Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ilani ya ACT Wazalendo itakayokuwa

Muktasari:

  •  Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema Serikali haipaswi kuondolewa madarakani kwa kukata tamaa.

Kibondo. Chama cha ACT Wazalendo kimesema, kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya ilani yake ya uchaguzi kwa mwaka 2025/2030, kikisema itakuwa tumaini la ustawi wa kiuchumi na maisha bora kwa Watanzania.

Hatua hiyo ni mwanzo kuelekea kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kikisisitiza kukata tamaa hakujawahi kuwa silaha sahihi ya kutatua tatizo la mifumo mibovu ya utawalaz, badala yake unapaswa ujengwe mshikamano na mapambano ya haki stahiki za raia.

Sambamba na hilo, kimesema vyama vya siasa havipaswi kuwasusia watawala mchakato wa uchaguzi, bali vinapaswa kushikamana kushindana ili kujenga thamani ya kura kwa maslahi ya raia.

Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Julai 3, 2025 na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, alipohutubia mkutano wa hadhara wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 15 ya Operesheni Majimaji.

Amesema chama hicho kipo katika hatua ya mwisho ya kuandaa ilani yake ambayo anaamini ikiwekwa hadharani itakuwa tumaini jipya la ukombozi wa kiuchumi kwa Taifa.

"Tunaandaa ilani ambayo itakuwa na sera zitakazokuwa tumaini jipya la ukombozi wa kiuchumi kwa Taifa. Tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha," amesema.

Amesema chama hicho kimeamua kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kikiamini ndilo jukwaa la kuyasemea makundi mbalimbali ya Watanzania.

"Tumashiriki ili kuhakikisha tunautumia uchaguzi kama jukwaa la kumsemea Mtanzania na kueleza sera zitakazomnufaisha. Jukwaa la kumsemea bodaboda, mamalishe ambaye kila siku anakimbizwa kunyang'anywa au kudaiwa rushwa," amesema.

Amesema ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwahamasisha wananchi wajibu wao wa kupiga kura na kuzilinda ipasavyo.

"Kukata tamaa hakujawahi kuwa silaha sahihi ya kutatua tatizo lolote, zaidi ya kuhakikisha unapambana, ili kufikia haki za raia," ameeleza.

Amesema katika msimamo huo wa kushiriki uchaguzi, chama hicho kinapendekeza kufuatwa sheria katika usimamizi wa uchaguzi na mawakala wa upinzani waachwe huru kufanya kazi zao.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema kuanzishwa kwa operesheni hiyo kunalenga kuwafanya wananchi wasisalimu amri dhidi ya udhalimu unaofanywa na watawala.

Amesema matajiri wengi nchini kwa sasa ni watumishi wa Serikali, huku wananchi wakiendelea kudidimia kiuchumi.

Amesema inashangaza Halmashauri ya Kibondo yenye ardhi yenye rutuba inashindwa kukusanya mapato ya Sh2 bilioni kwa mwaka, lakini viongozi wake wanatumia magari yenye thamani kubwa.

Katika mwaka wa fedha uliopita, Kibondo ilikusanya Sh600 milioni ikiwa ni chini ya lengo ililowekewa.

Kada wa chama hicho, Emmanuel Ntobi amesema kuna umuhimu wa vyama vya upinzani kuunganisha nguvu kufanikisha kuiondoa CCM madarakani.

Amesema alipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisikia ajenda mbalimbali na hatimaye ukatoka msimamo wa kususia uchaguzi, jambo lililomfanya kubadili uamuzi na hatimaye kujiunga na ACT Wazalendo.

Ntobi amesema sio dhambi wala usaliti kuhamia chama kingine, ilimradi tu, shabaha ya kufanya hivyo iwe ni kufuata misingi ambayo pengine imepotea kutoka pale ulikokuwa.

Wakili Peter Madeleka, amesema raia wana wajibu wa kwenda kupiga kura kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu ni haki yao.

"Tunatakiwa kwenda kutimiza haki yetu ya kuwachagua viongozi tunaowataka. Ukishapiga kura yako Oktoba, hakikisha unailinda," amesema.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, amesema ni uchaguzi ndiyo mchakato unaomwezesha mwananchi apate kiongozi anayemtaka.

Ameeleza ni muhimu kuhakikisha wanapatikana viongozi watakaoweza kusimama mbele ya wananchi na anapaza sauti kuiambia mamlaka husika kwamba kuna changamoto fulani.