Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yapinga matokeo ya ripoti ya Jaji Chande, yaja na mapendekezo mapya

Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala

Muktasari:

  • Chadema yakataa matokeo ya uchunguzi rasmi ya Jaji Chande, yaja na mapendekezo ya kufanyika uchunguzi huru wa kimataifa wenye sura ya kijaji huku ikishinikiza uchaguzi mkuu urudiwe.

Dar es Salaam. Baada ya kukataa matokeo ya ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeazimia kuundwa kwa Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi yenye hadhi ya kijaji ili kuchunguza kwa kina na kubaini wote waliohusika.

Chadema kimesema tume hiyo itakuja na majibu ya vitendo vya ukiukwaji vilivyotokea katika kipindi hicho na kupendekeza hatua za kuchukuliwa.

Pia, chama hicho kimedai kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu 2025 ili kurejesha misingi ya demokrasia huku kikitangaza kuwatambua kama “Mashujaa wa demokrasia ya kweli ya Tanzania” watu wote waliouawa au kujeruhiwa katika kipindi hicho cha vurugu.

Sambamba na hayo, kimependekeza kuvunjwa kwa Jeshi la Polisi, kikirejea mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai. Tume ya kuchunguza matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, kikidai haikutekeleza majukumu yake kwa kiwango kinachokubalika licha ya kutumia fedha za walipa kodi.

Chama hicho kimeendelea kuiomba Serikali kuweka hadharani ripoti kamili ya tume hiyo pamoja na viambatisho vyake. Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan, alipokabidhiwa ripoti hiyo Aprili 23, 2026 na Jaji Chande, alisema hiyo ni ripoti yake na asitokee mtu akaitaka.

Msimamo huo wa Chadema umetolewa leo Jumanne, Mei 5, 2026 na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, akirejea maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho yaliyofanyika Aprili 28 na 29, 2026.

Kikao hicho kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kutokana na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kuwa gerezani kwa kesi ya uhaini, kilijadili na kutathmini masuala mbalimbali, ikiwemo kuichambua ripoti hiyo ya Jaji Chande.

Aprili 23, 2026, akiwasilisha matokeo ya uchunguzi huo, Jaji Chande alibainisha vyanzo vitano na vichocheo vinne vya matukio ya vurugu za Oktoba 29 na baada yake, akitaja miongoni mwao kauli za wanasiasa na matukio ya utekaji.

Leo Jumanne, Mei 5, 2026, Dk Nshala akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam, amesema kuwa hawakubaliani na uchunguzi uliofanywa.

"Kamati Kuu imeazimia njia pekee ya kufahamu ukweli ni kuundwa kwa Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi yenye sifa ya Tume ya Kijaji ili kuchunguza na kuwabaini wale wote waliotenda maovu yote yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Oktoba 29, 2025. Wale watakaobainika kuwa na hatia watafungwa na kutakiwa kuwafidia wale waliowajeruhi na kuwaua," amesema.

Amesema Kamati Kuu imeamua kuwatangaza kama Mashujaa wa Demokrasia ya Kweli ya Tanzania wale wote waliojeruhiwa na kuuawa wakati huo wakipigania demokrasia na wanastahili fidia ya haki na toshelevu.

"Kamati Kuu imeazimia kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu ili Watanzania wasiendelee kutawaliwa kimabavu na wauaji ambao wametwaa madaraka kwa kutumia polisi na vyombo vya usalama wa taifa.

"Uchaguzi huo lazima usimamiwe na Tume mpya kabisa ya Uchaguzi. Kamati Kuu inasisitiza uongozi uliopo madarakani umejiweka madarakani kibabe kwani wametwaa madaraka kwa mtutu wa bunduki na kwa kumwaga damu ya maelfu ya Watanzania. Sio rais wa Watanzania," amesema.

Amesema Kamati Kuu ya chama hicho imeazimia na kusisitiza tena takwa lake la muda mrefu juu ya kutungwa kwa Katiba Mpya mara moja chini ya Bunge huru la Katiba ambalo halitawahusisha wale wote waliotenda unyama.

"Kamati Kuu inasisitiza kuvunjwa kwa Jeshi la Polisi kama ambavyo tayari Tume ya Haki Jinai ilipendekeza, lakini mapendekezo yake hayajatekelezwa. Vivyo hivyo, kuundwa upya kwa taasisi za utumishi wa umma," amesema.

Dk Nshala amesema Kamati hiyo imeazimia Tume ya Jaji Chande ivunjwe kwa kuwa imefanya kazi hiyo kwa kodi za wananchi lakini majibu ya ripoti hayajaakisi ukweli dhidi ya magumu waliyopitia wananchi.

"Serikali iweke ripoti ya tume hadharani pamoja na viambatisho vyake, na kwa kuwa kilichowasilishwa ni hotuba na si ripoti, basi ripoti itapowekwa hadharani Kamati Kuu imeazimia itafanya uchambuzi wake kikamilifu. Haki ya kuishi ni haki mama; pale haki hii inapokiukwa, sababu za kukiukwa kwake haziwezi kuwa siri ya rais au watu wachache," amesema.

Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Dk Nshala amesema kwa kipindi kirefu Watanzania wamepata matatizo makubwa yanayotokana na Katiba iliyopo.

"Kamati Kuu inasema Watanzania hawawezi kusubiri tena Katiba Mpya kwa kipindi kingine isipokuwa sasa. Kwa sababu hiyo, Kamati Kuu imeazimia kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Kamati Kuu ili kuandaa mkakati wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya," amesema.

Amesema Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa muswada wa sheria, kwa niaba ya wananchi, utakaoeleza utaratibu wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya.

"Muswada huo utaeleza namna kura ya maoni ya Katiba Mpya itakavyofanyika, chombo huru cha kusimamia kura hiyo ya maamuzi. Kamati Kuu imeazimia kuwa chama kiongoze wananchi kutaka kuanzia sasa mchakato uanze na Katiba Mpya ipatikane mapema hadi mwaka 2027 na si zaidi ya hapo," amesema Dk Nshala.


Chadema yamjibu Kihongosi

Katika hatua nyingine, Chadema kimemjibu Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, aliyekitaka chama hicho kuheshimu mhimili wa Mahakama, kikisisitiza kinachodai ni haki na si kuingilia mhimili huo.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Garubindi, amesema Tanzania imefikia hatua ya kuwepo kwa malalamiko ya kubambikizwa kesi kutokana na kukosekana kwa utawala thabiti wa sheria.

Msingi wa majibizano hayo unatokana na kauli za viongozi wa Chadema wanaodai kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, wakisisitiza kuwa tuhuma hizo ni za kisiasa na hazina msingi.

Jana, Mei 4, 2026, Kihongosi akizungumza na wanahabari alisema CCM itaendelea kulinda demokrasia kwa kuheshimu mihimili ya dola Bunge, Serikali na Mahakama akionya kuwa hakuna chombo kinachopaswa kuingilia uhuru wa Mahakama.

Katika maelezo yake, alisema viongozi wa Chadema wanaotoa kauli za kuonyesha mtu anaonewa bila uamuzi wa Mahakama wanakiuka misingi ya demokrasia.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Garubindi amesema Chadema haiingilii Mahakama bali inasisitiza umuhimu wa haki kutendeka kwa wakati. Alieleza kuwa ni muhimu Mahakama kupewa rasilimali za kutosha ili kusikiliza kesi kwa haraka na kutoa maamuzi ya haki.

“Hatusemi Mahakama imuachie Lissu, tunataka isikilize kesi yake na kutoa uamuzi kwa mujibu wa ushahidi. Haki ya mtu haiwezi kucheleweshwa kwa muda usiojulikana; kilichopo ni Mahakama kutumika kama sehemu ya kuegesha kesi badala ya kuzisikiliza,” amesema.

Amesema chama hicho hakitaki kuona hali ya kesi kucheleweshwa mahakamani, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaleta taswira ya Mahakama kutumika kama sehemu ya kuchelewesha haki badala ya kuitenda.