Lema ahimiza kauli za viongozi wa dini kujenga umoja wa kitaifa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema akizungumza wakati mkutano wa hadhara uliofanyika leo Ijumaa Mei 8, 2026 eneo la Soko Kuu jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
Muktasari:
- Viongozi wa madhehebu ya dini wameombwa kutoa kauli zinazojenga mshikamano na umoja wa kitaifa na kuacha kutoa kauli zinazochochea migawanyiko kwa misingi ya kidini.
Arusha. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema amesema viongozi wa madhehebu ya dini wana nafasi muhimu ya kuunganisha jamii badala ya baadhi yao kutoa kauli zinazoashiria kuwagawa wananchi kwa misingi ya kidini.
Amesema hayo leo Ijumaa, Mei 8, 2026 wakati akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Soko Kuu jijini Arusha kuwa viongozi wa upinzani wanapokosoa viongozi waliopo madarakani hawafanyi hivyo kwa sababu ya misingi ya kidini bali ni wajibu wa kuhimiza utawala bora unaozingatia sheria.
“Nawasikia baadhi ya viongozi wa Kikristo na Kiislamu wakizungumza mara kwa mara. Baadhi yao kauli zao zinajaribu kuonesha tunapokosoa utendaji kazi wa Serikali tunailenga dini fulani. Niwaonye kuacha mwelekeo huo kwa sababu upinzani tumekuwa tukikosoa viongozi wa awamu zote bila kujali imani zao,” amesema Lema.
Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 8, 2026 kwenye eneo la Soko la Kuu jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu
Hotuba yake pamoja na mambo mengine ilijikita kuichambua ripoti ya Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande iliyochunguza vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na baada ya hapo amesema lazima waliohusika wawajibishwe bila upendeleo au kuwaonea wasiohusika licha ya kukosoa uhalali wa tume hiyo.
Amesema viongozi wa upinzani wanafanya kazi zao katika mazingira magumu ya kuwindwa licha ya kuwa shughuli za kisiasa za vyama vingi zipo kwa mujibu wa sheria na kuahidi wataendelea kuwasemea wananchi bila kujali gharama wanayolipa kwa sababu huo ndio wito waliochagua.
Lema amekemea matukio ya utekaji na vifo vinavyotokea katika mazingira yasiyoeleweka akisema mambo ya namna hiyo yanajenga chuki ya wananchi dhidi ya watawala na kutaka wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.
“Maridhiano ya kweli, mchakato wa Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi unapaswa kuanza sasa hivi. Kuchelewesha mchakato wa masuala muhimu kama haya kunalenga uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2030 ufanyike katika mazingira ambayo wananchi hawatakubali,” amesema Lema.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob akihutumia wakazi wa Arusha kwenye mkutano uliofanyika Mei 8, 2026 eneo la Soko Kuu. Picha na Filbert Rweyemamu
Kwa upande wake, Boniface Jacob maarufu ‘Bon Yai’ ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amekemea mwenendo uliokita mizizi katika jamii wa wananchi kukamatwa bila kuzingatia misingi ya kisheria na baadhi ya waliokamatwa kutoweka na wakati mwingine kukutwa wamekufa.
“Tunapaswa kuishi kwenye nchi inayozingatia utawala wa sheria. Vyombo vya sheria vinavyohusika na ukamataji wa watuhumiwa vinapaswa kuvaa sare ili vitambulike na vitoe nafasi kwa mtuhumiwa kuwasiliana na ndugu zake pamoja na wanasheria kwa ajili ya msaada zaidi,” amesema Jacob.