Mgogoro wa Israel, Iran na hesabu za Marekani

Muktasari:
- Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alitoa tamko kwamba “ilikuwa muhimu”, kufanya mashambulizi hayo ya kushitukiza. Netanyahu alisema kuwa Israel iliiwahi Iran ili isifanikishe mpango wa kutengeneza mabomu ya nyuklia.
Vita au mgogoro wa Iran na Israel, kama unavyoitwa “Iran - Israel proxy conflict au Iran - Israel Cold War”, zipo tafsiri mbalimbali zinatolewa. Vinatazamwa vyanzo vya karibu, inatazamwa historia. Binafsi, namtazama Rais wa Marekani, Donald Trump.
Usiku wa Alhamisi (Juni 12, 2025), kuamkia Juni 13 (Ijumaa), Israel iliishambulia Iran, shabaha ikawa maeneo ya kijeshi na serikali. Mashambulizi hayo ya Israel, yakaua viongozi wengi waandamizi wa jeshi, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Kimapinduzi (IRGC), Hossein Salami na Mnadhimu wa Jeshi la Iran, Mohammad Bagheri. Wanasayansi mashuhuri wa nyuklia nchini Iran, nao wameuawa.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alitoa tamko kwamba “ilikuwa muhimu”, kufanya mashambulizi hayo ya kushitukiza. Netanyahu alisema kuwa Israel iliiwahi Iran ili isifanikishe mpango wa kutengeneza mabomu ya nyuklia.

Kisha, Iran nayo ikajibu mapigo. Matokeo yake, watu zaidi ya 220, wameripotiwa kufariki dunia na zaidi ya 1,000 kujeruhiwa Iran, wakati Israel, makumi wameuawa na mamia wamejeruhiwa katika mashambulizi kutoka Iran.
Inafahamika, Iran inaunga mkono vikosi vinavyopambana na Israel, kuanzia Hezbollah, Lebanon, mpaka Hamas, Palestina. Wakati Israel, imekuwa mkono wa kulia wa kikundi cha People’s Mujahedin of Iran, ambacho itikadi yake inakinzana na mamlaka za Tehran (Iran).
Mdadisi yeyote hatakubaliana na utetezi wa Netanyahu kuwa mashambulizi dhidi ya Iran, yalikuwa kuuwahi mpango wa mabomu ya nyuklia wa Serikali ya Tehran. Badala yake, atataka kuhoji ni kwa nini sasa, na je, kipi kinatafutwa Iran? Ni hapo Marekani inaingia, maana ni mshirika wa “kufa-na-kuzikana” wa Isarel.
Mtaalamu wa kuunda nadharia, atakuwa wa kwanza kutazama jinsi ambavyo Iran imekuwa ikichokonolewa hadi uvunguni. Bila shaka, kinachotafutwa ni Iran itoke nje, ili nguvu zake zijulikane.
Kuanzia kuuawa kwa Meja Jenerali wa Iran, Qasem Soleiman, Januari 3, 2020, nchini Baghdad, Iraq, kwa shambulizi lililoamriwa na Trump hadi aliyekuwa mwanasayansi mkuu wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh, ambaye msafara wake ulishambuliwa jirani na Tehran, kisha akauawa na walinzi wake, Novemba 27, 2020.
Ongezea, kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, Julai 31, 2024, mjini Tehran. Kila shambulio, unaweza kuliweka kwenye mtazamo wa jinsi ambavyo Iran inachokolewa.
Siku Marekani ikibaini kuwa Iran siyo tishio kijeshi, itakuwa historia kama ya Saddam Hussein, Iraq.
Marekani ina uzoefu wa vita kwa faida na hasara.
Ilijijenga sana kiuchumi wakati wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Iliathirika sana kiuchumi kupitia Vita ya Vietnam, Vita ya Korea, vilevile dhidi ya Saddam, Iraq.
Wamarekani wanayajua maumivu ya kupigwa vitani. Jinsi jeshi la Cuba lilivyoidhalilisha Marekani katika vita ya Bay of Pigs Invasion.

Kikosi kilichotengenezwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), kilichoitwa Brigedi 2506, kilichoingia Cuba kumpindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Fidel Castro, kilidhibitiwa Aprili 17, 1961. Wanajeshi wa Marekani walilazimishwa kusalimu amri ndani ya siku tatu tangu kuanza kwa mapigano. Hakuna wakati mbaya Marekani ilijiona imedhalilishwa vitani kama hapo.
Korea lilikuwa taifa moja kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Na ilikuwa koloni la Japan. Baada ya Japan kudhoofishwa na pigo la nyuklia katika miji ya Nagasaki na Hiroshima, lililopigwa na Marekani, Korea iligawanywa.
Marekani walichukua Kusini na Urusi Kaskazini. Na hiyo ndio ikawa sababu ya kuundwa kwa nchi mbili, Korea Kaskazini na Korea Kusini.
Mwanzo wa Vita ya Korea ni Marekani kuitangaza Korea Kaskazini kuwa iliivamia Korea Kusini, hivyo mapambano yalianza. Awali ilionekana kama Marekani isingetumia msuli mkubwa kuikabili Korea Kaskazini.
Hata hivyo, Marekani ikiwa imeweka kambi ya vita ambayo hufahamika kama Chosin Reservoir Campaign, Novemba 27, 1950, ilishambuliwa kwa kushtukizwa na China, hivyo mapigano makali yalitokea.

China iliamua kuishambulia Marekani ili kuudhoofisha mpango wake wa kuipiga Korea Kaskazini.
Mapambano hayo ambayo yalidumu kwa siku 16 kati ya China na Marekani, huitwa Battle of Chosin Reservoir. Yalianza Novemba 27 mpaka Desemba 13, 1950.
Mwaka 1955 Marekani waliamua kujitosa kwenye Vita ya Vietnam, iliyokuwa inahusisha makundi ya itikadi hasimu, Ubepari na Ukomumisti.
Marekani waliingia kusaidia kundi lililokuwa na mrengo wa Ubepari. Moto uliowaka haukuwa mdogo.
Vita ilipiganwa miaka 20 mfululizo. Hasara ambayo Marekani iliipata haiwezi kufidiwa. Hakuna ushindi uliopatikana.
Agosti 2, 1990, Marekani ikiungwa mkono na mataifa 35 duniani, ilifungua mashambulizi dhidi ya Iraq ya Saddam Hussein.
Ilikuwa baada ya Saddam kuivamia Kuwait na kusababisha mgogoro wa mafuta duniani.
Pamoja na kwamba Marekani ilifanikiwa kuikomboa Kuwait kutoka kwenye himaya ya Saddam, nguvu iliyotumika ilikuwa kubwa lakini matokeo hayakuwa rahisi. Mataifa 35 dhidi ya moja, lakini vita ilidumu miezi sita.
Kumbukumbu ya Vita ya Vietnam, Korea, Bay of Pigs na nyingine ambazo Marekani ilipata wakati mgumu ndio inayolifanya taifa hilo litafute hesabu za kuivamia Iran. Je, nchi hiyo ya Kiajemi ina silaha gani na wapo na nani? Yasije kutokea ya mwaka 1950, wanajipanga kuipiga Korea Kaskazini, wakajikuta wanapigwa na China kisha Urusi.
Hesabu hii ndio iliwapa ushindi kwa Saddam, walimkagua na kugundua hana kitu na kumwondoa.
Wamarekani hawajapata fursa ya kuikagua Iran. Wairan hawajatoa huo mwanya.
Hesabu hiyohiyo ndio inafanya Korea Kaskazini ibaki salama leo.
Mwaka 2017, Marekani walipeleka meli yao ya kivita na vifaa vyao mpaka kwenye peninsula ya Korea Kaskazini, lakini hawakuishambulia. Ni kwa sababu Marekani hawajui siri ya silaha ndani ya Korea Kaskazini.

Hesabu ya pili ambayo Marekani wanacheza nayo ni madhara. Je, wataweza kuipiga Iran bila wao kupata madhara? Na wakipigana yatakuwa kiasi gani? Vifo, majeruhi na uharibifu wa vifaa.
Siku wakipiga hesabu na kuona uwiano wa madhara ni chanya kwao, ni hakika wataipiga Iran.
Hata Korea Kaskazini. Ni hesabu tu. Mashambulizi ya Isarel nchini Iran na kuuawa viongozi wake, ipo hesabu itafutwa. Ni hesabu ya Mmarekani.