Ndani ya Boksi: No totoz, no TikTok, no waganga, no maombezi

Muktasari:
- Wanawake mnafanya dunia iwe hivi. Hebu fikiria dunia bila pisi, totozi, warembo ingekuwaje? Ingekuwa dunia ya kipuuzi sana aisee. Sitamani hilo litokee hata kwa nusu saa ya dunia bila totozi
Dar es Salaam. Mtu mwenye akili zake timamu hawezi kuoa mke wa mitandaoni. Hawezi kuwa na demu muuza sura mitandaoni. Sikatai kuwa nao ni viumbe walioumbwa na Mungu. Lakini wenye ukaribu zaidi na shetani.
Wanawake mnafanya dunia iwe hivi. Hebu fikiria dunia bila pisi, totozi, warembo ingekuwaje? Ingekuwa dunia ya kipuuzi sana aisee. Sitamani hilo litokee hata kwa nusu saa ya dunia bila totozi.
Pengine FA mpaka leo asingetoka kimuziki. Mabinti walimfanya awe miongoni mwa wanamuziki wa kizazi kipya. Ukitaka ufanikiwe haraka sana kimuziki, waimbie hawa viumbe kina Hawa. Wao ndiyo wamiliki wa muziki.
Magereza yasingekuwepo.
Wengi wamefungwa jela kwa sababu ya kuwaridhisha totozi zao kifedha. Pale wanapoona bila pesa wataishia kuwaita shemeji, wanaamua kufanya lolote. Dunia ni ya mwanamke.
Kuna walioiba, kupora, kutapeli, kuua kwa ajili ya mapenzi. Na wenye maovu mengine ambao chanzo kilikuwa ni wanawake. Ndani ya muda mfupi siku za karibuni, kuna askari wamejiua kwa sababu ya viumbe hawa.
Asilimia kubwa masela hununua magari kwa sababu ya pisi kali. Na siyo kurahisisha usafiri. Bila pisi kupenda magari wallah wengi wasingenunua. Pisi zinalazimisha pesa ya kiwanja na tofali elfu tatu, zinunue ndinga kwanza.
Halafu sijui nao wamerogerezewa kwenye magari. Hata mtu akiwa na gari la kubebea maiti ili mradi kuna viti. Basi kwao ni burudani. Totozi na ndinga ni kama siasa na rushwa. Ni kama samaki na maji au pombe na komba.
Mitindo na nyumba za fasheni zisingekuwepo. Wabunifu kama na wengine wangekuwa wapasua mbao. Ubunifu upo kwa ajili yao tu, lakini hawa wanaume ni kama kulazimisha.
Pia vitu kama poda, wanja, na vinginevyo vingi visingekuwepo. Changamoto nyingi na maisha ya dunia hii yanaletwa na wao. Bila wao hakuna kidume wa kwenda kwenye majumba ya filamu.
Msela gani wa kukaa sehemu zaidi ya saa mbili kuangalia igizo huku akitafuna bisi? Kila kizuri kipo kwa ajili ya mwanamke. Wao ndio wanunuaji wakubwa wa bidhaa zote. Na ndiyo watumiaji wakubwa vitu.
Hununua chakula kingi kuliko uwezo wao wa kula. Hununua nguo na viatu kwa wingi kuliko muda wanaotumia kuzurura. Wanavaa vitu vingi mwilini kuliko ukubwa wa miili yao. Yaani kila kitu kwao ni kwa wingi.
Nywele za kuvaa, Kope za bandia. Sikioni hereni. Mkononi bangiri. Shingoni mkufu, kiunoni cheni au shanga. Mguuni vikuku na kucha zote za kuvalishwa. Nguo, mafuta na mapambo yasiyo ya lazima.
Mwanamke ni pambo la dunia. Wameumbwa hivyo na miili yao inaruhusu kupambwa. Tena kwa maneno na vikolombwezo. Wewe ukitaka utajirike uza bidhaa kwa ajili ya wadada.
Hawa ndio wameifikisha dunia hapa ilipo. Wao ndio chanzo cha uchungu na chanzo cha utamu pia. Wanafanya dunia iwe hivi ilivyo kama ni mbaya au nzuri.
Wanawake ni maua kiroho na kimwili.
Huleta furaha na hufanya vidume wafurahie maisha au wasifurahie. Nenda sehemu walipo wanaume tupu. Eneo hilo lazima lijenge urafiki na uchafu kuanzia watu mpaka mazingira. Wanawake ni jeshi kubwa sana.
Na kwa wingi wao kama kila mmoja akasimama kwenye nafasi yake, dunia itabarikiwa. Kwa maana hata Mwenyezi Mungu anamsikiliza mwanamke zaidi. Lakini kwa sasa imekuwa tofauti sana.
Sidhani kama wanawake wote wanasikilizwa siyo tu na Mungu, bali hata shetani mwenyewe hataki kuwasikiliza. Wanafanya ambayo shetani hata miaka 1000 mbele, hatokuja kufanya.
Kuna pisi za sasa kama shetani angewafuata kama Hawa wa Adam. Shetani angekutana nao njiani, wakimfuata kumshawishi yeye aje kuiteketeza dunia na viumbe wake. Hawa wa mjini hivi sasa shetani wao ni mitandao.
Utandawazi umekuwa shetani kamili kwa wanawake wengi. Kuliko shetani mwenyewe wa kuzimu kama siyo ahera. Yule aliyemrubuni Eva arudi shuleni kusomea upya.
Ili akapate elimu ya kurubuni wasichana, ili awe sawa na mitandao ya kijamii. Akili ya wasichana wengi hivi sasa ipo mitandaoni. Huko kunafanya wanawake wafanye lolote ili wanaonekana.
Kuanzia wake za watu na wengi tu huko mitaani, wamekuwa mateja mtandao. Ni ngumu kujua wapi zaidi. TikTok wapo, Insta wapo, Telegram wapo. Kwa waganga wa kienyeji wapo na makanisani wapo.