Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Israel yashambulia Iran, yajiandaa kwa hatua za kisasi

Muktasari:

  • Israel imefanya shambulio la anga nchini Iran, ambapo Brigedia Jenerali Mohammad Bagheri ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Iran na kiongozi wa pili kwa mamlaka baada ya Ayatollah Ali Khamenei, ameuawa.

Tel Aviv, Israel. Jeshi la Israel limetekeleza mashambulizi kadhaa ya anga ndani ya Iran na kuwaua makamanda wawili waandamizi wa jeshi la Iran, kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la Israel na vyombo vya habari vya taifa hilo la Kiislamu.

Katika mkutano na waandishi wa habari, ofisa mwandamizi wa jeshi la Israel amesema kuwa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel yalilenga maeneo ya nyuklia nchini Iran.

Amedai kuwa Iran inatekeleza mpango wa siri wa kutengeneza bomu la nyuklia, hatua ambayo Israel inaiona kama tishio kwa usalama wake na kwa eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Katika mkutano wa waandishi wa habari uliowahusisha wanahabari, ofisa mmoja wa jeshi la Israel alieleza kuwa jeshi la anga la Israel lilikuwa likilenga maeneo ya nyuklia ya Iran, likiituhumu Tehran kuendesha mpango wa siri wa kutengeneza bomu la nyuklia.

Ripoti kadhaa kutoka Tehran zimeripoti milipuko mikubwa kusikika kaskazini-mashariki mwa mji mkuu huo wa Iran.

Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa Brigedia Jenerali Mohammad Bagheri, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Iran na mtu wa pili kwa mamlaka baada ya Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, ameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Israel.

Aidha, televisheni hiyo imesema kuwa Israel ililenga makao makuu ya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Revolutionary Guards) jijini Tehran, na kumuua Kamanda Hossein Salami. Kikosi hicho kina ushawishi mkubwa kijeshi na kisiasa ndani ya Iran, na ni miongoni mwa mihimili mikuu ya ulinzi wa taifa hilo.

Vyombo vya habari vya Serikali ya Iran pia vimeripoti kuwa ndege zote katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini jijini Tehran zimesitishwa.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa majeshi ya Iran, Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, ametahadharisha kuwa Israel na Marekani ‘watalipa gharama kubwa’ kwa mashambulizi hayo.

Mapema alfajiri, ving’ora vya tahadhari vilisikika katika maeneo mbalimbali ya Israel.

Ofisa mmoja wa jeshi la Israel ameliambia Shirika la NPR kuwa vilikuwa ni ving’ora vya tahadhari ya awali. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alitangaza hali maalum ya dharura kote nchini, akisema taifa hilo lijiandae kwa mashambulizi ya makombora na droni.

Katika ujumbe wa video alioweka kwenye mitandao ya kijamii, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa operesheni hiyo iliyopewa jina la ‘Rising Lion’ imepiga “moyo wa programu ya nyuklia ya Iran” na itaendelea kwa muda wote utakaohitajika.

“Ni wazi kuwa Iran inachelewesha kwa makusudi. Inakataa kabisa kutii masharti ya msingi ya mataifa yenye kupenda amani. Ndiyo maana hatuna budi kuchukua hatua  na kuchukua hatua sasa,” amesisitiza Netanyahu.

Habari za mashambulizi haya zilitetemesha masoko ya kimataifa, bei ya mafuta ilipanda kwa karibu asilimia 12, huku hisa za Marekani zikiporomoka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ametoa taarifa akieleza kuwa majeshi ya Marekani hayakuhusika kwenye mashambulizi hayo.

“Israel ilitujulisha kuwa waliamini hatua hii ilikuwa muhimu kwa ajili ya kujilinda. Rais Trump (Donald) pamoja na Serikali yake wamechukua hatua zote za kulinda wanajeshi wetu, na tuko katika mawasiliano ya karibu na washirika wetu wa kikanda. Hebu niseme wazi: Iran isithubutu kushambulia maslahi au watu wa Marekani,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hii ilikuja saa chache tu baada ya Rais Trump kutoa onyo kuwa shambulio dhidi ya Iran lingeweza kutokea wakati wowote.

“Ni rahisi tu, halihitaji ufafanuzi. Iran haiwezi kuruhusiwa kuwa na silaha ya nyuklia. Zaidi ya hapo, natamani waendelee vizuri. Natamani wawe wa kipekee. Tutawasaidia kufanikisha hayo,” alisema Trump, ambaye alikuwa ameonya kuwa iwapo mazungumzo na Iran yangeshindwa kuzuia mpango wake wa nyuklia, basi hatua za kijeshi zingechukuliwa.

Mjumbe wake wa Mashariki ya Kati, Steven Witkoff, alikuwa amepangwa kukutana na wajumbe wa Iran nchini Oman siku ya Jumapili.