Straika fundi wa AC Milan anayetikisa kwenye Hiphop Ureno

Muktasari:

Licha ya kuichezea AC Milan ya Italia na timu ya Taifa ya Ureno inayoshiriki Kombe la Dunia la Fifa 2022 nchini Qatar, Rafael Leao ni msanii wa hiphop mwenye albamu iitwayo ‘Beginning’ yenye nyimbo saba.

Licha ya kuichezea AC Milan ya Italia na timu ya Taifa ya Ureno inayoshiriki Kombe la Dunia la Fifa 2022 nchini Qatar, Rafael Leao ni msanii wa hiphop mwenye albamu iitwayo ‘Beginning’ yenye nyimbo saba.

Leao ni sehemu ya kikosi cha Ureno huko Qatar na alifunga goli la ushindi timu yake ilipoibugiza timu ya Taifa ya Ghana mabao matatu kwa mawili katika mchezo wa kundi H.

Jina lake kamili ni Rafael Alexandre da Conceicao Leao, alizaliwa Juni 1999, Almada nchini Ureno, amekulia katika klabu ya Sporting CP, kisha Lille, kabla ya kutimkia AC Milan mwaka 2019 kwa dau la Euro35 milioni, wastani wa Sh84.7 bilioni.

Katika ulimwengu wa hiphop, Leao anatumia jina la ‘Way 45’, nyimbo zake maarufu ni pamoja na ‘Ballin’, ‘Escolhas’ na ‘Layah’, huku akiwa na wastani wa kupata wasikilizaji zaidi ya 19,000 kila mwezi katika mtandao wa Spotify.

Akizungumza na Jarida la Rollingstone mwaka mmoja uliopita, Leao alisema anavutiwa sana na wasanii wa Rap kutoka Marekani kama Jay Z, Migos, Travis Scott, 6ix9ine, Roddy Rich, Meek Mill na Da Baby.

“Ninapenda hiphop na R&B, nadhani nikimaliza maisha yangu ya soka nitawekeza nguvu huko,” alisema Leao.

Alisema anapenda kila kinachofanywa na Jay Z kwenye muziki. “Huenda siku zijazo nikatafuta namna ya kufanya kazi pamoja, napenda hata namna anavyoendesha maisha yake,” alisema Leao ambaye ana mkataba AC Milan hadi Juni, 2024.

Utakumbuka Jay Z ana ushiwishi mkubwa katika muziki, akiwa ndiye msanii pekee wa hiphop aliyeshinda tuzo 21 za Grammy, ana rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa Rap kuwa bilionea ambapo utajiri wake sasa ni Dola za Marekani bilioni 1.3, ambazo ni wastani wa Sh3.0 trilioni.

Leao anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola135 milioni, wastani wa Sh314.7 bilioni, huku akipokea mshahara wa Dola2 milioni, wastani wa Sh4.6 bilioni kwa msimu, hivyo ni wazi anafanya muziki kwa mapenzi kama alivyosema katika mahojiano yake na Rollingstone.

Albamu yake ya kwanza ‘Beginning’ yenye nyimbo saba ilitoka Januari 2021, ikiwa ni takribani miaka miwili tangu kuonekana katika video ya wimbo ‘Longe’ wa kundi la BGang’s uliotoka Septemba 2020.

Wimbo wake ‘Ballin’ ndio uliopata mapokezi makubwa zaidi kwenye albamu hiyo, video yake iliyotoka Januari 30, 2021 imefikisha watazamaji 419,000 YouTube. Wimbo mwingine ambao haupo katika albamu hiyo, ‘Layah’, video yake iliyotoka miezi mitano iliyopita, imeshapata watazamaji zaidi ya 211,000. Kwa ujumla video za nyimbo zake zimefikisha watazamaji zaidi ya milioni 1.1 YouTube tangu ajiunge na mtandao huo Januari 18, 2021. Leao anasema maisha yake ndani ya AC Milan kwa kiasi kikubwa yamezungukwa na muziki. “Tunapokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo tunapokezana kuamua nini cha kusikiliza, kwa mfano kuna Theo ambaye ana asili ya Kihispania kila mara huweka nyimbo za Reggaeton, Daniel Maldini pia alinionjesha kidogo Rap ya Kiitaliano,” alisema winga huyu mwenye umri wa miaka 23.

Nyota huyo si mchezaji pekee wa Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ kujaribu muziki. Juni 2018 aliyekuwa golikipa wa Atalanta B.C, Pierluigi Gollini aliachia wimbo wake ‘Rapper Coi Guanti’ (rapa mwenye glovu).


UKIMKUTA UWANJANI BALAA

Rafael Leao, anacheza nafasi ya ushambuliaji katika klabu ya AC Milan na timu ya Taifa ya Ureno akikiwasha kwenye Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

Baada ya kuhitimu mafunzo ya soka katika timu za vijana za Sporting CP, Leao alianza kutumikia timu ya wakubwa mwaka 2018, akashinda taji la Taça da Liga msimu wa 2017–18, kabla ya kuvunja mkataba wake, baada ya kutokea utata ndani ya klabu yake.

Muda mfupi baadaye, akajiunga na klabu ya Ligi Kuu ya Ufaransa ya Lille akiwa mchezaji huru.

AC Milan ikamsajili mwaka 2019 kwa ada ya uhamisho ya Euro 35 milioni na katika msimu wake wa tatu klabuni humo, akaisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu wa 2021–22, mafanikio ambayo yalihitimisha ukame wa miaka 11 ya klabu hiyo bila ya kutwaa taji hilo.

Pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa Serie A baada ya kumaliza msimu akiwa amefunga mabao 11 na kutoa asisti za mabao mengine 11 na pia alitajwa miongoni mwa wachezaji 30 waliowania tuzo ya Ballon d’Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia.

Leao pia alijenga heshima ya kuwa mmoja wa wachezaji wakali wa kukokota mpira akifanya hivyo mara 186 kwenye Serie A na kushika nafasi ya tatu Ulaya nzima, nyuma ya Vinicius Junior (210) wa Real Madrid ya Hispania na Allan Saint-Maximin (205) wa Newcastle ya Ligi Kuu ya England.


MKWANJA SIO TATIZO

Kwa mujibu wa taarifa za fedha za mshambuliaji huyo kwa mwaka 2019 alikuwa alikuwa akilipwa mshahara wa Euro 1.4 milioni ambazo ni wastani wa Sh3.3 bilioni kwa mwaka. ikiwa na maana anapokea Euro 3,836 wastani wa Sh9.1 milioni kwa siku na Euro 160 wastani wa Sh380,800 kwa saa.