Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Idd ya majonzi Gaza, mashambulizi ya Israel yaua 64

Muktasari:

  • Mashambulizi ya anga ya Israeli yaua makumi ya watu Gaza huku Wapalestina wakisherehekea Idd el-Fitr huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akisisitiza Hamas iweke silaha chini na viongozi wake waondoke Gaza.

Gaza. Mashambulizi ya Jeshi la Israel (IDF) katika Ukanda wa Gaza yameendelea katika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Idd na kusababisha vifo vya watu 64, wakiwemo watoto.

Wakati IDF ikitekeleza mashambulizi hayo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameonya kutokuwa na nia ya kupunguza mashambulizi dhidi Hamas, wakati mazungumzo mapya ya kusitisha mapigano yakiendelea nchini Misri.

Mashambulizi kadhaa ya anga katika saa za asubuhi za Jumapili na Jumatatu yamelenga mahema na nyumba huku wananchi wakisherehekea Sikukuu ya Idd el-Fitr.

Shirika la Msalaba Mwekundu limeieleza Al Jazeera kuwa watu 64 wameuawa katika miji ya Kusini mwa Gaza ya Rafah na Khan Younis.

Mauaji hayo yanatokea wakati Shirika la Msalaba Mwekundu la Palestina (PRCS) likipata miili ya wahudumu wa afya 15, waliouawa kwenye mashambulizi makali ya Israel huko Rafah, wiki iliyopita.

Kitengo cha uthibitishaji wa habari cha Al Jazeera, Sanad kimepata picha za setilaiti zinazoonyesha kuwa magari matano ya uokoaji yaliharibiwa na Jeshi la Israel katika mashambulizi hiyo.

“Hili ni janga si kwetu tu bali pia kwa kazi ya kibinadamu na ubinadamu,” PRCS imesema katika taarifa yake, ikiongeza kuwa kushambuliwa kwa wahudumu wa afya na Jeshi la Israel, hakuwezi kuchukuliwa kawaida isipokuwa ni uhalifu wa kivita.


Katikati ya machafuko hayo, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza nchini Palestina inazidi kuzorota kwani Israel imesitisha usambazaji wa misaada tangu mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

“Wapalestina wanapaswa kuvunja swaumu yao kwa mlo mzuri kwa ajili ya Idd, lakini leo hawawezi hata kupata mlo mmoja, ni hali mbaya sana Gaza,” amesema mwandishi wa Al Jazeera, Hind Khoudary, akiripoti kutoka Deir el-Balah.

“Chakula katika Ukanda wa Gaza ni adimu na ghali sana, huku wazazi wakisema kulisha familia zao ni “kazi isiyowezekana,” amesema Khoudary.

Wakati huohuo, matumaini ya mafanikio katika mazungumzo ya kusitisha mapigano yanazidi kufifia kwa pande zote.

Jumapili, Netanyahu alisisitiza tena madai yake kwamba Hamas iweke silaha chini na viongozi wake waondoke Gaza, huku akiahidi kuongeza shinikizo kwa kundi hilo ili kuwaachilia mateka 59 waliobaki, 35 wanahofiwa kuwa wamekufa.

Hiyo ni sehemu ya masharti mpya yaliyowekwa na Israel, kwa msaada wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambayo yanatarajiwa kurekebisha masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya hatua tatu yaliyosainiwa Januari.

Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, baada ya kundi la kwanza la mateka kuachiliwa kila wiki, pande zote mbili zilipaswa kuingia katika awamu ya pili ya mazungumzo kujadili kumalizika kwa vita, kuachiwa kwa mateka waliobaki, na kuondolewa kwa wanajeshi wa Israeli kutoka Gaza.

Lakini Israel inasisitiza kuwa Hamas inapaswa kuwaachilia mateka wote bila Israel kujitolea kumaliza vita.

Kwa kuwa Hamas inakataa madai hayo mapya, Israel imeanza tena mashambulizi ya anga na kuhamisha wanajeshi ndani ya eneo la Gaza.

Jumapili, Netanyahu pia amesema Israel itafanya kazi kutekeleza mpango wa uhamiaji wa hiari wa Trump kwa Gaza na kuongeza kuwa baraza lake la mawaziri limekubaliana kuendelea kuiwekea Hamas shinikizo, hata baada ya kundi hilo kusema limekubali pendekezo jipya la usitishaji mapigano kutoka kwa wasuluhishi Misri na Qatar.

Ofisa Mwandamizi wa Hamas, Sami Abu Zuhri, amesema matamshi ya Netanyahu ni mpango wa kuongeza mgogoro bila kikomo katika eneo hilo.

Netanyahu amekanusha madai kwamba Israel haishiriki katika mazungumzo, akisema: “Tunayaendesha chini ya mashambulizi, na kwa hivyo yanakuwa na ufanisi.”

“Tunaona kuna nyufa ghafla,” amesema katika taarifa ya video iliyotolewa leo Jumatatu Machi 31, 2025.

Kiongozi wa Hamas huko Gaza, Khalil al-Hayya, amesema kundi hilo limekubali pendekezo ambalo vyanzo vya usalama vilisema linajumuisha kuachiliwa kwa mateka watano wa Israel kila wiki.

Jumuiya ya Msalaba Mwekundu tayari imepata miili ya wahudumu wa afya wanane, wafanyakazi wa ulinzi wa raia watano na mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa, wiki moja baada ya magari yao kushambuliwa na karibu na Rafah, kusini mwa Gaza.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC) limelaani mauaji hayo, likisema tukio hilo linaleta maafa na ni shambulio baya zaidi dhidi ya wafanyakazi wake duniani kote, tangu mwaka 2017.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema Wapalestina wasiopungua 50, 277 wamethibitishwa kuuawa na wengine 114,095 wamejeruhiwa katika vita vya Israeli dhidi ya Gaza.

Hata hivyo, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Gaza ilisahihisha idadi ya vifo takriban miezi miwili iliyopita na kusema kuwa zaidi ya watu 61,700 wameuawa, huku maelfu ya waliopotea chini ya vifusi wakihofiwa kuwa wamefariki.

Takriban watu 1,139 waliuawa Israel wakati wa mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas Oktoba 7, 2023, na zaidi ya 200 walichukuliwa mateka.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaasa wa Mashirika ya Habari.