Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema bado hakujatulia, viongozi Shinyanga wajivua uanachama

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Kishapu, Boniface Masanja (kushoto), aliyekuwa Katibu wa Bawacha mkoa wa Shinyanga, Furahisha Wambura (katikati) na Katibu wa jimbo la Msalala, Yussuf Paulo, leo Mei 14, 2025, wakati wakitangaza kujivua uanachama wa Chama hicho. Picha na Amina Mbwambo

Muktasari:

  • Viongozi hao ni wa matawi, wilaya na mkoa wa Shinyanga, kwa kile walichodai ni ubaguzi ndani ya chama kwa wale waliomuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho,  Freeman Mbowe kwenye uchaguzi wa ndani.

Shinyanga. Wanazidi kukibungua chama, ndiyo unavyoweza kusema baada ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) mkoani Shinyanga akiwemo aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) mkoani humo, Furahisha Wambura, na wanachama wengine wametangaza kujivua uanachama wa chama hicho.

Kwa wiki kadhaa zilizopita, Chadema imekumbwa na mfululizo wa wanachama na viongozi kujiondoa, wakiwamo akina Benson Kigaila, John Mrema, Julius Mwita, Salum Mwalimu na Catherine Ruge huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwamo ya kudai kubaguliwa kwa sababu walimuunga mkono Mbowe.

Akizungumza na wanahabari leo Mei 14, 2025, kwa niaba ya viongozi wengine, Wambura amesema, "ndugu wanahabari kwa sauti yetu ya pamoja tumekubaliana kuanzia leo Mei 14, 2025, tunatangaza rasmi kujivua uanachama wa Chadema."

Wengine waliojivua uanachama ni aliyekuwa Katibu wa Chadema jimbo la Msalala, Yussuf Paulo, mwenyekiti wa jimbo la Kishapu, Boniface Masanja na viongozi wa kata za jimbo la Kishapu, Shija Mshamo kata ya Sumageni, Evans Hilu kata ya Sumageni na Emmanuel Kinyambi kutoka kata ya Mloleji.

Amesema "Kumekuwa na upendeleo na ubaguzi mkubwa sana ndani ya chama kwa wale waliomuunga mkono Freeman Mbowe kwenye uchaguzi wa chama taifa"

"Ukionekana wewe ulikuwa timu au ulikuwa na mrengo fulani ndani ya chama chetu kumekuwa na changamoto za kufukuzana ovyo pasipo kufuata misingi ya katiba ya chama," ameongeza.

Amesema wataona namna watatafuta vyama au majukwaa mengine watakayotumia kufanya siasa zao, kuliko kuendelea na jukwaa hili lililojaa malumbano, kashfa, matusi, udhalilishaji na kutoheshimiana.

Amesema kila anayetoa hoja tofauti na kinachoendelea ndani ya chama anatengwa na kuitwa msaliti.

"Sisi ni baadhi ya watu tuliopewa jina la usaliti, kutokana na kuwa na maoni tofauti na wao, kwa hiyo tumeamua tutoke tutafute sehemu nyingine tufanye siasa,”amesema

Sababu nyingine ni kukosekana kwa misingi ya kidemokrasia, kusikilizana, kutokuwa na uhuru wa maoni.

"Tumekuwa tukijifariji na mikutano ya hadhara, tukipanda majukwaani, tunajiona tunaungwa mkono sana na wanachama, lakini ukweli ni kwamba hawajui nini kinaendelea ndani ya uongozi uliopo tumechoka kujidanganya."

"Kufurika kwa watu tusione kama tunakubalika, watu wanaweza wakafurika hata kwenye ugomvi na mambo mengine yasiyo hata na msingi, na hapa chama kimekuwa na kiburi kwa kuona kinakubalika kwenye mikutano kwa hiyo hata tukiwafukuza viongozi fulani sisi tunakubalika, hapana,”amesema.

Sababu nyingine ya kujivua kwao ni msimamo wa 'No reforms, no election' uliozua maoni tofauti miongoni mwao, na kuwa chama hakina mkakati wa kuzuia uchaguzi.

"Kama chama cha siasa tukishindwa kwenda kwenye uchaguzi, tafsiri yake ni kuogopa, tunadaije haki pasipo kwenda 'front' na ili ushinde vita lazima upambane, wao wanahubiri siku ya kupiga kura tujifungie ndani, hicho sisi tumeona hapana,”amesema.

Kwa upande wa Boniface amesema amekitumikia chama hicho kwa miaka 29, lakini leo ameamua kujivua uanachama na atatangaza baadaye chama atakachojiunga nacho.

Amesema "Ndani ya Chadema nimekuwa nikishughulikiwa mara kwa mara, hata kama ukifanya kazi ya kukijenga chama, unashughulikiwa mitandaoni, mwishowe nimeona nimekuwa mnyonge."

Yussuf Paulo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa chama hicho aliyefukuzwa uongozi bila kufuata utaratibu, amesema ameamua kujivua uanachama wa Chadema na atatoa tamko lake mwenyewe baada ya siku chache.