Iran yaishtukiza Israel, idadi waliouawa yashtua

Muktasari:
Miongoni mwa viongozi wa Iran waliouawa kwenye shambulizi la Jumamosi Juni 14, 2025, ni pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Jenerali, Hossein Salami na Jenerali, Amir Ali Hajizadeh ambaye ni Mkuu wa Programu ya utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.
Tehran. Hali bado siyo shwari kwenye mzozo kati ya Israel dhidi ya Iran kutokana na mataifa hayo kushambuliana kwa awamu, huku mamia ya raia wakiuawa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei Hamaneh, watu 70 wameuawa katika mashambulizi matatu yaliyotekelezwa na Israel katika kipindi cha saa 24 zilizopita wengi wao ni wanawake na watoto.

Hamaneh amesema mauaji hayo yanafanya idadi ya waliouawa nchini Iran kufikia 220 huku zaidi ya 200 wakijeruhiwa. Wakati huo, mashambulizi ya Iran yaliyofanyika nchini Israel yameua watu nane usiku wa kuamkia leo.
Kutokana na taarifa zinazotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz idadi ya waliouawa nchini humo ni zaidi ya watu 24 hadi kufikia leo Jumatatu Juni 16, 2025 huku 540 wakijeruhiwa.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian akihutubia taifa leo amesema pamoja na kurusha makombora zaidi ya 100 nchini Iran, taifa hilo la Kizayuni linapaswa kutambua kuwa hakuna kifo cha raia yoyote kitakachopita bila kulipwa kisasi.

“Kifo cha raia wetu mmoja kitafuatiwa na mamia watakaojitokeza kukitetea,” amesema Pazeshkian.
Amewataka raia wa taifa hilo kuungana kupingana na mashambulizi hayo ya Israel huku akisisitiza kuwa taifa hilo halitofumbia macho alichokiita udhalimu wa Israel.
Hata hivyo, Katz ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Israel amesisitiza kuwa kila shambulizi la Iran litakalopenya nchini mwake litalipwa kwa mashambulizi mengi ya kulipa kisasi.
“Iran italipa gharama ya matendo yake,” amesema Katz alipozungumza na vyombo vya habari leo asubuhi.
Kauli hiyo ya Katz imekuja muda mfupi baada ya Iran kufanya mashambulizi kwa mafanikio katika miji mitatu ya Jerusalem, Tel Aviv na Haifa yaliyosababisha vifo vya watu nane na kujeruhi zaidi ya 100.
Mzozo kati ya Israel na Iran, unatajwa kuchochewa na mashambulizi yaliyotekelezwa katika maeneo ya Gaza, Yemen na Lebanon.
Iran imekuwa ikiituhumu Israel kwa kufanya mashambulizi na kuua raia wasiyo na hatia. Pia imeituhumu Israel kwa kufanya uvamizi na kutwaa radhi ya eneo la Gaza, Palestina kimabavu.
Tangu Israel itangaze operesheni yake eneo la Gaza Oktoba 7, 2023, wapalestina zaidi ya 55, 362 wameuawa huku 128,741 wakijeruhiwa huku Waisrael 1,113 wakiuawa katika shambulizi la kushtukiza lililofanywa na kundi la Hamas.
Shambulizi hilo la kushtukiza la Hamas, ndiyo kilikuwa chanzo cha Israel chini ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kutangaza operesheni ya kijeshi dhidi ya alichokiita ni makundi ya kigaidi akilitaja Hamas na wafadhiri wake ikiwemo Iran.

Mbali na kudai kuwafifisha nguvu Hamas kwa kuwaua wapiganaji na viongozi wake na kundi la Hezbollah (Lebanon), Israel imehamishia mashambulizi yake Iran ambapo tayari imetangaza kuwaua viongozi wa kitaifa na kijeshi nchini humo.
Miongoni mwa viongozi wa Iran waliouawa kwenye shambulizi la Jumamosi Juni 14, 2025, ni pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Jenerali, Hossein Salami na Jenerali, Amir Ali Hajizadeh ambaye ni Mkuu wa Programu ya utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.
Wakati shambulizi lililowaua viongozi hao wa Iran linatekelezwa, kiongozi mkuu wa Iran Ayattolah Ali Khamenei alilazimika kufichwa kwenye ‘banker’ (chumba) maalum kisichoruhusu mashambulizi kupenya.
imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.