Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maandalizi uzinduzi wa C4C ya Chaumma yalivyo viwanja vya Furahisha

Muktasari:

  • Chaumma muda mfupi ujao itazindua operesheni ya C4C jijini Mwanza na itaendelea katika mikoa mbalimbali kwa kutumia helikopta na magari matano aina ya Toyota Land Cruiser. Mwenyekiti wa Taifa, Hashim Rungwe 'Mzee wa Ubwabwa', atarajiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Mwanza. Magari yatakayotumiwa na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) katika uzinduzi wa operesheni yao ya C4C kwenye viwanja vya Furahisha, jijini Mwanza, yameonekana yakiwa katika hatua za mwisho za maandalizi, yakiandaliwa kwa kufungwa bendera tayari kwa shughuli hiyo.

Chaumma kinazindua operesheni yake mpya ya C4C (Chaumma For Change) leo Juni 3, 2025, katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Mbali na uzinduzi huo, pia ndio uzinduzi wa ziara ya kuwatambulisha viongozi wapya na kukitangaza chama, ambayo inafanyika kwenye mikoa yote nchini kwa siku 16, ikianza na Kanda ya Ziwa.

Uzinduzi huo, utakaotanguliwa na msafara wa helikopta na magari matano ya Toyota Land Cruiser, utaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Hashimu Rungwe, pamoja na Katibu Mkuu, Salum Mwalimu, pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya kitaifa.

Shughuli hii itaambatana na mikutano ya hadhara katika mikoa mbalimbali nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma (Bara), Benson Kigaila (wapili kulia) akiwa eneo la Mkolani jijini Mwanza ambapo wanachama wa chama hicho watakutana kuelekea uwanja wa Furahisha kwaajili ya uzinduzi wa operesheni yao ya C4C. Picha na Saada Amir
 

Amsha amsha tayari yameanza eneo la Mkolani, ambapo maandamano ya wanachama na boda boda yanatarajiwa kuanzia kuelekea uwanja wa Furahisha kwa ajili ya mkutano huo.

Baadhi ya viongozi, ikiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama (Bara), Benson Kagaila wameonekana wakikusanya wanachama katika eneo hilo.

Magari matano aina ya Toyota Land Cruiser kama yanayotumiwa na watalii yameonekana yakiwa yamepakwa rangi za bendera ya Chaumma na kupambwa na maandishi mbalimbali ubavuni na maandishi yaliyokolezwa kwa wino mweupe yakisomeka ‘Tunaendelea tulipoishia’.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo leo, magari hayo yanatarajiwa kuongoza maandamano ya wananchi na makada wa chama hicho kuanzia eneo la Buhongwa, jijini Mwanza.

Mbali na magari hayo, maandamano hayo pia yatasindikizwa na helikopta iliyokodiwa kutoka nchini Afrika Kusini, itakayoruka kuelekea viwanja vya Furahisha.

Katika mkutano huo, mgeni rasmi atakuwa Hashimu Rungwe mwenyekiti wa chama hicho pamoja na viongozi wengine waandamizi akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila.

Baadhi ya bodaboda zikiwa eneo la mkolani jijini Mwanza ambapo wanachama wa Chaumma watakutana kuelekea Furahisha kwenye mkutano wa uzinduzi wa C4C.
 

C4C baada ya kuzinduliwa leo inatarajiwa kuzunguka mikoa yote Tanzania kwa usafiri wa chopa, rasmi kwa utambulisho wa safu mpya ya uongozi wa chama hicho na kupokea wanachama wapya kisha kuwaingiza kwenye mifumo ya Katiba ya chama hicho.

Shughuli hiyo ambayo Katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu anasema itakuwa imekamilika hadi mwishoni wa mwezi huu, pia inalenga kuziba ombwe la uongozi kwa kuweka viongozi wapya kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kanda zote.

Mandhari eneo la Furahisha

Shughuli za maandalizi katika viwanja vya Furahisha zinaendelea huku jukwaa kubwa, litakalokaliwa na viongozi wa kitaifa likiwa katika hatua za mwisho za kupambwa.

Kazi hiyo inaenda sambamba na upangaji wa viti pamoja na usimikaji wa bendera za chama hicho zilizoizunguka sehemu kubwa ya uwanja huo.

Wakati maandalizi yakiendelea, muziki unaopigwa na DJ unaendelea, huku wakazi wa maeneo ya jirani wakianza kujongea eneo hilo wakitaka kufahamu kinachoendelea.

Hadi kufikia saa 1: 40 mchana, viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho hawajawasili viwanjani, isipokuwa John Mrema, ambaye ameonekana akikagua maendeleo ya maandalizi kisha akaondoka.