Mapigano Israel, Iran yazidi kuitikisa Mashariki ya Kati

Tehran, Iran. Hali ya wasiwasi imetanda Mashariki ya Kati baada ya mfululizo wa mashambulizi ya anga na makombora kati ya Israel na Iran, katika kinachoonekana kuwa moja ya machafuko makubwa zaidi ya kijeshi kwa siku za karibuni.
Kwa mujibu wa magazeti ya The Telegraph la Uingereza na 'The Wall Street Journal' la Marekani, Iran imerusha makombora ya kuelekea Israel kama kulipiza kisasi, kufuatia mashambulizi ya ghafla ya anga yaliyofanywa na Tel Aviv dhidi ya vituo vya nyuklia na makamanda wa jeshi lake, likiwamo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Katika mashambulizi hayo, viongozi wakuu wa kijeshi wa Iran waliuawa na maeneo zaidi ya 100 ya kimkakati yalilengwa, ikiwa ni pamoja na vituo vya uboreshaji wa urani na maghala ya makombora, hivyo nayo ikaamua kulipiza kisasi kwa ‘mvua ya makombora yanayorushwa na ndege zisizokuwa na marubani.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amelaani mashambulizi ya Iran akisema, “Iran imevuka mstari mwekundu kwa kushambulia maeneo ya raia.”
Taarifa ya jeshi la Israel imesema makombora mengi yalizuiliwa angani kwa msaada wa Marekani, lakini baadhi yalifaulu kupenya na kusababisha uharibifu mkubwa na vifo.
Kwa mujibu wa 'The Guardian', makombora ya Iran yamepiga maeneo ya makazi katika pwani ya kati ya Israel na kuua watu watatu, wakiwamo mwanamke wa miaka 60 na mwanamume wa miaka 45.
Takribani watu wengine 34 wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo Jumamosi Juni 14, 2025, wengi wao wakiwa na majeraha madogo, huku watu wawili zaidi wakiuawa leo asubuhi katika shambulio la moja kwa moja katikati ya Israel.
Katika mji wa Tel Aviv, ving’ora vilisikika usiku mzima huku wakazi wakikimbilia kwenye hifadhi za dharura. Saa 3 usiku, makombora ya 'Arrow' ya ulinzi wa anga yalifyatuliwa, yakizua milipuko angani na kutawanya vipande vya chuma vilivyodondoka kwenye majengo ya ghorofa, mojawapo likipiga jengo la makazi na kusababisha uharibifu mkubwa.
Vyombo vya habari vya Israel vimeonyesha askari wa uokoaji wakifanya kazi katika kifusi, karibu na mabaki ya gari lililoharibiwa kabisa.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, katika hotuba yake ya televisheni kabla ya mashambulizi hayo, aliahidi kwamba “vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu vitatoa pigo kubwa kwa adui huyu muovu.”
Mkuu mpya wa IRGC, Jenerali Mohammad Pakpour, ambaye aliteuliwa kwa dharura baada ya mtangulizi wake kuuawa, alitishia kufungua “milango ya jehanamu” dhidi ya Israel.
Iran pia iliripoti kwamba Uwanja wa Ndege wa Mehrabad mjini Tehran, ambao uko karibu na maeneo nyeti ya uongozi wa nchi hiyo na una kituo cha ndege za kijeshi, ulipigwa kwa makombora mawili. Moto mkubwa uliripotiwa katika eneo hilo, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alieleza kuwa kampeni ya kijeshi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran “bado ni mwanzo tu,” na kuonya kuwa mashambulizi zaidi yako njiani. Katika hotuba ya video, alisema: “Tumeangamiza makamanda wa juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, kituo muhimu zaidi cha uboreshaji wa urani na sehemu kubwa ya silaha zao za makombora. Wao hawajui kilichowapiga—au kinachowafuata.”
Iran, kupitia balozi wake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, ilisema watu 78, wakiwemo maofisa waandamizi, waliuawa kwenye mashambulizi ya awali ya Israel, huku wengine zaidi ya 320—wengi wao raia—wakijeruhiwa. Tehran imetaja mashambulizi hayo kama “tamko rasmi la vita.”
Kadri hali inavyoendelea kuwa tete, mlolongo wa milipuko mipya umeripotiwa Iran usiku wa kuamkia Jumamosi, ishara kuwa awamu ya pili ya mashambulizi ya Israel tayari imeanza, hali inayozidi kuongeza wasiwasi wa kuzuka kwa vita kamili visivyojulikana vitamalizika lini—vita ambavyo chimbuko lake linaweza kufuatiliwa hadi miaka 25 iliyopita wakati Iran ilipoanza kwa siri miradi ya uboreshaji wa urani chini ya ardhi, jambo lililokumbana na upinzani mkali kutoka Marekani na Israel.
Hadi sasa, hali ya wasiwasi imetanda katika miji ya Tel Aviv na Jerusalem, huku mashambulizi yakiendelea kuumiza raia wasio na hatia na mashambulizi ya kulipizana yakiashiria hatari kubwa kwa amani ya kikanda na kimataifa.