Hofu ya wadau INEC ikitoa orodha ya wasimamizi wa uchaguzi

Muktasari:
- Wadau wa uchaguzi wameeleza hofu kuhusu uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi na INEC, wakisema wengi ni maofisa wa Serikali na huenda wakakosa uadilifu. Wamependekeza usimamizi huo ufanywe na watu huru wasiokuwa watumishi wa umma.
Dar es Salaam. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikitoa orodha ya majina ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwa halmashauri zote 184, kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, baadhi ya wadau wameeleza wasiwasi wao kuhusu uadilifu na uhuru wa wateule hao, ambao wengi wao ni maofisa waandamizi wa Serikali.
Kabla ya kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo, chaguzi zilizopita zilikuwa zikisimamiwa na wakurugenzi wa halmashauri, jambo lililozua malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wadau wa siasa.
Malalamiko hayo yalihusiana na wasiwasi kwamba watendaji hao wa Serikali wangeweza kutotenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia uchaguzi, kutokana na nafasi zao katika mfumo wa utawala wa kiserikali.
Kwa mujibu wa kifungu cha sita cha sheria hiyo mpya, kifungu kidogo cha kwanza, tume inaweza kumteua mtumishi wa umma mwandamizi kuwa msimamizi wa uchaguzi kwa madhumuni ya kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata, na msimamizi huyo wa uchaguzi anaweza kuwa msimamizi wa uchaguzi kwa jimbo au kata zaidi ya moja.
Kifungu kidogo cha pili cha sheria hiyo kinaeleza kuwa tume inaweza kuteua mtu kutoka miongoni mwa watumishi wa umma, kwa jina au nafasi aliyonayo katika ofisi, kuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwa madhumuni ya kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata.
Sheria hiyo katika kifungu kidogo cha tatu inaelekeza sifa za ofisa mwandamizi anayeweza kuteuliwa kuwa msimamizi wa uchaguzi ni yule ambaye hajawahi kutiwa hatiani katika shauri la nidhamu au kosa lolote la jinai na kuadhibiwa kwa kifungo kinachozidi miezi sita; na (b) hajawahi kuwa kiongozi wa chama cha siasa.
Hata hivyo, baadhi ya wadau waliozungumza na Mwananchi leo, Julai 2, 2025 wamehoji uadilifu wao na kama watatenda haki kwa wagombea wa vyama vyote bila kuingiza maslahi ya kisiasa.
Mchambuzi wa masuala ya siasa ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk George Kahangwa, amesema licha ya kuwaondoa wakurugenzi kwenye usimamizi wa uchaguzi bado kuna shaka ya upatikanaji wa haki kwa uchaguzi kusimamiwa na maofisa waandamizi wa Serikali.
Amesema upatikanaji wa wasimamizi hao ulipaswa kuzingatia sifa na vigezo vinavyohitajika kwa wadau wa uchaguzi, kubwa ikiwa ni kuwapata watu huru.
“Mchakato ungehusisha watu kuomba na kuchujwa hadharani, kwa hawa waliopatikana nani ana uhakika kuwa hao maofisa waandamizi wa Serikali hawana chembechembe za kisiasa na wanaweza vipi kusimamia uchaguzi kwa haki?
“Jambo hili lingefanyika hadharani, wangeweza kuhojiwa, na kama ana kadi au uanachama wa chama fulani anapaswa kuukana katika kipindi cha utendaji wake ndani ya tume. Ukweli ni kwamba maofisa wa Serikali wengi wana itikadi za kisiasa. Tulitamani kuona wasimamizi wa uchaguzi huru, siyo maofisa wa Serikali,” amesema.
Hoja hiyo imeelezwa pia na mchambuzi wa siasa, Kiama Mwalimu anayesema maoni ya wadau yalipaswa kusikilizwa kwa kuwaweka wasimamizi ambao si watumishi wa Serikali.
“Tume ingetangaza kazi, watu wakaomba, wakafanya usaili, kisha watakaofaulu wafanyiwe vetting. Hapa lengo ni kuwapata watu walio nje ya mfumo wa Serikali,” amesema Mwalimu.
Mchambuzi huyo ameeleza kuwa kwa aina hiyo ya wasimamizi walioteuliwa, hakuna namna Serikali itakosa malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wa siasa.
“Hata kama watatenda haki, bado itaonekana wana upande kwa sababu wao ni maofisa wa Serikali, hivyo malalamiko yatakuwepo na huenda yakawa mengi zaidi wakati huu.”
Mwanasiasa mkongwe Magdalena Sakaya amesema hakuna mabadiliko yoyote yanayotegemewa kwa kuwaondoa wakurugenzi wa halmashauri na jukumu la usimamizi wa uchaguzi kupewa maofisa wa Serikali.
“Kilichofanyika ni kuwahadaa Watanzania kuwa Serikali sasa haisimamii uchaguzi kama ilivyokuwa zamani kutokana na malalamiko ya wakurugenzi kupewa jukumu hilo. Hapo hakuna tofauti, maofisa wa Serikali ni wale wale. Ni sawa na kutoa mvinyo kwenye chupa na kuweka kinywaji kingine,” amesema.
Sakaya amesema kilio kikubwa cha wadau ni tume kuwa na watendaji wake, ambao ndiyo wanapaswa kutekeleza jukumu hilo na si kurudi tena kwa watendaji wa Serikali.
“Hivi kwa mfano huyo msimamizi mmoja anayepewa majimbo manne, ikitokea shida kwenye jimbo moja ambalo hayupo, utatuzi wake wa haraka unafanywa na nani kama si wale wa chini ambao ni watendaji wa kata, mitaa au hawa wasimamizi wengine ambao ni watumishi wa Serikali?
“Msisitizo wangu ni ule ule, ili tume iwe huru iwe na watendaji wake. Hapo itakuwa na mamlaka ya kuwahoji na kuwawajibisha, lakini hao watumishi wa Serikali hawana mamlaka nao,” amesema.