Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira arusha zigo kwa wabunge wataka majimbo

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara Stephen Wasira akizungumza na wanachama wa viongozi mbalimbali wa chama hicho Wilaya ya Magu mkoani Mwanza leo Juni 23, 2025 kupitia kikao cha ndani ya kukiimarisha chama hicho.

Muktasari:

  • Amesema ubunge hupatikana kwa kujenga uhusiano na watu, huku akionya watia nia wapya wa nafasi za ubunge na udiwani kabla ya kufanya hivyo, kupima kina cha maji.

Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu si tukio la ajali, hivyo wabunge ambao hawakuwa karibu na wananchi wakati wa uongozi wao hawapaswi kumlaumu mtu yeyote.

Amesema nafasi ya ubunge hupatikana kwa kujenga uhusiano mzuri na wananchi, huku akiwashauri wanachama wa CCM wanaotaka kugombea nafasi za udiwani au ubunge kupima kwanza kina cha maji, yaani kukadiria kama wanakubalika.

Kauli hiyo ya Wasira inakuja wakati Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likijiandaa kufungwa rasmi Juni 27, 2025, baada ya hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo itafungua pazia la mchakato wa uchaguzi kuanzia ngazi ya ndani ya chama hicho, kwa wale wanaotaka kuwania, wataanza harakati za kuwashawishi wajumbe wawapigie kura za maoni kabla ya kupitishwa rasmi na chama chao kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu.

Akizungumza na wanachama wa CCM na wakazi wa Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, leo Jumatatu, Juni 23, 2025, wakati wa mkutano wa ndani wa chama, Wasira amesema kumalizika kwa Bunge Juni 27 si jambo la ajabu, kwa sababu wabunge walijua tangu awali kwamba baada ya miaka mitano uchaguzi mpya utafanyika.

Amebainisha kuwa wawakilishi wasiofanya kazi waliotumwa na wananchi pekee ndio wenye sababu ya kuwa na hofu.

“Bunge linaisha Juni 27, 2025, na hii si ajali. Hata wakati wabunge waliingia, walijua baada ya miaka mitano kutakuwa na uchaguzi mwingine. Kama unafunga vioo na hutaki kuwasalimia wananchi, utamlilia nani wakati wa uchaguzi?

“Nimekuwa mbunge wa kuchaguliwa karibu mara nne, hivyo naweza kueleza kwamba nafasi ya ubunge hupatikana kwa kujenga uhusiano na wananchi,” amesema Wasira.

Amesema wabunge pekee wasiofahamika kwa wananchi waliowachagua ndio watakaopata wakati mgumu wakati wa uchaguzi.

Ameongeza kuwa wanachama wapya wanaotaka kugombea nafasi za udiwani au ubunge wanapaswa kwanza kupima kina cha maji kabla ya kujaribu.

“Wanachama wenzangu wanaotaka kugombea, hakuna mtu anayewazuia, lakini ni vyema kutembea na fimbo kupima kina cha maji. Ukiona kina kirefu, rudi, subiri wakati ukifika. Hata hivyo, sijui kama kina kitapungua kabla ya uchaguzi kumalizika,” amesisitiza.

Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga, kwa upande wake amesema kwenye uchaguzi wa mwaka huu, Jimbo la Magu limejipanga kuhakikisha Rais Samia anapata ushindi wa kishindo.

Amesema amejifunza siasa kwa Wasira, ambaye wakati wa ubunge wake alikuwa akitembelea kila kijiji, naye amefuata nyayo hizo kwa kufika kila kijiji na kueleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wa Rais Samia.

Kiswaga ameongeza kuwa mkoani Mwanza hakuna makundi ya kamati za siasa, na kama kuna mtu anayejaribu kuunda makundi, hayo ni makundi binafsi yasiyotambuliwa na chama.

Wasira yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kukiimarisha chama. Alianza na Wilaya ya Sengerema, kisha Magu, kuelezea mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.