Likizo za madaktari, wauguzi wote zafutwa Iran

Tehran, Iran. Wakati mapigano kati ya Iran na Israel yakizidi kushika kasi, taarifa kutoka Iran na Gaza zimezua hofu mpya kuhusu hali ya kibinadamu na usalama wa kikanda.
Iran imeamua kuwaita kazini madaktari na wauguzi wote waliokuwa likizo, huku ikiendelea na mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Israel.
Wakati huohuo, Gaza imeshuhudia kile kinachoelezwa kuwa "mauaji mapya" dhidi ya raia waliokuwa wakitafuta misaada ya dharura.
Wahudumu wa afya waagizwa kurudi kazini mara moja.
Naibu Waziri wa Afya anayeshughulikia Huduma za Tiba, Dk Seyed Sajjad Razavi, ametangaza kufutwa kwa likizo zote za madaktari na wauguzi nchini Iran.
Amesema hatua hiyo imelenga kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa kwa ufanisi huku timu za matibabu zikipatiwa msaada wa kisaikolojia na kiakili ili kuhimili hali ya sasa ya dharura.
“Wahudumu wa afya wote wametakiwa kuwa kazini muda wote katika vituo vya afya, si tu kwa ajili ya kutoa huduma, bali pia kusaidia katika kuimarisha ari na utulivu wa kitabibu kwa wenzao walioko mstari wa mbele,” alisema Dk Razavi kupitia shirika la habari la Tasnim.
Ameongeza kuwa wizara hiyo inatoa mwongozo maalum kwa hospitali na vyuo vikuu kuhusu namna ya kuhudumia waathirika wa matukio ya vifo vya watu wengi kwa wakati mmoja. “Tuko tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika,” aliongeza kwa msisitizo.
IRGC yadokeza walipolenga
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC), makombora yao yaliyolenga Israel yamepiga kituo cha ujasusi wa kijeshi wa Jeshi la Israel pamoja na kituo cha kupanga operesheni za shirika la ujasusi la Mossad.
Taarifa hiyo, iliyonukuliwa na shirika la habari la Tasnim, inaeleza kuwa mashambulizi hayo yamelenga miundombinu ya kimkakati, ikiwa ni sehemu ya kile Iran inasema ni hatua ya kujilinda na kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Israel.
Mapema, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa kombora lililolipuka katika jiji la Herzliya — mji wa pwani ulio katikati mwa nchi hiyo — liliathiri eneo “nyeti”, dhana inayotumika mara nyingi kumaanisha kituo cha kijeshi au rasilimali ya kimkakati.
Gaza yapoteza raia zaidi
Katika Ukanda wa Gaza, taarifa za hivi karibuni kutoka kwa mashirika ya misaada zimeeleza juu ya tukio jipya la mauaji ya raia waliokuwa wakijaribu kupata misaada ya chakula na dawa.
Ingawa taarifa kamili bado hazijatolewa, picha na ushuhuda kutoka kwa walionusurika vinaonyesha hali ya kutisha inayozidi kuikumba Gaza, huku dunia ikiendelea kushuhudia janga la kibinadamu linalozidi kuota mizizi.