Prime
Njia mbili zatajwa kufanikisha maazimio ya Chadema
Muktasari:
- Baada ya siku 309 za kifungo na kuruhusiwa kuendelea na shughuli za kisiasa wiki kadhaa zilizopita, Chadema imekuja na maazimio 12, ikiwamo ya madai ya Katiba mpya, wito wa kuachiwa kwa mwenyekiti wao, Tundu Lissu pamoja na masuala mengine kama maridhiano na kuondoa tozo kwenye mafuta.
Dar es Salaam. Maazimio ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yameibua mjadala mpana wa kisiasa nchini, huku njia mbili zikitajwa kuwa msingi wa kufanikisha hoja za chama hicho, zikiwamo madai ya Katiba mpya, wito wa kuachiwa kwa mwenyekiti wao, Tundu Lissu, pamoja na masuala mengine kama maridhiano na kuondoa tozo kwenye mafuta.
Wachambuzi wa siasa wanaona maazimio hayo ni mkakati mpana wa kisiasa, ambao mafanikio yake yatategemea mambo makuu mawili, huku swali likibaki iwapo msukumo huo utazaa matokeo au utaishia kuwa sehemu ya ushindani wa kisiasa kati ya upinzani na dola.
Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie, akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Mei 3, 2026, amesema maazimio ya Chadema hayawezi kufanikiwa kwa mbinu moja pekee, bali yanahitaji mkakati wa mashinikizo na ujenzi wa hoja zitakazoshawishi umma kuwaunga mkono.
“Silaha kubwa waliyonayo Chadema ni mashinikizo na uwezo wa kujenga hoja. Kwa mfano, suala la Katiba mpya ni matamanio ya Watanzania wengi na limekuwa ajenda ya muda mrefu,” amesema.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa Katiba mpya utategemea zaidi utashi wa kisiasa wa chama kilichopo madarakani pamoja na shinikizo la wananchi.
Hata hivyo, itakumbukwa katika mapendekezo ya tume iliyoundwa na Rais Samia ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, pia imependekeza Katiba mpya ipatikane ifikapo 2028 ili uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 2029 na uchaguzi Mkuu utakaofanyika 2030 utumie katiba hiyo.
Kuhusu suala la Lissu, Dk Loisulie amesema ni haki ya Chadema kushinikiza kuachiwa kwake, akibainisha kuwa chama hakiwezi kunyamaza wakati mwenyekiti wake yuko gerezani kwa muda mrefu.
Amesema njia kuu ya kufanikisha ajenda hizo ni shinikizo la umma, ujenzi wa hoja na ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu azimio la kuundwa kwa tume mpya ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29, mchambuzi huyo amesema changamoto ya tume iliyopo sasa ni kukosa imani kwa wadau tangu mwanzo, na hata baada ya kutoa ripoti imeacha maswali mengi kuliko majibu.
Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda akizungumzia hoja hiyo, amesema pendekezo la kuunda tume mpya ni sahihi, akibainisha kuwa wengi walitarajia ukweli kubainishwa wazi kupitia tume iliyopo, lakini hali hiyo haikutokea.
“Kibaya zaidi, hata ripoti yenyewe haijapatikana kirahisi, hivyo inaacha maswali mengi bila majibu,” amesema.
Akizungumzia Katiba mpya, Dk Mbunda amesema hiyo ni ajenda ya muda mrefu ya Chadema na kupata uungwaji mkono wa wananchi ndiyo njia kuu ya kufanikisha azma hiyo.
Kuhusu tozo za mafuta, mchumi Samwel Wangwe amesema kupunguzwa kwa tozo kutasaidia kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
“Sote tunafahamu athari za mfumuko wa bei. Kupunguza tozo kwenye mafuta kutachangia kushuka kwa bei za bidhaa na huduma nyingi, hivyo kuleta nafuu kwa wananchi, hasa wa kipato cha chini,” amesema.
Kuhusu maridhiano, Chadema imeeleza kuwa mazungumzo yoyote yanapaswa kuhusisha upatanishi na usuluhishi wa kimataifa. Msimamo wa chama hicho ni kwamba mchakato wa maridhiano uanze kwa kubaini ukweli kupitia uchunguzi huru wa matukio ya Oktoba 29, ukiwahusisha wadau wa kimataifa, wakiwamo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumzia hilo, Dk Loisulie amesema changamoto kubwa katika maridhiano ni kukosekana kwa imani kati ya pande husika na kusisitiza kuwa Serikali inapaswa kuonesha unyenyekevu ili kufikia mwafaka.
Kwa upande wake, Dk Mbunda amesema Chadema ni mdau muhimu katika mchakato wa maridhiano na kinapaswa kusikilizwa, akibainisha kuwa maridhiano yanahitaji zaidi ya makubaliano ya juujuu bali hatua za vitendo zinazojumuisha pande zote.
Maazimio ya Chadema
Katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Aprili 28 na 29, 2026 jijini Dar es Salaam, Chadema kiliweka maazimio 12, likiwamo la kusisitiza juu ya kesi ya Lissu, ambayo chama kinadai kuwa ya kisiasa. Kupitia azimio hilo, kimewataka wananchi kusimama pamoja na watetezi wa haki na kushinikiza aachiwe huru bila masharti.
Azimio jingine lilihusu uhitaji wa haraka wa kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza matukio ya vurugu za Oktoba 29. Hii ni licha ya kuwepo kwa tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo tayari imewasilisha ripoti yake, huku Chadema ikiendelea kuonesha kutokuwa na imani nayo tangu awali.
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Chadema kimeazimia kuwa ipatikane kabla ya mwaka 2027, kikisisitiza kuwa Watanzania hawawezi kuendelea kusubiri kwa muda mrefu zaidi. Chama hicho pia kimependekeza kuundwa kwa kamati ndogo ya Kamati Kuu itakayokuwa na jukumu la kuandaa mkakati wa kuharakisha mchakato huo, ikiwamo kuandaa muswada wa sheria kwa niaba ya wananchi utakaobainisha namna ya kura ya maoni itakavyofanyika chini ya usimamizi wa chombo huru.
Akiwasilisha maazimio hayo kwa waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alizungumzia pia kupanda kwa bei ya mafuta, akieleza kuwa chama kimeazimia kuwaongoza wananchi kudai hatua za haraka, zikiwamo kupunguza tozo mbalimbali ili kushusha bei ya mafuta pamoja na Serikali kuweka ruzuku kufidia ongezeko la bei.
Katika utekelezaji wa maazimio hayo, Mnyika alisema Chadema itaanza mikutano ya hadhara nchi nzima kupitia oparesheni maalumu iliyopewa jina la “Free Tundu Lissu,” yenye lengo la kudai Katiba Mpya na kuachiwa kwa Lissu.
Oparesheni hiyo itatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itaanza katika kanda za Serengeti, Victoria na Kaskazini kuanzia wiki ya tatu ya mwezi huu.
Aidha, chama kimeibua hoja za uwajibikaji kuhusiana na vurugu za Oktoba 29, kikitaka uchunguzi huru ufanyike pamoja na fidia kwa waathirika wa matukio hayo.
Maazimio mengine ya Chadema ni pamoja na kuwaenzi waasisi wa chama hicho, Edwin Mtei na Bob Makani, kwa kuyapa majina yao majengo ya makao makuu ya chama, jengo la Mikocheni litaitwa Edwin Mtei, huku lile la Ufipa, Kinondoni likiitwa Bob Makani.
Aidha, Kamati Kuu imesisitiza kuwa hakukuwa na uchaguzi huru na wa haki na imetaka waliohusika kupanga, kufadhili na kutekeleza vitendo vya mauaji katika vurugu za Oktoba 29 wawajibishwe.
Wakati huohuo, Chadema imekamilisha uteuzi wa baadhi ya nafasi za uongozi wa kanda zilizokuwa wazi, kwa kuwateua Godbless Lema na Salma Kasanzu kusimamia shughuli za kanda ya kati hadi uchaguzi mdogo utakapofanyika.
Pia, imesema itatoa taarifa rasmi kuhusu msimamo wake juu ya ripoti ya tume ya uchunguzi wa vurugu za Oktoba 29, Mei 5, 2026.