ACT-Wazalendo kuja na 'Operesheni Majimaji'

Muktasari:
- Viongozi wa ACT -Wazalendo kugawana mikoa ya Tanzania tayari kuanza 'Operesheni Majimaji'
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza kuja na kampeni ya 'Operesheni Majimaji' yenye lengo la kuwaamsha Watanzania kurejesha thamani ya kura zao.
Operesheni hiyo inakuja wakati ikiwa imebaki miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, wabunge na Madiwani hapo Oktoba, 2025.
Akizungumza leo Jumapili, Juni 29, 2025, makao Makuu ya Chama hicho Magomeni Dar es Salaam, Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Shangwe Ayo amesema itachukua siku 15 kuanzia Julai mosi.
"Kama ambavyo wazee wetu walivyounganisha Watanganyika kupambana na mkoloni kwenye vita vya Majimaji, ndivyo ambavyo ACT- Wazalendo inafanya kazi ya kuunganisha makundi yote ya jamii katika kulinda demokrasia yetu kwa kuhakikisha thamani ya kura inalindwa ifikapo Oktoba 2025," amesema Shangwe.
Akielezea ziara ya operesheni majimaji, amesema itafanyika nchi nzima huku ikiongozwa na viongozi wa chama hicho akiwamo Zitto Kabwe, Dorothy Semu, Isihaka Mchinjita.
"Kiongozi wa chama,Dorothy Semu pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara Isihaka Mchinjita wataongoza msafara utaokwenda katika majimbo yaliyopo mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam.
"Katika msafara huo wataambatana pia na Naibu Katibu Mwenezi Taifa na Waziri Kivuli, Shangwe Ayo, Mwenyekiti wa Vijana Taifa Abdul Nondo, Mwenyekiti wa Mkoa wa Kigoma na Waziri Kivuli wa Fedha, Kiza Mayeye, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Peter Madeleka na Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Emmanuel Ntobi," amesema.
Aidha, kiongozi wa chama mstaafu Zitto na Naibu Katibu Mkuu Bara, Ester Thomas wataongoza msafara utaokwenda kwenye majimbo yaliyopo kwenye mikoa ya Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Selous, Mtwara, Lindi na Mwambao.
Amesema, katika msafara huo wataambatana na Mwenyekiti wa Wanawake Taifa Janeth Rithe, Waziri Kivuli Nishati, Mbarala Maharagande, Kada wa chama, Maftaha Nachuma na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Halima Nabalang'anya.
Amesema kwenye ziara hiyo, mbali na mikutano ya hadhara, viongozi watafanya vikao vya ndani vitavyojumuisha wajumbe wa mikutano mikuu (viongozi wa majimbo na kata zote) pamoja na watiania wa ubunge na udiwani.
ACT Wazalendo wanatarajia kuanza ziara hiyo wakati wakiendelea kupokea wanachama wapya akiwamo Naghenjwa Kaboyoka aliyekuwa kada wa zamani wa Chadema, Sheikh Ponda Issa Ponda, Emmanuel Ntobi, Grory Taus(Chadema) Maftaha Nachuma aliyewahia kuwa makamu mwenyekiti wa CUF (bara) na mbunge wa zamani wa Mtwara Mjini.