Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge la 12 limehutubiwa na Rais wawili, limeongozwa na Spika wawili

Muktasari:

  • Ni Bunge ambalo halikiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, isipokuwa wabunge wanane wa upinzani kutoka ACT-Wazalendo (3), CUF (4) na Chadema (1), walioshinda majimboni.

Dodoma. Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemaliza muda wake likiweka rekodi ya kuwa la kwanza kuhutubiwa na Rais wawili.

Vilevile limeongozwa na Spika wawili katika kipindi cha uhai wake, huku likishuhudia mabadiliko kadhaa katika safu ya Baraza la Mawaziri. Aliyedumu katika nafasi yake muda wote ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni – Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mwingine aliyedumu katika nafasi yake kwenye uongozi wa Bunge ni Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga.

Rais John Magufuli alilihutubia Bunge la 12 Novemba 13, 2020 ambalo mbali na wabunge wa CCM, halikiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, isipokuwa wabunge wanane wa upinzani kutoka ACT-Wazalendo (3), CUF (4) na Chadema (1), walioshinda majimboni.

Hapakuwa na wabunge wa viti maalumu kutoka vyama vya upinzani. Novemba 24, 2020 waliapishwa 19 kutoka Chadema ambao hata hivyo chama hicho kilisema hakiwatambui.

Spika Job Ndugai aliwaapisha zikiwa zimepita siku 10 baada ya kuchaguliwa kuwa Spika, nje ya ukumbi wa Bunge licha ya kuwapo mzozo kwamba hawakupitishwa na chama hicho kushika nyadhifa hizo.

Dk Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo kushindwa kufanya kazi.

Baada ya kifo cha Dk Magufuli, aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021 na akalihutubia Bunge Aprili 22, 2021.

Dk Magufuli na Samia walipohutubia Bunge, kiti cha Spika kilikaliwa na Ndugai, akiwa Spika katika muhula wa pili.

Ndugai akiwa ameweka historia ya kuwakaribisha Rais wawili kuhutubia Bunge moja alijiuzulu nafasi hiyo Januari 6, 2022.

Akiwa mbunge wa Kongwa tangu mwaka 2000, alijiuzulu akieleza amefikia uamuzi huo kwa hiari baada ya kutafakari kwa kina. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Spika kujiuzulu katika historia ya Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Alifikia uamuzi huo baada ya vuguvugu la siku 12 mfululizo baada ya kauli yake kuhusu deni la Taifa aliyoitoa Desemba 26, 2021 kwenye Mkutano wa Umoja wa Wagogo (Mikalile ye Wanyausi) alikozungumzia suala la kujitegemea kuliko kuwa tegemezi kwenye mikopo.

Katika hotuba alitoa mfano wa Bunge lilivyopitisha sheria ya tozo kwenye miamala ya simu ili kupunguza utegemezi na mikopo kwani nchi ilishakopa sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ndipo akasema: “Kuna wakati nchi itapigwa mnada” kama hatutakuwa makini katika kujitegemea.

Kauli hiyo iliibua mjadala wa pande mbili, waliomkosoa na waliompongeza lakini waliomkosoa walimzidi nguvu hadi akajiuzulu.

Baada ya Ndugai kujiuzulu, aliyekuwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alichaguliwa kuwa Spika Februari mosi, 2022, nafasi yake ikichukuliwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Bunge.

Dk Tulia alipitishwa kuwa mgombea pekee wa CCM akichuana na wagombea wanane kutoka vyama vya upinzani.

Mbunge huyo wa Mbeya aliibuka mshindi kwa kupata kura 376.

Dk Tulia amepata nafasi ya kumkaribisha Rais Samia kulihutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge kwa mujibu wa Katiba.

Ni katika Bunge la 12, historia imeandikwa kwa Spika Tulia kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023 nchini Angola.

Katika uchaguzi huo Dk Tulia alipata kura 172, wakati mpinzani wake wa karibu Catherine Gotani Hara wa Malawi alipata kura 61, Adji Diarra Kanouté wa Senegal (59) na Marwa Abdibashir Hagi wa Somalia (11).

Dk Tulia ni mwanamke wa kwanza kuongoza Bunge hilo lenye nchi wanachama 179 na wabunge 705 wanaoziwakilisha nchi zao.

Alichukua nafasi ya Duarte Pacheco, Spika wa Bunge la Ureno, ambaye alichaguliwa mwaka 2020.

Kwa Bunge la Tanzania, Dk Tulia ni Spika wa pili mwanamke baada ya Anne Makinda aliyeliongoza Bunge la 10, Naibu Spika akiwa Ndugai.

Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Njau anasema wabunge wamefanya kazi kwa bahati kubwa ndani ya Bunge la 12, ambalo licha ya misukosuko iliyopitia, limeweka historia kubwa.

“Ni Bunge ambalo lilitunga sheria nzuri, lilipitisha marekebisho kwa baadhi ya mambo mengi ambayo ni msaada kwa wananchi, tunaondoka tukijivunia mambo mengi na yataandikwa kwa wino wa dhahabu,” amesema.

Amesema ni jambo la heshima kuongozwa na Spika mwenye hadhi ya kuongoza mabunge duniani, akisema wakiwa huko anakuwa kiongozi lakini akirudi ndani ya jengo wanajiona kama wako kwenye viwango vya juu.

Mkazi wa Kisasa jijini Dodoma, Dk Geofrey Shoo anasema katika Bunge la 12 jambo atakalolikumbuka ni namna lilivyorudi kwenye mtindo wa matangozo ya moja kwa moja (Bunge Live) ambao ulikuwa umefutwa awali.

Dk Shoo anasema kurudi kwa matangazo ya moja kwa moja kuliwafanya wananchi kujua kilichokuwa kikiendelea ndani ya Bunge hilo.