Prime
Wataalamu watoa onyo mashindano ya kugida pombe

Muktasari:
- Profesa Harun Nyagori amesema bila kuangalia ni aina gani ya pombe, matumizi yake kwa namna yoyote yana athari kiafya, mojawapo ni misuli ya moyo kupanuka.
Dar es Salaam. Mashindano ya kugida pombe na hasa vinywaji vikali, yanaonekana kuongezeka kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii yakiwahusisha vijana.
Kupitia video zinazosambaa kwenye mitandao ya Instagram na X, baadhi ya vijana huonekana wakichuana kufakamia pombe kupata mshindi anayeweza kunywa nyingi na kwa haraka zaidi.
Kwa mujibu wa wataalamu waliozungumza na Mwananchi Juni 27, 2025, aina hii ya unywaji pombe kwa harakaharaka pasipo kupumzika ina madhara makubwa kwa afya ya mtu, akili, familia na jamii kwa ujumla.
Kwa nyakati tofauti, yameripotiwa matukio ya watu kufa wakishindana kunywa pombe.
Miongoni mwa hayo linamuhusu dereva wa bodaboda, Charles Ngaga, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Juni 28, 2024 katika Mtaa wa Kiswanya A, Manispaa ya Morogoro.
Taarifa ilieleza alikuwa akishindana na wenzake kunywa pombe kali chupa tano kwa wakati mpigo, jambo lililosababisha kifo chake.
Hatari kwa afya
Daktari Ernest Winchislaus anayehudumu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya anasema tatizo mojawapo la kiafya atakalokumbana nalo mtu anayegida pombe ni ini kusinyaa.
Anasema ugonjwa huo hutokana na uharibifu wa kudumu wa ini, ambao seli za kawaida za kiungo hicho huharibiwa na kukifanya kushindwa kufanya kazi zake vizuri.
“Kazi kubwa ya ini mwilini ni kuchuja sumu, kwa hiyo sumu isipochujwa ikakaa mwilini, mtu wa namna hiyo anasubiri tu kifo,” anasema na kuongeza:
“Pia anaharibu figo na matokeo yake ni kiungo hicho kushindwa kufanya kazi, matibabu yake ni kusafishwa damu kila mara au kubadilishwa figo.”
Dk Winchislaus anasema hatari nyingine ni uwezekano wa kupata saratani ya koo kwa kuwa pombe kali zina kemikali zinazochoma au kuharibu tabaka laini la koo.
Anasema unywaji wa vinywaji vikali husababisha koo kuwasha au kuwa na vidonda.
Kwa upande wake, mtaalamu wa magonjwa ya ndani, Profesa Harun Nyagori kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), anasema binadamu yeyote anapofanya jambo tofauti na inavyotakiwa, ana changamoto ya afya ya akili.
“Unywaji wa aina hii husababisha tatizo la akili na mtu hupoteza fahamu, mtu kupata msongo wa mawazo unaochangia kujiua na wengine kufanya matukio ya ajabu bila kujua. Unapokunywa pombe unapata ujasiri kupindukia, unafanya vitu unavyodhani ni sahihi kumbe si sahihi,” amesema.
Profesa Nyagori anasema bila kuangalia ni aina gani ya pombe, matumizi yake kwa namna yoyote yana athari kiafya, mojawapo ni misuli ya moyo kupanuka.
Anasema mishipa ya moyo ikipanuka athari yake ni kutorejeleka katika hali yake ya kawaida na huibua matatizo mengine ya moyo kushindwa kusukuma damu na kuishia kupata maradhi mengine kama kiharusi na mapafu kujaa maji.
“Matumizi ya pombe kupitiliza huweza kutengeneza umeme wa moyo kupitiliza na kusababisha mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida na mtu hufariki ghafla. Pia hutengeza kiwango kikubwa cha sumu ambayo huharibu chembechembe za ini na mtu kupata saratani ya ini,” amesema.
Suala hilo pia limezungumziwa na Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige kuwa athari mojawapo ya unywaji huo wa pombe, ni ongezeko la kilevi kwenye damu.
Kutokana na ongezeko hilo, amesema mhusika anakuwa kwenye hatari ya kufanya uamuzi hatarishi kama kuendesha gari akiwa amelewa, ngono zembe au kushiriki ugomvi.
“Hakuna kiwango chochote cha pombe kinachopendekezwa mtu atumie, lakini wanasayansi wanasema mtu anapaswa anywe bia moja kwa saa moja, ili kuruhusu umeng’enyaji uchukue nafasi. Mtu asilewe kwa haraka,” amesema.
Dk Mzige anasema mtu anapokunywa pombe kupindukia hufikia hatua ya kuwa mrahibu na mwili unapokosa kinywaji hicho hutetemeka.
Mtazamo kisaikolojia
Ramadhani Masenga, mtaalamu wa saikolojia amesema unywaji pombe wa aina hiyo unalenga kutafuta umaarufu.
“Maisha ya binadamu mara nyingi huhitaji kuwa bora, maarufu au kuwa na thamani kuliko mtu mwingine yeyote, hivyo wakati mwingine watu hujitofautisha na wengine kwa kuhatarisha afya zao,” amesema.
Masenga anasema asilimia kubwa ya vitu anavyofanya binadamu vinatokana na kuiga au kuangalia.
Anasema inapotokea mtu anakunywa pombe kwa kugida na kupakia video mtandaoni, husababisha watu wengine kuvutiwa kuiga kufanya.
“Athari ya kufanya mambo haya na kusambaza kwa kuwa hakuna onyo lolote kwenye jamii, mtu mwingine anaweza kuiga. Watu wanapaswa kufahamu kuwa hivi tulivyo leo ni kutokana na wale waliopita kabla yetu; hivyo matendo yetu na maneno yetu vinakuja kuwaathiri wanaokuja baada yetu,” amesema.
Mei 14, 2025 akiwa kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo mkoani Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo aliitaka jamii kuzingatia matumizi ya pombe kwa kiasi, hasa pombe kali.
Kauli hiyo ilitokana na utafiti uliofanywa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kunaonyesha unywaji kupindukia miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa katika jamii.
Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kilimanjaro (KCMC) kati ya Oktoba 2021 na Mei 2022 uliweka wazi kukithiri kwa tatizo la ulevi mkoani Kilimanjaro.
Kupitia utafiti huo wagonjwa 678 watu wazima (zaidi ya miaka 18) waliofika kupata huduma katika hospitali hiyo, matokeo ya awali yalionyesha wanaume waliohudumiwa matibabu ya kawaida, walikuwa wameathirika zaidi kuliko wanawake wa matibabu ya kawaida na wanawake wa kliniki ya uzazi salama, hali iliyohusishwa na unywaji wa pombe.
Katika utafiti huo uliofanyika katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baadhi waliohojiwa ya washiriki walisema pombe husababisha unyanyapaa, unyanyasaji wa kijinsia, tabia za ngono hatari na uwezo wa wanajamii kutekeleza majukumu yao binafsi.
Wengi waliona pombe inachangia katika ugomvi wa kimwili, kimaneno na kihisia kati ya wanafamilia na waliamini inachangia katika masuala ya afya ya muda mrefu na kutokuwa na uhakika wa kifedha.