzania bila shaka mmeona wote, wako kazini wanaweka,” alisema.

Alisema kazi kama hiyo iliwahi kufanywa Igombe na hakukuwa na shida, kote wananchi wanashirikishwa na kusisitiza kuwa eneo la Loliondo wananchi wameshirikishwa zaidi kwa kuwa kulishaanza kuibuka maneno ya wananchi kutaka kuondolewa.

“Kwa hiyo Serikali ya watu ikaamua, tukae na wananchi, tuzungumze, tukubaliane, kilomita za mradi 2,500 wananchi chukueni zitumieni, kilometa 1,500 tunazihifadhi hili ni eneo linalotunza ikolojia ya Serengeti.Wale wananchi ndiyo walikwenda kuwafuata askari, hakuna askari waliokwenda kuwafuata wananchi, naomba hiyo tafsiri tuiweke vizuri,” alisema.

Kuhusu madiwani waliokamatwa, alisema hana taarifa nalo, lakini wote waliohusika kusababisha wananchi kushambulia maofisa waliokuwa wanatekeleza shughuli, sheria itachukua mkondo wake.

“Lakini niwahakikishie hali ni shwari, tofauti na baadhi ya watu ambavyo wanapeleka picha ya kwamba kama vile Loliondo kuna mapambano. Hakuna mapambano ni kikundi fulani cha watu walikusanyika wakaenda kuwavaa maofisa pale na kukatokea hicho ambacho kimetokea.

“Kunapotokea uzushi wa namna hii na sisi kama Watanzania, tunalo jukumu la kuwaambia wananchi ukweli juu ya kinachoendelea Loliondo. Hakuna mapambano kama nilivyosema.

Hakuna askari waliotumwa kwenda kuwaondoa watu, hakuna zoezi la kumuondoa mtu yeyote Loliondo na hakuna askari waliokwenda kuwashambulia watu kwa silaha za moto,” alisema.

Msigwa akizungumzia picha zilizosambazwa mitandaoni, alisema baadhi zimegundulika ni za zamani na zimetolewa maeneo ya mbali.

“Lakini nataka niwaambie, taharuki inayotengenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Loliondo haina uhalisia. Loliondo ni shwari, wapo baadhi ya watu wanaofanya uchochezi na Serikali ipo macho, hii ni nchi huru ambayo ina taratibu zake,” alisema.