Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma yasitisha mikutano ya C4C kupisha Sikukuu ya Idd

Muktasari:

  • Ratiba ya mikutano ya hadhara itaendelea Jumapili, Juni 8, 2025, katika mikoa ya Kanda Nne: Victoria, Kaskazini, Magharibi na Serengeti baada ya kufanya tathmini.

Simiyu. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimesitisha kwa muda wa siku mbili mikutano yake ya hadhara chini ya Operesheni Chaumma For Change (C4C), ili kutoa fursa kwa viongozi na wananchi kushiriki na kusherehekea pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sikukuu ya Idd.

Hivyo, ratiba ya mikutano ya hadhara ya kuzungumza na umma itaendelea rasmi kuanzia Juni 8, 2025, katika mikoa ya Kanda Nne ambazo ni: Victoria, Kaskazini, Magharibi na Serengeti.

‘Operesheni Chaumma For Change’ (C4C), yenye malengo makuu manne, ilizinduliwa rasmi Juni 3, 2025, katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Dhamira kuu za operesheni hiyo ni kutambulisha safu ya uongozi wa kitaifa wa chama kote nchini, kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025, pamoja na kuziba ombwe la uongozi katika nafasi zilizo wazi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), John Mrema, chama hicho kimeamua kusogeza mbele baadhi ya mikutano ya Operesheni Chaumma For Change (C4C) baada ya kufanya tathmini ya awali ya ziara hiyo.

“Baada ya vikao vya ndani vya tathmini ya mikutano iliyofanyika tangu uzinduzi wa operesheni hii, tumefikia uamuzi wa kuahirisha mikutano iliyopangwa kufanyika leo, Ijumaa Juni 6, 2025,” amesema Mrema.

Ameongeza kuwa, “Pia, mikutano iliyokuwa imepangwa kufanyika kesho, Jumamosi Juni 7, haitafanyika ili kutoa nafasi kwa viongozi na wananchi kushiriki shughuli za kijamii na kijamii, ikiwemo kusherehekea Sikukuu ya Idd pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu.”

Hadi sasa, mikutano mitano tayari imeshafanyika, ukiwemo ule wa uzinduzi uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Mwanza.

Mikutano mingine mitatu imefanyika mkoani Mara na mmoja umefanyika Bariadi, mkoani Simiyu.