Heche: Chadema tumepitia misukosuko, tutasonga mbele tukiwa imara
Muktasari:
- Amesema licha ya magumu inayopitia ikiwemo kutofanya shughuli za siasa kwa mwaka, bado kitasimama imara.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema licha ya magumu kiliyoyapitia ikiwemo kutofanya shughuli za siasa kwa takribani mwaka mmoja, kitasimama imara na kusonga mbele.
Juni 10, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam ilitoa zuio la Chadema kujihusisha na shughuli za kisiasa kutokana na kesi ya mgawanyo wa mali iliyokuwa ikiendelea.
Hata hivyo, Aprili 15, 2026 ikiwa imepita miezi 10, Mahakama ya Rufani ilibatilisha uamuzi huo wa Mahakama Kuu na kukiruhusu chama hicho kufanya siasa, huku kesi ya msingi ikiendelea.
Leo Jumapili, Aprili 26, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche ameshiriki mkutano mkuu maalumu uliofanyika jimbo la Kibamba na kusema
chama hicho kitaendelea kujipambanua dhamira yake njema ya kutaka Watanzania waishi maisha bora kutokana na rasilimali zilizopo nchini.
Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche akizungumza na wananchi katika stendu Kuu ya Magufuli jijini Dar es Salaam leo,baada ya msafara wake kusimamishwa na wanainchi.Picha na Michael Matemanga
Akitolea mfano, amesema yeye mwenyewe aliwahi kukaa mahabusu kwa karibu mwezi mmoja alipokamatwa Dar es Salaam akisema ni miongoni mwa magumu na kashikashi wanazopitia, huku akiahidi kutokata tamaa.
Aidha, ametolea mfano kesi ya ugadi iliyowahi kumkabili aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kukamatwa kwa wanachama pamoja na kesi inayomkabili mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu.
Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche akizungumza katika mkutano wa ndani na viongozi na wanachama wa jimbo la kibamba jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Akisistiza Heche amesema hawapaswi kukata tamaa huku akisema lazima wajifunge mkanda kuendelea na safari.
"Mkituunga mkono mimi na Mwenyekiti Lissu tutasonga mbele," amewaambia wanachadema waliohudhuria mkutano huo.
Kiongozi huyo pia amewapongeza wanachama na viongozi wa chama hicho kwa uvumilivu waliouonesha katika kipindi chote walichokuwa kifungoni.
Aidha, Heche amewataka viongozi wa chama hicho na wanachama wapige kazi, huku wakipokea wanachama wapya, pamoja na kujenga ofisi mpya za kisasa.
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema kanda ya Pwani, Ntele Benjamin amesema misukosuko wanayoipitia katu haitawafanya warudi nyuma.