Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema kurudi na ‘makali’ yake? wadau washauri

Viongozi wa Chadema wakiwa katika Makao Makuu ya chama hicho leo Jumatano Aprili 15, 2026, jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Chadema, ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini kikiwa na madiwani na wabunge, kwa sasa hakina mwakilishi yeyote bungeni wala katika mabaraza ya madiwani.



Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikikutana katika kikao cha Kamati Kuu kufanya tathmini ya kipindi cha mpito cha siku 309 kilichojaa changamoto za kisheria na kiutendaji, kinatarajiwa kutoka na uelekeo mpya wa kisiasa.

Chadema, ambacho awali kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini kikiwa na madiwani na wabunge, kwa sasa hakina mwakilishi yeyote bungeni wala katika mabaraza ya madiwani, baada ya kususia kushiriki Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Aidha, Chadema ya sasa haina ruzuku, fedha ambazo ziliwezesha kusaidia uendeshaji wa chama na kulipa mishahara ya watumishi wake.

Wabunge ambao, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, walikuwa wakichangia sehemu ya mishahara yao kugharamia shughuli za uendeshaji wa chama, sasa hawapo.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walivyowasili makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo Jumatano Aprili 15, 2026. Picha na Michael Matemanga

Pia, Chadema ya sasa inayokutana kwenye Kamati Kuu hata katika Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) si sehemu ya wajumbe wake, kwani ili uwe mjumbe unapaswa kuwa na diwani au mbunge.

Kikao cha kesho na keshokutwa, chini ya uenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wake Bara, John Heche, kinafanyika wakati Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, yupo gerezani kwa mwaka mmoja sasa, akikabiliwa na kesi ya uhaini.

Kutokana na hali hiyo, kikao hicho kinatarajiwa kutoka na uelekeo mpya utakaokiwezesha chama kuendelea kuishi na kufanya siasa katika mazingira ambayo hakina nyenzo hizo, ili kiendelee kukubalika kwa jamii.

Wachambuzi na wadau wa siasa nchini wana shauku ya kuona uamuzi utakaochukuliwa na chama hicho ili kurejesha nguvu yake katika medani ya siasa na kuimarisha uungwaji mkono wa wananchi.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, amesema hali hiyo ni kipimo cha uimara wa chama, akieleza kuwa kikifanikiwa kuvuka kipindi hicho, kinaweza kujijengea imani kubwa zaidi kwa wananchi.

“Chadema kikiweza kusimama, kufanya mikutano na shughuli zinazokiunganisha na wananchi sambamba na kuzungumzia changamoto za wananchi mara kwa mara, kitaendelea kubaki kwenye ulingo wa kisiasa,” amesema.

Aidha, chama hicho kilijikuta kikiwekewa zuio na Mahakama Kuu ya Tanzania la kutofanya shughuli za kisiasa baada ya kufunguliwa kesi ya mgawanyo wa mali mahakamani.

Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche akizungumza na wananchi katika stendu Kuu ya Magufuli jijini Dar es Salaam leo,baada ya msafara wake kusimamishwa na wanainchi.Picha na Michael Matemanga

Hata hivyo, Aprili 15, 2026, kilipata nafuu ya kurejea katika ulingo wa siasa baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kuondoa zuio lililokuwa limewekwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija, Issa Maige na Abraham Mwampashi, waliokiruhusu chama hicho kuendelea na shughuli zake za kisiasa bila kikwazo.

Shauri hilo lilitokana na kesi ya madai ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, iliyofunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar.

Kikao hicho cha siku mbili, kinacholenga kutoa mwelekeo mpya wa kisiasa kwa chama hicho, kinatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa, huku wajumbe wakikumbuka kuwa mara ya mwisho walipokutana ana kwa ana katika kikao kama hicho ilikuwa Aprili 7, 2025.

Kikao hicho cha awali kilikuwa cha kipekee na kisichosahaulika, kwa sababu Mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu, alizungumza na watia nia wa nafasi mbalimbali za uongozi na kutoa kauli ya “No reforms, no election,” iliyozua mjadala mpana na baadaye kuambatana na hatua za kisheria zilizomfanya ashikiliwe mpaka sasa.

Ingawa kulifanyika kikao cha kidijitali mwishoni mwa Novemba 2025 na kupitisha maazimio kadhaa, kikao cha sasa kinatarajiwa kuwa na uzito wa kipekee, kikilenga kutathmini hali ya chama baada ya zuio hilo pamoja na kuweka mkakati wa kisiasa wa baadaye.

Imeelezwa kwamba kikao hicho kitaongozwa na ajenda za hali ya kisiasa nchini, kushikiliwa kwa mwenyekiti wao gerezani, ripoti ya Tume ya Mohamed Chande kuhusu uchunguzi wa vurugu za kabla na baada ya Oktoba 29, mwaka jana, pamoja na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pia, Kamati itajadili namna chama kitakavyokabiliana na changamoto kadhaa, ikiwamo kukosa ruzuku ya Serikali, kutokuwa na wabunge wala madiwani, na kutokuwa mwanachama wa TCD.

Tangu kuondolewa kwa zuio hilo, maandalizi ya kikao hicho yameendelea kuanzia ngazi ya kanda, ambako taarifa za hali ya kisiasa zimeandaliwa.

Kamati maalumu ya Zanzibar nayo ilifanya kikao kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.


Mitazamo ya wanazuoni

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda, amesema suala la kukosa ruzuku na kutokuwa na wawakilishi si tatizo la moja kwa moja, bali ni changamoto inayoweza kushindwa iwapo chama kitajikita katika kujitegemea kupitia michango ya wanachama wake.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walivyowasili makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo Jumatano Aprili 15, 2026. Picha na Michael Matemanga

“ACT-Wazalendo ilipoanzishwa mwaka 2014, kwa muda mrefu haikuwa na wawakilishi wala mwanachama wa TCD. Hata hivyo, waliunda baraza kivuli na kuwasemea wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, amesema changamoto zinazoikumba Chadema ni za kawaida katika siasa.

Dk Masabo amesema, ingawa chama hicho kinaweza kuyumba, hakiwezi kushindwa kabisa kuendesha shughuli zake za kisiasa.

“Mtihani uliopo ni kubuni mbinu madhubuti za kukifanya kifanye siasa na kushawishi wadau kukichangia fedha. Hapo ndipo changamoto ilipo,” amesema.

Amesisitiza kuwa kutokuwa na wawakilishi si kipimo sahihi cha kuipima Chadema, bali ni uwezo wake wa kufanya siasa katika mazingira magumu.

“Kila chama kinapaswa kubuni mbinu mpya za kufanya siasa katika mazingira tofauti. Hii ndiyo changamoto kubwa, hasa baada ya matukio ya Oktoba 29 kuonesha kuwa wananchi wanaweza kuandamana hata kama mamlaka hazipendi,” amesema.

Wanachama na wafuasi wa Chama mcha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa wakiwa katika ofisi za Kanda hiyo zilizopo Mtaa wa Kdege jijini Mbeya baada ya kufungua ofisi hiyo kuendelea na majukumu kufuatia kufunguliwa kwa Chama hicho Aprili 15.

Ameongeza kuwa matukio ya Oktoba 29 yanaashiria uwezekano wa matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi, hivyo vyama vinapaswa kuzingatia hali hiyo huku vikijenga ushawishi kwa wananchi.

“Chadema wana faida moja kubwa; hawakuwa sehemu ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, hivyo lawama kwao ni ndogo ukilinganisha na vyama vingine,” amesema Dk Masabo.


Maandalizi ya kikao yaiva

Kwa upande wa chama hicho, akizungumza na Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa, amesema maandalizi ya kikao cha Kamati Kuu yanaendelea vizuri huku wajumbe wakianza kuwasili kutoka mikoa mbalimbali.

“Kikao hiki, kinachofanyika baada ya siku 309, kitapokea na kujadili taarifa ya hali ya siasa nchini yenye mawanda mapana. Baada ya siku hizo mbili, tutatoka na maazimio kuhusu msimamo wetu wa kisiasa,” amesema.

Wanachama na wafuasi wa Chama mcha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa wakiwa ofisi ya Chadema Veta Manispaa na mkoani Iringa katika zoezi la kufungua ofisi ili kuendelea na majukumu kufuatia kufunguliwa kwa chama hicho Aprili 15, 2026. Picha na Christina Thobias

Golugwa amesema pia kikao hicho kitafanya tathmini ya ripoti ya Tume ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29 iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026, akibainisha kuwa awali chama hicho kilipinga namna tume hiyo ilivyoundwa pamoja na utendaji wake.

“Tutafanya tathmini ya ripoti hiyo na kupokea pia taarifa ya hali ya siasa, kisha tutatoa maazimio ya jumla. Baadaye tutatoa mwelekeo wa kisiasa pamoja na ratiba ya shughuli za chama zitakazoratibiwa na makao makuu na kanda,” amesema.

Ameongeza kuwa kikao hicho kinafanyika baada ya vikao viwili vya sekretarieti kuandaa ajenda, huku akisisitiza kuwa watakuja na dira, ratiba mpya pamoja na mtindo mpya wa kufanya siasa.

Akizungumzia hali ya rasilimali za chama, Golugwa amesema kipindi cha siku 309 kimeathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya chama, ikiwemo ofisi za kanda ambazo zimechakaa kutokana na kutotumika kwa muda mrefu.

“Baadhi ya mali za chama kama vifaa vya muziki vimeharibika na magari pia yameathirika kwa kukaa muda mrefu bila kutumika. Hata hivyo, kupitia kikao hiki cha Kamati Kuu, tutafanya tathmini ya jumla na baadaye kutoa majibu,” amesema kiongozi huyo.