Israel italazimika kufanya haya, kulipua Fordow

Muktasari:
Kwa mtazamo wake, ikiwa vita dhidi ya Iran vitamalizika sasa, basi Israel haitapata chochote. Ameeleza kuwa nchi yake haiwezi kujikomboa peke yake dhidi ya miundombinu yenye nguvu ya kijeshi na nyuklia ya Iran bila msaada wa nje.
Tel Aviv, Israel. Alon Pinkas, aliyewahi kuwa mwanadiplomasia wa Israel na kwa sasa ni mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia, anaeleza kuwa dhamira ya Israel ya kuondoa tishio la Iran haitafanikiwa bila usaidizi wa Marekani.
“Iwapo Israel itafanikiwa, basi mafanikio hayo yatatokana na Marekani; kama hilo litatimia au la, bado hatujui. Rais Trump anazungumza mambo yanayokinzana kila siku,” Pinkas alifafanua katika mahojiano na Al Jazeera.

Kwa mtazamo wake, ikiwa vita dhidi ya Iran vitamalizika sasa, basi Israel haitapata chochote. Ameeleza kuwa nchi yake haiwezi kujikomboa peke yake dhidi ya miundombinu yenye nguvu ya kijeshi na nyuklia ya Iran bila msaada wa nje.
“Israel peke yake haiwezi kuharibu miundombinu ya nyuklia ya Iran. Hilo linahitaji silaha nzito na mfumo maalumu wa kusafirisha bomu mambo ambayo Israel haina, na ndiyo maana Netanyahu anashinikiza na kushawishi kuihusisha Marekani moja kwa moja kwenye mgogoro huu.”
Pinkas amesema lengo kuu la mashambulizi ya Israel ni kulipua kituo cha Fordow ambacho ni kikubwa cha kurutubisha urani kilichopo chini ya ardhi kusini mwa Tehran.
“Wanausalama wa Israel wanatamani kwa dhati Marekani iingie vitani ili washiriki katika awamu ya mwisho ya mashambulizi, lakini pia wanatambua kuwa jambo hilo linaweza lisitekelezeke,” aliongeza.
Historia ya kituo cha nyuklia cha Fordow
Kituo cha Fordow (Fordow Fuel Enrichment Plant – FFEP) kimejengwa chini ya ardhi, kilomita 30 kaskazini-mashariki mwa Qom, Iran. Kikiwa katika eneo la zamani la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kituo hiki kinaendeshwa na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) na ni kituo cha pili kwa ukubwa nchini humo baada ya kile cha Natanz.
Iran ilikizindua rasmi Septemba 21, 2009, ingawa baadaye kiligunduliwa na mashirika ya kijasusi ya Magharibi. Serikali ya Iran ilijitetea kwamba uanzishaji wa kituo hicho ulikuwa ndani ya misingi ya mkataba wa ulinzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), unaozitaka nchi wanachama kutangaza vituo vipya vya nyuklia siku 180 kabla ya kuanza kufanya kazi rasmi.
Makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yaliweka masharti ya kukifanya kituo cha Fordow kuwa kidogo cha utafiti. Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, hali ya sasa inaashiria mabadiliko tofauti na makubaliano hayo.
Changamoto za kulipua Fordow
Hadi sasa, Israel imekuwa ikilenga maeneo mbalimbali ya miundombinu ya mpango wa nyuklia wa Iran, lakini bado haijafanikiwa kukiteketeza kituo hicho nyeti cha kurutubisha urani.
Kituo cha Fordow kimefukiwa ndani ya ardhi kwa kina kikubwa kiasi kwamba ili kukiteketeza itahitajika silaha ya aina ya GBU-57, inayojulikana kama ‘Massive Ordnance Penetrator’ – bomu lenye uzito wa kilo 13,600 (zaidi ya tani 13). Bomu hili lina uwezo wa kupenya ardhini kwa kasi kubwa kwa kutumia uzito wake na nguvu ya asili ya msukumo, kabla ya kulipuka ndani kabisa ya lengo lililojificha ardhini.
Lakini kwa sasa, Israel haina uwezo wa kubeba wala kurusha bomu hilo zito. Silaha hiyo inaweza tu kurushwa na ndege ya kivita ya Marekani aina ya ‘B-2 stealth bomber’, iliyoundwa kwa teknolojia ya hali ya juu ya kuficha mwonekano wake kwenye rada.
Kwa mujibu wa kampuni ya kutengeneza ndege hiyo, ‘Northrop Grumman’, ina uwezo wa kubeba hadi kilo 18,000 (sawa na tani 18).
Zaidi ya hapo, Jeshi la Anga la Marekani limeshatangaza kuwa limefanikiwa kufanya jaribio la kubeba mabomu mawili ya GBU-57 A/B kwa pamoja ambao ni mzigo wa takribani kilo 27,200.
Ndege hiyo ya kivita, inayotambulika pia kama ‘mbebaji wa mizigo mizito kwa safari za masafa marefu’, ina uwezo wa kusafiri umbali wa hadi kilomita 11,000 (sawa na maili 7,000) bila kujaza mafuta, na inaweza kufika sehemu yoyote duniani kwa muda mfupi, kwa mujibu wa taarifa rasmi za Northrop Grumman.
Kwa sasa, changamoto ya kulipua kituo cha Fordow inasalia kuwa kubwa kwa Israel, na suluhisho linaonekana kuhitaji zaidi ya teknolojia ya hali ya juu. Ushirikiano wa karibu wa kijeshi na kimkakati na washirika wake hususan Marekani, unaweza kuwa msingi wa kufanikisha operesheni yoyote dhidi ya Fordow. Kituo hiki kimekuwa mfano halisi wa jinsi ambavyo mataifa hujenga ulinzi wa tabaka nyingi dhidi ya mashambulizi ya ghafla ya kijeshi.