Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Israel yashambulia zaidi Tehran, Trump aonya

Muktasari:

  •  Israel inaonekana kupanua zaidi mashambulizi yake ya angani dhidi ya Tehran siku tano baada ya shambulio la ghafla dhidi ya majeshi na miundombinu ya nyuklia ya Iran, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiandika ujumbe mzito akiwataka wakazi wa jiji hilo kuhama mara moja.

Tehran. Israel inaonekana kupanua zaidi mashambulizi yake ya angani dhidi ya Tehran siku tano baada ya shambulio la ghafla dhidi ya majeshi na miundombinu ya nyuklia ya Iran, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiandika ujumbe mzito akiwataka wakazi wa jiji hilo kuhama mara moja.

“Iran haiwezi kumiliki silaha ya nyuklia,” Trump aliandika jana usiku kabla ya kuondoka mapema kutoka katika mkutano wa viongozi wa G7 uliofanyika Canada na kurejea Washington. “Kila mtu anapaswa kuondoka Tehran mara moja!” aliongeza.

Baadaye Trump alikanusha taarifa kwamba alirudi mapema ili kushiriki kwenye mpango wa usitishaji mapigano, akisisitiza kuwa kuondoka kwake hakuhusiani na mpango wowote wa usitishaji mapigano. Kuna jambo kubwa zaidi,” alieleza bila kufafanua ni jambo gani.

Mapema leo, jeshi la Israel limetoa agizo la kuwahamisha wakazi takriban 330,000 kutoka eneo la kati la jiji la Tehran.

Tehran ni mojawapo ya miji mikubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, ikiwa na watu wapatao milioni 10, idadi inayokaribia kulingana na idadi ya raia wote wa Israel. Tangu mashambulizi yaanze, wakazi wengi wamekuwa wakikimbia.

Israel inadai kuwa mashambulizi hayo makubwa dhidi ya viongozi wa kijeshi wa Iran, wanasayansi wa nyuklia, maeneo ya kurutubisha urani na mpango wa makombora ya masafa marefu ni hatua ya kuzuia adui wake wa muda mrefu kujiandaa na utengenezaji wa bomu la nyuklia. Kufikia sasa, watu wasiopungua 224 wamepoteza maisha tangu Ijumaa iliyopita.

Kwa upande wake, Iran imelipiza kisasi kwa kurusha makombora zaidi ya 370 na kutumia mamia ya ndege zisizo na rubani kuelekea Israel.

Hadi sasa, watu 24 wameuawa nchini Israel na zaidi ya 500 kujeruhiwa. Jeshi la Israel limesema wimbi jipya la makombora limerushwa leo Jumanne Juni 17,2025, huku milipuko ikisikika kaskazini mwa Israel.


Shughuli zafungwa, misururu ya mafuta Tehran

Leo asubuhi, maeneo ya katikati mwa Tehran yameonekana kuanza kuwa tupu, maduka mengi yakiwa yamefungwa. Soko kuu la kihistoria la Grand Bazaar pia limefungwa  jambo linalotokea mara chache hususan wakati wa maandamano au mlipuko wa janga kama Uviko-19.

Barabarani, hasa kuelekea magharibi mwa Tehran, magari yamejazana bila kusogea. Wengi wanaonekana kuelekea ukanda wa Bahari ya Kaspi. Vituo vya mafuta vimekuwa na misururu mirefu.

Wakati hayo yakijiri, viongozi wa serikali ya Iran waliendelea kutangaza kuwa hali ipo shwari, bila kutoa mwongozo wowote rasmi kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua.

Kwa upande wa Israel, jeshi lake limedai kumuua jenerali mkuu wa Iran katika shambulio la angani mjini Tehran.

Iran haijatoa tamko rasmi juu ya kuuawa kwa Jenerali Ali Shadmani, aliyeteuliwa hivi karibuni kuongoza Makao Makuu ya Kati ya Khatam al-Anbiya, sehemu ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran.

Iran tayari imeshateua makamanda wapya kuchukua nafasi za waliouawa katika mashambulizi ya awali.


Trump aondoka G7 mapema kwa lengo la kushughulikia mgogoro

Kabla ya kuondoka Canada, Trump alijiunga na viongozi wengine kutoa tamko la pamoja kwamba Iran haiwezi kuruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia na wakataka kupunguzwa kwa chuki na mapigano Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na kusitisha mapigano Gaza.”

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran yalikuwa yanaendelea, lakini Trump alionekana kuyapinga katika chapisho lake la usiku.

“Macron alikosea kusema kwamba nimeondoka mkutano wa G7 kwenda (Washington) D.C. kushughulikia mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran,” Trump aliandika. “Si kweli! Hana habari yoyote kwa nini naelekea Washington sasa, ila ni jambo kubwa zaidi ya hilo.”

Wakati huohuo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alielekea katika chumba cha dharura cha Ikulu ya Marekani kwa kikao na rais na timu yake ya usalama wa taifa.

Hegseth hakutoa maelezo kamili kuhusu sababu ya mkutano huo, lakini aliliambia shirika la Habari la Fox News kuwa hatua hizo ni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa watu wao.


Israel yadokeza inadhibiti  anga la Tehran

Msemaji wa jeshi la Israel, Brigedia Jenerali Effie Defrin, jana alisema kuwa vikosi vyao vimepata udhibiti kamili wa anga ya Tehran.

Jeshi hilo lilisema limeharibu zaidi ya makombora 120 ya ardhini, sawa na theluthi moja ya makombora ya Iran, yakiwamo mengi yaliyokuwa tayari kurushwa kuelekea Israel.

Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa, Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, Rais wa Marekani Donald Trump, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen walipiga picha ya pamoja ya ukumbusho wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Kundi la Nchi Saba (G7), uliofanyika Kananaskis, Alberta, Canada, jana, Juni 16, 2025. (Picha kwa hisani ya REUTERS)

Hata hivyo, ndege mbili aina ya F-14 zilizotumiwa na Iran kulenga ndege za kivita za Israel ziliharibiwa.

Vilevile, ndege za kivita za Israel zimeripotiwa kushambulia vituo 10 vya kamandi vya Kikosi cha Quds kilicho chini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, tawi maalumu linalojihusisha na operesheni za kijeshi na kiintelijensia nje ya Iran.

Israel imetoa tahadhari ya kuhamishwa kwa wakazi wa eneo la kati mwa Tehran linalojumuisha makao ya televisheni ya taifa, makao makuu ya polisi na hospitali tatu kubwa mojawapo ikiwa ya Jeshi la Walinzi. Tahadhari kama hiyo ilitolewa pia kwa baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Gaza na Lebanon kabla ya mashambulizi.

Wizara ya Afya ya Iran imeripoti watu 1,277 wamejeruhiwa.

Mashirika ya haki za binadamu kama Human Rights Activists yenye makao yake Marekani yamesema idadi ya waliouawa ni kubwa kuliko inayotolewa na serikali. Wameeleza kuwa wamebaini vifo vya watu zaidi ya 400, wakiwemo raia 197.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema mashambulizi ya Israel yamechelewesha mpango wa nyuklia wa Iran kwa muda mrefu sana na akasisitiza kuwa anawasiliana kila siku na Trump.

Iran imeshikilia kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani, huku Marekani na mataifa mengine yakisema hakuna dalili kuwa Iran imekuwa na mpango ulioandaliwa wa kutengeneza silaha ya nyuklia tangu 2003.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) amewaonya mara kadhaa kuwa Iran ina urani ya kutosha kwa ajili ya kutengeneza mabomu kadhaa ya nyuklia endapo itachukua uamuzi huo.

Mpaka sasa, Israel imefanikiwa kushambulia maeneo kadhaa ya nyuklia ya Iran lakini haijafanikiwa kuliharibu kabisa eneo la Fordo, mojawapo ya vituo vya kurutubisha urani vya chini ya ardhi.

Kituo hicho kimejengwa chini kabisa ya ardhi na ili kukiharibu, Israel huenda ikahitaji bomu maalumu la GBU-57 la Marekani lenye uzito wa tani 14 linalotumika kupenya ardhi kwa nguvu ya msukumo.

Israel haina bomu hilo wala ndege maalumu ya kulitupa. Kwa sasa, bomu hilo hutumika kwa ndege ya kivita ya Marekani aina ya B-2 stealth bomber.


Mgogoro hauoneshi dalili ya kumalizika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alitoa kauli ya moja kwa moja kana kwamba anatoa ombi la Marekani kuingilia kati kurejesha mazungumzo.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X, Araghchi aliandika kwamba kama Trump ana nia ya kweli ya kidiplomasia na anataka kusitisha vita hivi, basi hatua zinazofuata ni muhimu sana.”

“Simu moja tu kutoka Washington inaweza kumtuliza Netanyahu,” aliandika. “Huenda ikafungua njia ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.”

Ujumbe huo ulitumwa wakati mazungumzo mapya kati ya Iran na Marekani yalikuwa yameahirishwa mwishoni mwa wiki baada ya mashambulizi ya ghafla ya Israel.

Juzi Jumapili, Araghchi alisema Iran ipo tayari kusitisha mashambulizi yake ikiwa Israel nayo itafanya hivyo.