Hatima kesi ya mgawanyo wa rasilimali Chadema kujulikana leo

Muktasari:
- Kesi ya mgawanyo wa rasilimali Chadema imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wanaojitambulisha kuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Juni 10, 2025 inatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya kesi ya mgogoro wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wanaojitambulisha kuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mdaiwa wa pili.
Sambamba na kesi hiyo, pia wadai wamefungua maombi ya zuio dhidi ya chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi yao ya msingi itakapoamuliwa.
Hata hivyo, Chadema imeweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, huku ikitoa sababu tisa za kutaka kesi hiyo itupwe bila kusikilizwa madai ya msingi ya wadai.
Pingamizi hilo limejikita katika mamlaka ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, haki ya wadai kufungua kesi hiyo, matumizi ya sheria walizotumia kufungua kesi hiyo na uhalali kumuunganisha Katibu Mkuu.
Vilevile chama hicho kimeweka pingamizi dhidi ya shauri la maombi ya zuio la muda, huku ikitoa sababu kama hizo ilizozitoa dhidi ya kesi ya msingi.
Waombaji (wadai) nao kwa upande wao wameibua pingamizi la awali dhidi ya kiapo kinzani cha wadaiwa kinachojibu kiapo cha wadai kinachounga mkono maombi hayo ya zuio la muda
Katika pingamizi hilo waombaji wameibua hoja tano za pingamizi, pamoja na mambo mengine kuhusiana na kasoro za kisheria kwenye kiapo hicho.
Kesi ilipotajwa kwa mara ya pili, Mei 12, 2025 kwa ajili ya amri muhimu, Jaji Mwanga alielekeza pingamizi la Chadema dhidi ya kesi ya msingi lisikilizwe kwa njia ya maandishi na akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo leo Jumanne.
Pia, Jaji Mwanga aliamuru mapingamizi yote, yaani pingamizi la Chadema dhidi ya maombi hayo ya zuio na pingamizi la wadai dhidi ya kiapo kinzani cha Chadema pamoja na shauri lenye la maombi ya zuio yasikilizwe Juni 10, 2025 kwa mdomo.
Usikilizwaji wa mapingamizi hayo dhidi ya maombi ya zuio la muda pamoja na maombi hayo yenyewe leo Jumanne, Juni 10, 2025 unategemea uamuzi wa pingamizi hilo la Chadema dhidi ya kesi ya msingi.
Kama Jaji Mwanga atalitupilia mbali pingamizi hilo la Chadema, basi kesi hiyo itaendelea kuwa hai mahakamani hapo.
Uamuzi huo ndio utakaotoa uhalali wa usikilizwaji mapingamizi dhidi ya maombi ya zuio maombi ya zuio yenyewe leo, kabla ya usikilizwaji wa madai ya kesi ya msingi.
Kama Jaji Mwanga atakubaliana na pingamizi hilo la Chadema, basi kesi hiyo itatupiliwa mbali hata bila kusikiliza madai ya msingi.
Kwa uamuzi huo, hata usikilizwaji wa mapingamizi dhidi ya maombi ya zuio na maombi yenyewe, leo hautafanyika kwani shauri hilo la maombi ya zuio litakuwa limekufa kwani hayawezi kusimamia mahakamani bila kuwepo kesi ya msingi.
Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru amri za kutamka kuwa, wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.
Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, walalamikaji hao wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba, wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Mbali na amri hizo, wanaiomba Mahakama iamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi