Kaboyoka: Nimekuja ACT Wazalendo na watu, tutaishangaza dunia Oktoba 2025

Muktasari:
- Kaboyoka aliyejiunga na ACT Wazalendo alikuwa ni miongoni mwa wabunge 19 wa Viti Maalumu walioingia kwenye mvutano na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) siku chache baada ya kuapishwa.
Dar es Salaam. Bado Tunaendelea na usajili wa vigogo, hii ndio kauli iliyotamkwa na viongozi wa ACT Wazalendo. Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya kumkabidhi kadi ya uanachama Naghenjwa Kaboyoka aliyekuwa kada wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kaboyoka anaungana na makada wapya wa ACT Wazalendo, Sheikh Ponda Issa Ponda, Emmanuel Ntobi, Grory Taus (Chadema) Maftaha Nachuma aliyewahia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara na mbunge wa zamani wa Mtwara Mjini.
Kada huyo mpya alikuwa ni miongoni mwa wabunge 19 walioingia kwenye mvutano na Chadema, kwa kile kilichodaiwa kuwa waliapishwa bila ridhaa ya chama hicho.

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu (kulia) akimkabidi kadi ya Chama Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu na kada wa zamani wa Chadema, Naghenjwa Kaboyoka ( kushoto) katika ofisi za chama jijini Dar es Salaam leo.Picha na Sunday George
Kaboyoka, ambaye alikuwa ni Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa miaka 10, amejiunga na ACT Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu leo Jumamosi Juni 28, 2025.
Baada ya kukabidhiwa fomu, Kaboyoka amesema uamuzi wa kujiunga na ACT Wazalendo, una baraka zote za wananchi wanaomuunga mkono tangu akiwa Chadema.
“Nimejiunga ACT Wazalendo sipo peke yangu nipo asilimia kubwa na watu, wakiwemo waliokuwa madiwani wanaoniunga mkono na tupo pamoja na 'mama'.

“Nimekuja kikamilifu ACT-Wazalendo sikuja kimchezo mchezo, nimekuja na mengi yatakayotufanya kujua tunakwenda wapi na namna ya kwenda huko,” amesema Kaboyoka aliyewahi kuwa mbunge wa Same Mashariki mwaka 2015/2020.
Amesema yeye ni mtu mwenye adabu na heshima ndio maana alivyokuwa akiitwa Covid- 19 hakuwa akijibu bali alikaa kimya na amefurahi kujiunga chama chenye adabu kinachopigania maslahi ya wote.
Sababu za kujiunga ACT Wazalendo
Katika maelezo yake, Kaboyoka amesema amejiunga na ACT Wazalendo kwa sababu ndio chama kilichojiandaa kushika dola, akiwashukuru viongozi wa chama hicho kwa kumpokea.

“Nawashuruku ACT Wazalendo, hawakususia uchaguzi, kimefanya uamuzi mzuri wa haki wa kupambana ndani kwa ndani ili watu wauze sera. Naamini Oktoba 2025 tutaishangaza dunia, nimeingia ACT kwa sababu ndio chama kitakachowatoa wananchi,” amesema Kaboyoka.
Kwa upande wake, Semu amesema: “Leo ni siku ya mama Kaboyoka, ambaye ni kiongozi wa mfano, mwanamke shujaa na mtumishi wa umma.

“Kwa miaka kadhaa wengi wamemfahamu Mama Kaboyoka kama kiongozi aliyejijengea heshima, kwa kuwa kiongozi mahiri, msema kweli, mchapakazi na anayesimamia misingi ya uwajibikaji pamoja na maslahi ya wananchi,” amesema Semu.
Semu amesema Kaboyoka akiwa bungeni alisimama imara kama sauti ya wananchi, akikemea uovu na kusisitiza utawala wa sheria na hakuwa kuyumbishwa na hofu wala vishawishi.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (Bara), Ester Thomas amesema chama hicho hivi sasa kimekuwa kimbilio la watu ndio maana kinafanya usajili mbalimbali kwa makada wapya.