Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaji Mutungi kuwafunda viongozi vyama vya siasa, INEC…

Muktasari:

  • Msajili ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho joto la uchaguzi huo linazidi kupanda ndani ya vyama 18, vilivyopo kwenye hatua ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kutia nia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa dola ikiwemo udiwani, ubunge na urais.

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi amejipanga kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoingia kwenye Uchaguzi Mkuu kuwapatia hadidu za rejea za kuzingatia ili wasiingie kwenye mtego wa kuvunja sheria za nchi.

Msajili ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho joto la uchaguzi mkuu linazidi kupanda ndani ya vyama 18, vilivyopo kwenye hatua ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kutia nia kuwania nafasi mbalimbali za udiwani, ubunge na urais.

Baada ya kumaliza mchakato huo kila chama kitajifungia kufanya mchakato wa mchujo wa wagombea kwa kushindanisha na kuangalia anayefaa kupeperusha bendera ya chama hicho, kisha kuwasilisha jina lake Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya uteuzi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Juni30, 2025 Jaji Mutungi amesema mkutano huo upo mbioni kufanyika kuanzia sasa, kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025 huku akisisitiza kalenda yake itatoka siku si nyingi.

"Lazima nikutane na viongozi wa vyama vya siasa. Niwaeleze, najua wanaenda kwenye uchaguzi watapitia vipindi vingi ikiwemo kampeni lazima wazingatie sheria za nchi ili kulinda amani na utulivu uliopo nchini," amesema Jaji Mutungi.

Amesema pamoja na kwamba wataingia kwenye mchakato huo unaosimamiwa na INEC baada ya kutoa ratiba yake, lazima wazingatie sheria za nchi.

Jaji Mutungi amesema awali ofisi yake ilishatoa barua ya angalizo kwenda kwa makatibu wote wa vyama vya siasa kuwakumbusha kuheshimu taratibu katika mikutano yao ya hadhara iliyokuwa inafanyika mikoani.

“Mikutano ya hadhara, vyama vinafanya kama njia ya kukusanya wanachama, kunadi sera zao, tuliandika barua ile makusudi kuwaonya wasifanye vitu ambavyo havikubaliki na niko mbioni kuitisha kikao kazi na viongozi wakuu wa vyama kuwapa tahadhari hata kipyenga kikipulizwa wawe makini kwa mujibu wa sheria,” amesema Jaji Mutungi.

Hata hivyo, amesema tangu ametoa barua hizo mpaka leo hajapelekewa malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria.

Mei 10, 2025, Ofisi ya Msajili kupitia idara yake ya sheria iliandika barua kwenda kwa makatibu wa vyama vyote vya siasa zikieleza kuwa zinaanza kufuatia mikutano ya vyama hivyo inayoendelea, ili kuwabaini viongozi au wanachama wanaovunja sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 kwa kutumia maneno ya uongo na kashfa dhidi ya chama kingine.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu amesema taarifa ya kufanyika mkutano huo alishadokezwa na msajili ingawa bado hajaitwa kwenda kuandaa ajenda.

"Kiutaratibu lazima niitwe kuandaa pamoja ajenda za kuzungumza kwenye mkutano huo, ingawa awali alishanidokeza kutafanyika mkutano kama huo lakini ngoja nifuatilie kujua mipango ikoje," amesema

Khatibu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, amesema mkutano huo ni muhimu ufanyike kwa kuwa kipindi wanachokiendea ni cha lala salama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele amesema muda wowote kuanzia sasa wanatarajia kutoa ratiba ya matukio yote kuelekea Uchaguzi Mkuu.

"Ratiba yetu tutatangaza muda si mrefu, tulikuwa tunasubiri ratiba ya Bunge kuvunjwa na kwa kuwa Rais ameshatoa hotuba yake basi nasi rasmi tunajiandaa kutoa ratiba yetu," amesema.

Juni 27, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alilihutubia Bunge la 12 na kuhitimisha shughuli zake huku akitangaza atalivunja rasmi Agosti 3, 2025.