Viongozi wapya CWT wapewa majukumu

Muktasari:
- Mchakato wa uchaguzi ngazi ya CWT ulianza Machi mwaka huu kwa wawakilishi wa shule, kisha ngazi ya wilaya na mikoa
Dodoma. Wakati Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kikikamilisha uchaguzi wake kwa ngazi ya Taifa, mambo matatu yanawasubiri viongozi waliochaguliwa ili kupeleka imani kwa wanachama.
CWT imekamilisha uchaguzi wao saa 11.45 ya leo alfajili, Jumatano Juni 10, 2025 uliokuwa na ulinzi mkali kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa milango ya nje huku ndani ya ukumbi kukiwa na polisi wa kutosha.
Kwa siku tatu mfululizo kulikuwa na mabango na vipeperushi vilivyozagaa katikati ya Jiji la Dodoma huku uchaguzi huo kwa mara ya kwanza ukitajwa kuendeshwa kwa ulinzi uliopitiliza.
Uchaguzi huo umempandisha aliyekuwa makamu wa rais wa CWT, Suleman Ikomba kuwa rais akimshinda aliyekuwa akitetea kiti hicho, Leah Ulaya.
Nafasi ya katibu mkuu imerudi kwa Joseph Misalaba awali alikuwa akikaimu Naibu Katibu Mkuu Magesa Protas kutoka Buhigwe, huku mweka hazina akipata Nashon Kidudu kutoka Kibondo.
Wanachama wametaja mambo yanayowasubiri viongozi wapya kuwa ni migogoro inayotajwa kukitafuna CWT na kusababisha kundi kubwa la walimu kukihama, makato makubwa ya michango ya wanachama na marekebisho ya katiba yao.
Mwalimu Julius Shangweli kutoka Mkoa wa Arusha amesema wanachama wengi wameihama CWT kwa sababu ya migogoro na mambo yanayoendelea ambayo hayana msingi wala afya kwa wanachama.
Mara kadhaa kumekuwa na mvutano wa kugombania wanachama kati ya CWT na Chama cha Kulinda na Kutetea Walimu Tanzania (Chakuhawata) kilichoundwa kutokana na mivutano ya viongozi.
"Ni migogoro ndiyo inawakimbiza wanachama wetu, sisi tuliobaki ni watu wafia dini na tutadumu hapa mwanzo hadi mwisho wa safari yetu," amesema Shangweli.
Mwalimu huyo, ametaja suala la makato kuwa makubwa kwamba yanakwenda kuwakatisha tamaa walimu kutokana na ugumu wa maisha walionao.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, kwa sasa kila mwalimu anakatwa asilimia mbili ya mshahara wake kwa ajili ya kuchangia mfuko wa CWT kiwango kinacholalamikiwa na wengi.
Kingine mwalimu huyo ametaja katiba ya chama chao ambayo amesema inawanyima haki na uhuru wa wanachama kuchagua viongozi badala yake, kikundi cha wachache kinafanya kazi hiyo kwa niaba ya wengine.
Aliyekuwa mgombea nafasi ya uwakilishi kundi la wanawake, Baby Tambuko amesema jambo kubwa ambalo angetamani waanze nalo viongozi ni kutafuta suluhu ya migogoro kuanzia uongozi ngazi ya Taifa hadi uwakilishi mashuleni.
Tambuko, amesema mbio za walimu wengi ndani ya chama ni kukosekana kwa utulivu kwa kuwa, baadhi wanahisi kuna kitu watu wanafaidi zaidi huko juu.
"Lakini hili la makato, kwa kweli linakera tena sana, tunajua kuna watumishi na mambo mengine lazima tujiendeshe lakini asilimia mbili? Hapana inabidi waangalie kwa kweli ni fedha nyingi," amesema Tambuko.
Akizungumzia mabadiliko ya katiba, amesema ni ya lazima na muhimu yakatazame kipengele cha jinsi viongozi wa juu wanavyopatikana kwa kuwa, inaminya demokrasia na uhuru wa watu katika kuwapata viongozi hasa kuanzia ngazi ya wilaya.
Kwa upande wake, Josephine Ruta kutoka Ngara amezungumzia alichokiita kiini macho kutoka benki ya walimu.
Josephine amesema wamekuwa wakisikia kitu kinaitwa Mwalimu Commercial Bank, lakini haoni faida wala manufaa yake kwani hata mikopo inakuwa na riba sawa na benki zingine.
Tambo za uchaguzi
Kwa siku mbili za kampeni jijini Dodoma, wagombea walikuwa wakibandika mabango makubwa tofauti ambayo hutumiwa na wagombea nyakati za uchaguzi.
Dalili za Ikomba kushinda zilianza kujionesha wazi kutokana na idadi ya wajumbe waliokuwa wakimuunga mkono, ingawa wengine walikuwa na hofu juu ya umri kwamba ataacha kabla ya miaka mitano.
Wagombea wengine katika nafasi zao walijitahidi kulifuata kundi la Ikomba wakitaja kuungana nalo ili wapate nafasi ya kuungwa mkono, hivyo wakajikuta wakiwa na makundi mengine nyuma yake.
Baada ya matokeo kutangazwa, Leah alipata wasaha wa kuzungumza na wajumbe wa mkutano huo akiwashukuru namna walivyompa ushirikiano tangu alipoanza kuongoza CWT huku akiacha kwa mambo matatu.
La kwanza amewaomba viongozi kudumisha mshikamano na kumaliza makundi, pili akataka watazame ni kwa nini walimu wengi wanazidi kuhama ndani ya CWT na kujiunga na chama kipya na mwisho ameomba viongozi kudumisha upendo.
Kwa upande wake, Ikomba ameomba wanachama wa CWT kumaliza makundi ya uchaguzi ili kukijenga chama imara kisichokuwa na mipasuko.
"Kwanza tumshukuru Mungu uchaguzi tumemaliza salama, hivyo mimi niwaombe tumalize makundi tuliyoyatengeneza katika uchaguzi na tumemaliza salama kila kitu kiishie hapa tuanze kujenga CWT imara," amesema Ikomba.
Idadi ya kura
Nafasi ya urais ilikuwa na wagombea 19, idadi ya kura zilizopigwa zilikuwa 891 huku kura moja ikiharibika na wagombea Barua Mwalimu, John Chakupewa, Julius Shangweli, Robert Kasimba, Hamis Mahenga, Charles Mudui, Ngamera Mutungi na Ghodhard Ndonyalo kila mmoja aliipata kura sifuri.
Rose Nyatega alipata kura moja, Emmanuel Kondowe (1), Ally Malinga (1), Rajabu Munyimbegu (2) na Stephen Mlobi (2).
Wagombea wengine ni Tumaini Twambo alipata kura 4, James Ndomba (4), Ismail Mussa (14), Leah Ulaya (260) na Suleiman Ikomba (608).
Nafasi ya Katibu Mkuu waligombea wanne, kura 892 zilipigwa na tisa kati ya hizi ziliharibika.
Matokeo ya kura za Katibu Mkuu ni Abihudi Bukuku alipata sifuri, Jeston Benjamin (7), Simon Keha (134) na Joseph Misalaba aliyepata kura 742.
Nafasi ya mweka hazina wagombea walikuwa saba huku Yusph Chaba akipata sifuri, Nestory Mwampela (1), Goodluck Kimaro (2), Said Mnunga (4), David Emmanuel (47), Ruhumbika Kapesa (78) na Nashon Kidudu kura 786.