Prime
Zuio la Chadema laibua maswali tata, yenyewe yaanza utekelezaji

Muktasari:
- Hatua ya Mahakama Kuu kukizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake imezua maswali tele na mijadala ya kitaifa kuhusu namna ya utekelezaji wake.
Dar es Salaam. Uamuzi wa Mahakama wa kuizuia Chadema, chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake kwa muda, umeibua maswali na kuanzisha mjadala mpana ndani na nje ya duru za kisiasa.
Hatua hiyo ya mahakama si tu imeibua sintofahamu kuhusu tafsiri ya shughuli za kisiasa zilizozuiwa, bali pia imeacha pengo la kisheria na kukiweka chama hicho njiapanda kiutendaji na mustakabali wake ikiwa kesi ya msingi itachukua muda mrefu kusikilizwa na kuamuliwa.
Katika mjadala huo, baadhi ya wadau wanauliza iwapo zuio hilo linahusisha mikutano ya hadhara, ya wanahabari, ziara, usajili wa wanachama wapya au hata vikao vya ndani, huku wengine wakitaka kufahamu iwapo mali zilizozuiwa ni pamoja na ofisi, magari na vifaa vingine muhimu kwa uendeshaji wa kila siku wa shughuli za chama.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu, ulitolewa Jumanne, Juni 10, 2025, kutokana na maombi yaliyowasilishwa kwenye kesi ya madai iliyofunguliwa na viongozi watatu wa zamani wa Chadema kutoka Zanzibar, wakilalamikia walichodai ni mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama baina ya pande mbili za Muungano – jambo linalochochea mjadala mpana kuhusu usawa ndani ya vyama vya kitaifa na nafasi ya Zanzibar katika vyama vya siasa vya muungano.
Wakati wadau wakihoji maswali hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema michakato ya Mahakama ina taratibu zake, hivyo kutoa uamuzi ni jambo moja, lakini kutoa amri ya utekelezaji wa uamuzi husika ni jambo lingine.
Saa chache baada ya uamuzi huo kutolewa, Chadema ilitoa taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia ikidai uamuzi huo umechochewa zaidi na shinikizo la kisiasa badala ya msingi wa kisheria au haki ukihusishwa na hali ya kisiasa ilivyo nchini.
“Chadema inachukulia hatua hizi kama ishara hatari ya kuporomoka kwa demokrasia nchini. Viongozi wa chama watafanya mkutano wa dharura kutathmini hali hii na kuamua msimamo rasmi wa chama kuhusu hatua za kuchukua,” ilieleza taarifa hiyo.
Alichokisema Msajili
Akizungumzia hatua hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema michakato ya mahakama ina taratibu zake, si suala la kukurupuka.
Amesema suala la Mahakama kutoa uamuzi ni jambo moja, lakini kutoa amri ya utekelezaji wa uamuzi husika ni jambo lingine.
Katika mazingira ya sasa, amesema inakuwa vigumu kueleza utekelezaji wa uamuzi husika unahusisha kufanya kitu gani na gani kwa sababu bado hata yeye hajaelezwa hilo.
“Tukipata hukumu nitaomba drawn order (amri ya utekelezaji) ambayo ndiyo inayotoa maelekezo ya namna gani ya kutekeleza uamuzi husika,” amesema.
Hata hivyo, Jaji Mutungi amesema Chadema kwa sasa wanapaswa kuwatafuta wanasheria wao ili wafuatilie amri ya utekelezaji wa uamuzi husika, kujua utaratibu wote.
Ni zuio la kila kitu
Akizungumzia tafsiri yake kwa uamuzi huo, Wakili Jebra Kambole amesema kilichoandikwa na Mahakama ni kwamba Chadema hairuhusiwi kufanya shughuli zote za kisiasa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, shughuli za kisiasa kwa chama cha siasa, zinahusisha kufanya mikutano, ziara, kusajili wanachama, vikao na mipango yote ya uendeshaji.
Kwa uamuzi huo, Jebra amesema chama hicho kimekatazwa kufanya lolote ndani ya kipindi hicho hadi kesi ya msingi itakapotajwa.
“Ndiyo maana tunasema ni uamuzi wa ovyo, kwa sababu huwezi kukizuia chama kufanya shughuli za kisiasa, unataka kife? Maana kila shughuli inayofanywa na chama cha siasa ni ya kisiasa,” amesema.
Kuhusu zuio la matumizi ya mali za chama, amesema kwa mujibu wa uamuzi huo, chama hicho hakiruhusiwi kutumia mali yake yoyote, yakiwemo majengo ya ofisi na hata magari.
“Hii maana yake hata gari lilipo halipaswi kuguswa libaki hapohapo na ofisini watu wasiingie, wasifanye vikao, sasa vitu si vitaharibika. Ni uamuzi usiotekelezeka na wa ovyo kuwahi kutolewa,” amesema.
Jebra amesema uamuzi huo unatolewa katika nyakati ambazo kumewahi kutolewa uamuzi unaoeleza chama cha siasa hakipaswi kuzuiwa kufanya shughuli zake.
“Kwa hiyo ni uamuzi unaokinzana na uamuzi uliowahi kutolea na mahakama, ni jambo baya kwa nchi yetu,” amesema Jebra aliyekuwa wakili wa utetezi kabla ya kujitoa kwenye kesi hiyo, na hivyo maombi hayo kusikilishwa na kuamuliwa upande mmoja.
Chadema yatekeleza
Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mohamed amesema kwa sababu mahakama imetoa uamuzi na ukizingatia ni chombo kinachojitegemea, hawana budi kutekeleza.
Katika utekelezaji wake, Said amesema tayari chama hicho kimeshasitisha ziara yake ya No reforms no election na sasa Makamu Mwenyekiti -Bara, John Heche anarejea Dar es Salaam.
Sambamba na hilo, amesema tayari chama hicho kimekwishatoa maelekezo kwa watendaji wote kuzunga ofisi, wabaki tu walinzi, huku wao wakisalia nyumbani hadi maelekezo mengine yatakapotolewa.
“Hatupendi kuliingilia sana, kwa sababu ni suala lililopo mahakamani, lakini tunatambua kuna mashinikizo ya kisiasa kwenye uamuzi huu. Kwa sababu Mahakama ni muhimili unaojitegemea tumeamua kutekeleza,” amesema.
Kauli hiyo imesisitizwa na Dk Rugemeleza Nshalla, mwanasheria mkuu mteule wa chama hicho, akisema kwa sababu uamuzi umeshatolewa moja kwa moja na amri ya utekelezaji imetolewa.
Kinachoumiza, amesema uamuzi huo umekosa hekima na busara na una kila ishara ya uvunjwaji wa haki.
Amesema Mahakama inaposimamisha Chadema kutumia mali zake, maana yake ziachwe kiholela kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kuzichezea.
“Sasa kama tunafanya hivyo, maana ya kuzilinda siku zote na kuzitunza inakuwa wapi. Huu ni uamuzi wa ajabu kuwahi kufanywa,” amesema Dk Nshalla.
Chadema ifanye nini
Kufuatia uamuzi huo, Mwanazuoni wa Historia kutoka Chuo Kikuu cha Bonn nchini Ujerumani, Philemon Mtoi amesema inachopitia Chadema kimewahi kuvikuta vyama lukuki vya upinzani duniani.
Mtoi amesema hata Chama cha Mapinduzi (CCM), kabla ya jina hilo kiliwahi kuwa chama cha upinzani dhidi ya Serikali ya kikoloni, nacho kilipitia magumu kama hayo, ikiwemo kiongozi wake, Mwalimu Nyerere kufunguliwa kesi mahakamani.
Kinachopaswa kufanyika katika hali kama hiyo, amesema kwanza viongozi wa chama husika wakubali kukabiliana na mazingira magumu ili kuyafikia mafanikio tarajiwa.
“Kama hauna watu wenye ngozi ngumu, wavumilivu, utapoteza. Historia ina kawaida ya kujirudia ,magumu wanayopitia Chadema sasa sio jambo jipya kwa vyama vya upinzani, watu wake wanapaswa kuwa wavumilivu na kutengeneza mikakati ya kuvuka,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema Chadema inapaswa kujitafakari na kutathmini kuona kama inaweza kuvumilia na baadaye kukabiliana na magumu hayo, ili kuvuke salama.