Mgogoro kati ya Iran na Israel wazidi kuwa mbaya

Tel Aviv, Israel. Mapigano makali ya makombora kati ya Iran na Israel yameua watu wasiopungua 10 nchini Israel na zaidi ya 78 nchini Iran, huku mamia wakijeruhiwa katika mashambulizi ya usiku wa manane yaliyozidi kwa kasi. Katika hali inayozua taharuki duniani, mzozo huu pia umechochea kwa kiwango kikubwa janga la kibinadamu Gaza, ambapo raia waliokuwa wakisubiri msaada wa chakula wameuawa kwa risasi na jeshi la Israel.

Kwa mujibu wa ‘The Guardian’ na ‘The Telegraph’, mamlaka za Israel zimethibitisha kuwa watu sita waliuawa katika mji wa Bat Yam, kusini mwa Tel Aviv, baada ya kombora kutoka Iran kulipua jengo la ghorofa nane la makazi. Zaidi ya watu 180 walijeruhiwa, huku saba wakiendelea kutafutwa chini ya kifusi. Miongoni mwa waliopoteza maisha ni watoto wawili wenye umri wa miaka minane na kumi, pamoja na wanawake wawili wazee. Aidha, watu wanne wa familia moja ya Kipalestina waliuawa katika mji wa Tamra kaskazini mwa Israel, na kufanya idadi ya vifo kufikia 10.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Kati, Daniel Hadad, ameiambia gazeti la ‘The Jerusalem Post’ la Israel kuwa "uharibifu ni mkubwa sana" na kwamba zoezi la kuwatafuta waliokwama chini ya kifusi litachukua siku kadhaa. Kombora jingine lililenga Taasisi ya Sayansi ya Weizmann mjini Tel Aviv na chuo kikuu kilichoko Rehovot.
Wakati huo huo, katika Ukanda wa Gaza, vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa wanajeshi wa Israel walifyatua risasi katika maeneo kadhaa ya usambazaji wa misaada, na kuua angalau raia watano. Kwa mujibu wa Wafa News Agency, watu watatu waliuawa katika eneo la Netzarim katikati mwa Gaza, na wengine wawili katika Khan Younis walipokuwa wakisubiri msaada. Kituo cha runinga cha Al Jazeera kimeripoti majeruhi wengine baada ya mashambulizi ya mizinga ya Israel katika eneo la Al-Tawam.

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeonya kuwa kiwango kidogo cha misaada kinachoingia Gaza hakitoshi hata kidogo, huku vizuizi vya Israel vikisababisha njaa kali kwa maelfu ya watu. Taasisi ya Gaza Humanitarian Foundation (GHF), ambayo inaratibu usambazaji wa chakula, imekosolewa vikali kwa mfumo wake unaowalazimu raia kuvuka maeneo ya mapigano ili kupata msaada.
Katika hatua ya kushangaza, jeshi la Israel lililenga Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Iran pamoja na vituo vinavyodaiwa kuhusiana na mpango wa silaha za nyuklia.
‘The Sunday Times’ la Uingereza limeripoti kuwa mashambulizi ya usiku wa manane yalifanywa na ndege za kivita za Israel dhidi ya maghala ya mafuta na maeneo ya kijeshi jijini Tehran.
Iran bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu madhara, lakini Balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Amir-Saeid Iravani, alisema watu 78 waliuawa na zaidi ya 320 kujeruhiwa katika awamu ya kwanza ya mashambulizi hayo.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya vita ya mtandaoni, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kwa lugha ya Kiarabu, Avichay Adraee, aliwataka raia wa Iran kuondoka karibu na maeneo yanayohifadhi viwanda vya kutengeneza silaha, akisisitiza kuwa wanaweka maisha yao hatarini. Hii ni mbinu ambayo hapo awali ilitumika Lebanon na Gaza lakini haijawahi kutolewa kwa Iran.
Katika hali ya sintofahamu, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa kauli kupitia mtandao wake wa Truth Social, akikanusha ushiriki wa Marekani katika mashambulizi dhidi ya Iran lakini akatishia kuwa, "iwapo tutashambuliwa kwa namna yoyote, nguvu zote za jeshi la Marekani zitashuka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa."

Mlio wa ving’ora vya droni umeenea kaskazini mwa Israel huku taharuki ikiongezeka ya kuwa huenda mzozo huu ukazihusisha nchi zaidi, kufuatia taarifa kuwa Israel imewalenga pia viongozi wa kijeshi wa kundi la Houthi. Wachambuzi wa kimataifa sasa wanatoa wito wa haraka wa mazungumzo ya kidiplomasia kabla hali haijageuka kuwa janga la kimataifa.