Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgombea CWT aomba mdahalo na wenzake

James Ndomba (36), mwalimu wa Sekondari ya Msalato jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Uchaguzi Mkuu wa CWT unatarajiwa kufanyika Mei 29, 2025 jijini Dodoma na tayari wagombea wameanza kupishana mikoani kusaka kura.

Dodoma. Kampeni za uchaguzi kwa nafasi ya Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) zimeshika kasi, huku mgombea kijana kuliko wote akiomba mdahalo na wenzake.

Uchaguzi Mkuu wa CWT unatarajiwa kufanyika Mei 29, 2025 jijini Dodoma na tayari wagombea wameanza kupishana mikoani kusaka kura.

James Ndomba (36), mwalimu wa Sekondari ya Msalato jijini Dodoma, anatajwa kuwa mgombea mwenye umri mdogo zaidi kati ya walimu 18 waliopitishwa kwenye nafasi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Mei 24, 2025, Ndomba amesema ili kumpata kiongozi mwenye uwezo, ni vema ukawekwa mdahalo na watu wakaulizwa wanataka kuifanyia nini CWT kuliko kuwachagua kwa kuangalia majina.

James Ndomba (36), mwalimu wa Sekondari ya Msalato jijini Dodoma.

“Sitaki kuwabeza wagombea wenzangu, lakini natamani tukutane kwenye mdahalo ili watu watupime kwa kipi tunachotaka kukifanya mbele ya walimu. Naamini wakifanya hivyo, watapata viongozi wazuri,” amesema Ndomba.

Akizungumzia mikakati yake, amesema matamanio yake ni kuona CWT isiyo na migogoro wala malumbano, lakini lazima chama kiwajali walimu wanaostaafu baada ya kuwa wamechangia fedha zao kwa miaka mingi.

“Lakini lazima tupunguze makato. Haiwezekani kuwa na makato lukuki ndani ya chama, halafu wanachama wanabaki na vilio muda wote,” amesema Ndomba.

Hata hivyo, mgombea huyo amekosoa mfumo wa viongozi wa juu wa chama hicho kuchaguliwa na wawakilishi, akisema hauna afya. Badala yake, amesema ilipaswa viongozi wa ngazi ya juu wachaguliwe na wanachama wote.

Kuhusu vitega uchumi, amesema ni vema kuwa na benki, lakini ili kujiimarisha, CWT atakayoiongoza itanunua maeneo na kujenga shule za msingi na sekondari ambazo zitakuwa vitega uchumi vya kudumu. Walimu watakaofundisha ni pamoja na wastaafu.

Mwalimu Yusuf Komba kutoka Halmashauri ya Madaba amesema mchuano utakuwa mkali, kwani anamfahamu Ndomba na uwezo wake wa kuongoza tangu wakiwa chuoni, hivyo hamuoni kama mtu wa kubeza.

Komba amesema CWT inapaswa kuwa na viongozi wenye maono bila kujali umri wa mtu, kwani wamefika wakati hawataki migogoro kwa kuwa inawarudisha nyuma.

Mwakilishi wa kundi la wanawake kwenye mkutano wa CWT Mkoa, Liana Joseph, amekiri kuwepo kwa mpishano kutoka kwa viongozi wa juu wa chama hicho ambao wanataka kugombea ama kutetea nafasi zao, huku akikiri nafasi ya Rais itakuwa na mchuano mkali kuliko nafasi nyingine.