Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zitto: ACT Wazalendo tunashiriki uchaguzi kwa masilahi ya Watanzania

Muktasari:

  • Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini ameeleza hayo leo Jumatano Julai 2, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa sekondari ya Uyui mjini hapa. Mkutano ni sehemu ya ziara ya viongozi wakuu wa chama hicho iliyopewa jina 'operesheni majimaji linda kura yako'

Tabora. Kiongozi wa zamani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kitashiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa masilahi ya Watanzania na si kwa kuiamini Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Amesema ACT Wazalendo, kinawapenda na kuwajali Watanzania na viongozi wake wanaamini nguvu ya wananchi kwenye upigaji kura.

Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, ameeleza hayo leo Jumatano Julai 2, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sekondari ya Uyui mjini Tabora.

Mkutano ni sehemu ya ziara ya viongozi wakuu wa chama hicho iliyopewa jina 'operesheni majimaji linda kura yako.'

Operesheni majimaji linda kura yako itadumu kwa siku 30 kwa viongozi wakuu wa ACT Wazalendo kujigawa katika mikoa kwa ajili ziara ambayo imejikita kuvuna wanachama wapya.

Katika mkutano huo, Zitto amewaambia Watanzania na wananchi wa Tabora, kuwa ACT Wazalendo kinashiriki mapambano ili kupigania thamani ya kura yao kwa lengo la kuiondoa CCM madarakani, ambayo amedai kikwazo cha maendeleo nchini.

"Tupo katika operesheni majimaji, kampeni maalumu ya kuwaamsha Watanzania kurejesha thamani ya kura zao. Tabora ni moja ya miji mingi tunayozuru ili kuunganisha Watanzania kuhakikisha kuwa Oktoba 2025 thamani ya kura inarudi.

"Uamuzi wa ACT Wazalendo kushiriki uchaguzi wa 2025 badala ya kususia haukuwa uamuzi rahisi, lakini ulikuwa wa muhimu. Ni uamuzi uliozingatia hali yetu halisi, yakichukua mifano ya mapambano ya kimataifa 'uamuzi wa busara kama yalivyokuwa mwaka 1958 hapa Tabora," amesema Zitto.

"Hapa Tanzania tumejifunza Zanzibar, mwaka 2015 CUF ilisusa na CCM haikujali na uchaguzi ulirudiwa. ACT Wazalendo tunasema miaka mitano ijayo ya Bunge la chama kimoja hatuwezi kuruhusu hilo," amesema Zitto.

Zitto, amesema kuingia kwenye uchaguzi kutachangia baadhi ya kata na majimbo yatakwenda upinzani, badala ya kukaa kando na kuwanufaisha CCM.

"Inawezekana katika majimbo zaidi ya 200 tusipate majimbo yote lakini angalau tutapata machache yatakayogeuza Bunge la chama kimoja kama lililopita. Tunataka kujenga Bunge liwe la uwajibikaji ili kuleta hali bora ya maisha ya Watanzania," amesema Zitto.

Katika hatua nyingine, Zitto amesema Tabora ni miongoni mwa mikoa sita ambayo inakabiliwa na changamoto ya umaskini, amedai hali hiyo inasababishwa na sera za chama kilichopo madarakani ndio maana ACT Wazalendo imechukua jukumu kushiriki uchaguzi ili kukabiliana nacho.

"Leo nimesimama mbele yenu kwa moyo uliojaa shauku, imani na azma ya kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi yetu ya Tanzania.

"Nimerudi tena Tabora, kama nilivyofanya mara nyingi kwa miaka mingi, si tu kwa sababu ni njia ya kwenda na kutoka nyumbani kwangu Kigoma, bali ni mji wa asili wa mapambano ya ukombozi," amesema.

Jana Jumanne, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita aliyekuwa Kigoma kwa ziara hiyohiyo, alisema kususia uchaguzi si mbinu stahiki ya kukabili ukiukwaji haki na sheria wowote unaofanywa nchini, badala yake kunahitajika ushirikiano na mshikamano katika harakati za kufanikisha mapambano hayo.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Janeth Rithe amesema kukataa kushiriki uchaguzi maana yake chama hicho kimeshindwa kutatua changamoto za wananchi ikiwemo mikopo ya kausha damu.

"Tunataka kufanya mabadiliko ndani ya Tanzania, hatuikimbii hii vita (uchaguzi mkuu) msikubali kudanganyika hasa wanawake. Tumechoka kuchagua viongozi wasiowajibika, twendeni kwenye uchaguzi tukafanye mabadiliko ACT Wazalendo ndio mbadala wenu," amesema Rithe.