Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katiba, ukatiba na taasisi za kulinda Katiba (2)

Muktasari:

  • Tulitazama nini kilitokea baada ya watu weusi kufanikiwa kuondoa utawala wa wakoloni na kujiwekea utawala wa Kiafrika, na tukachambua tatizo la msingi lililojitokeza la viongozi wa Afrika kuanza kutumia nguvu kubwa kujiwekea mifumo ya kulinda madaraka waliyotwaa na kuyafanya kuwa yao, familia zao, ndugu zao na marafiki zao kuliko kazi ya ujenzi wa mifumo imara ya kitaasisi.

Wiki iliyopita tulitizama kwa kifupi historia fupi ya mahitaji ya kidemokrasia barani Afrika na namna Waafrika walivyopigania uhuru na kujitawala. Tulitazama nini kilitokea baada ya watu weusi kufanikiwa kuondoa utawala wa wakoloni na kujiwekea utawala wa Kiafrika, na tukachambua tatizo la msingi lililojitokeza la viongozi wa Afrika kuanza kutumia nguvu kubwa kujiwekea mifumo ya kulinda madaraka waliyotwaa na kuyafanya kuwa yao, familia zao, ndugu zao na marafiki zao kuliko kazi ya ujenzi wa mifumo imara ya kitaasisi.

Kitendo cha viongozi wa Afrika kuacha misingi hiyo ndiyo sababu kubwa ya Afrika kuitwa bara la shida, vita, umaskini, maradhi na kila aina ya matatizo. Na bila ubishi, fuatilia matatizo yote yaliyoko Afrika, utakuta ama yanahusu nchi kutokuwa na Katiba imara au nchi kuwa na Katiba imara lakini mamlaka hazitaki.

Mfano mzuri ni Kenya, wametengeneza Katiba nzuri baadhi ya viongozi wanaihujumu, kwa hiyo tatizo la Kenya siyo kukosa ukatiba, ni kwamba kundi la baadhi ya viongozi bado lina nguvu na uwezo wa kuihujumu Katiba na mifumo ya kuilinda Katiba, badala ya kuwacheka Kenya au kudhani wao ni mfano mbaya, tuwatumie kujifunza kuwa hali wanayopitia hivi sasa ni changamoto ya ujenzi wa misingi ya ulinzi wa Katiba kitaasisi. Kama ni ukatiba, Wakenya wamejawa nao, tatizo ni viongozi wachache.

Upotoshaji wa msemaji wa CCM

Hivi karibuni, akihojiwa katika Kituo kimoja cha televisheni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliweka bayana kuwa wao kama chama wanaunga mkono maamuzi (yasiyotajwa kwa uwazi) ya Rais wa sasa ya kuweka kando uhuishaji wa mchakato wa Katiba hadi hapo atakapomaliza kuinyoosha nchi.

Polepole anasisitiza kuwa wakati Rais akiinyoosha nchi ndipo wananchi watakuwa wanajenga ukatiba, kisha ndipo Katiba itaweza kutungwa na ikasaidia kuendeleza ukatiba kwa maana ya nidhamu za matumizi ya rasilimali za nchi na kuwa waaminifu na wazalendo.

Kauli hizi za Humphrey zimejaa upotoshaji wa makusudi ambao unapaswa kurekebishwa na nitaanza kutoa mifano dhahiri.

Taifa la Marekani ambalo tunadhani lina demokrasia iliyokua na maendeleo makubwa ya kiuchumi limepitia kwenye hatua nyingi, moja kati ya masuala yaliyolisaidia taifa hilo siyo kujenga ukatiba, bali ni kutengeneza Katiba bora yenye misingi ya haki sawa kwa watu wote na kisha kuitumia kujenga ukatiba kupitia kwenye mifumo au taasisi za ulinzi wa Katiba zilizopo (Bunge, Mahakama na taasisi muhimu za Serikali).

Polepole anajua vizuri (lakini hasemi ukweli) kwamba kwenye michakato ya kuhuisha nchi tunaanza kwanza kutungiana sheria kuu ili hata hao ambao tunahitaji watusaidie kunyoosha nchi, wafanye hivyo kupitia katika sheria kuu tuliyojitungia.

Anajua kuwa Katiba mpya bora na imara ndiyo inajenga ukatiba ambao unatokana na kazi ya mifumo na taasisi zilizowekwa kulinda Katiba na kuifanya iishi mioyoni mwa watu.

Mathalani, Tanzania haina sheria inayokataza viongozi kuchuma pesa zetu na kuzitunza kwenye akaunti nje ya nchi. Jambo hilo limekuwa njia ya kutorosha trilioni za pesa za walipa kodi maskini na kumekuwa na taarifa juu ya akaunti za viongozi wetu kukutwa na mabilioni ya fedha kama si matrilioni, wakati tuna ushahidi kuwa vipato vya viongozi hao hata kama wangelifanya kazi wa miaka 100 haviruhusu wawe na mabilioni ya pesa.

Ikitokea leo Rais Magufuli anaondoka madaraka kwa sababu za mapenzi ya Mungu, Katiba au sheria, ataiacha nchi ikiwa inachumwa na viongozi na kuweka fedha hizo nje ya nchi, kwa sababu tu hatukuwa na sheria kuu ambayo imepiga marufuku masuala hayo.

Katazo la Rais wa nchi siyo sheria kuu, likiazima hadhi ya sheria itakuwa hadhi ya muda mfupi na likitegemea zaidi muda ambao Rais husika atakuwa madarakani. Rais akiondoka, makatazo yake yote, minyoosho yake yote na kila mapambano aliyoendesha yanakoma. Ili kuwe na mwendelezo na mambo anayoyafanya Rais, lazima yawekwe kwenye sheria kuu ambayo ni Katiba.

Lakini, kubwa kuliko yote ni kwamba hata huyo Rais ambaye kwanza anajenga ukatiba (kunyoosha nchi – kwa tafsiri ya Polepole), anapaswa kufanya hivyo kwa mujibu na chini ya sheria kuu ambayo ni bora; huwezi kujenga nyumba imara kwa kutumia msingi mbovu. Kama Rais ananyoosha nchi na kushughulika na mafisadi na wahujumu uchumi lazima masuala hayo yawemo kwenye Katiba bora, tuweke ukomo wa nini kiongozi wa umma afanye, kama atakuwa mfanyabiashara afanye kwa masharti yapi, kama atakuwa mfanyakazi awekwe chini ya misingi gani.

Haiwezekani kwamba taifa la watu milioni 50 linajiachia mikononi mwa mtu mmoja na anainyoosha nchi kwa kutumia Katiba mbovu iliyopo kwa wakati huo halafu tunatetea mwendelezo wa masuala hayo kwa hoja dhaifu ya ati tujenge kwanza ukatiba - hivi unajengaje ukatiba bila kujenga Katiba bora? Yaani nani anasema utamaduni wa kuheshimu katiba unajengwa kwanza halafu katiba inafuata? Mbona huko ni kujidanganya mchana kweupe?

Watanzania ni wazalendo

Hoja inayotolewa kwamba Katiba si muhimu ila “ukatiba” ndiyo uanze, inajengwa kwenye hoja kwamba Watanzania wamepoteza misingi ya uzalendo, kujitoa kwa Taifa lao, kuwa waaminifu na kuheshimu misingi ya kikatiba – kwa hiyo watetezi wa hoja hiyo wanatamba kuwa panahitajika mtu mmoja kama Rais aachiwe kwanza ainyooshe nchi, ajenge uzalendo kwa wananchi, awafanye watu wote wawe waaminifu na waiheshimu Katiba mbovu iliyopo – na kwamba hayo yakishafanikiwa (ukatiba ukifanikiwa) ndipo tuandike Katiba bora ije na kuwakuta watu wameshazoea kuishi kwa kufuata Katiba. Tunasahau kuwa watu hao watajengewa uaminifu, uzalendo na uheshimu wa Katiba mbovu na ukatiba wataujenga juu ya misingi mibovu isiyomithilika.

Na tena, kitakachotokea kama tunaanza kudharau misingi ya kuweka Katiba kwanza ni kutengeneza ombwe na lazima lijazwe na chochote kitakachotokea. Nchi ambayo inaishi bila Katiba bora ina ombwe kubwa, na kama haizibi viraka na kuondoa mapungufu ya Katiba yake ina maana mapungufu hayo yatajazwa na mambo mengine.

Mathalani, kama tunaendelea kuabudu Katiba hii ya sasa na ubovu wake huku tukijificha kwenye hoja ya kujenga ukatiba kwanza (ambao hata hatuujui), tutapelekea makundi mawili ya jamii yetu kila moja lijijengee utamaduni wake. Tabaka la viongozi litaendelea kutumia madaraka vibaya na kuwakandamiza wasio na madaraka na litaendelea na utaratibu wa kufanya mambo vilevile chini ya utamaduni wa Katiba mbovu – na wakati huohuo, tabaka la wanaoongozwa litaanza kutafuta mbinu ya kupambana na mibinyo ya haki na uhuru wa kikatiba ambao wananchi waliupigania miaka 50 iliyopita.

Ni katika mazingira hayo ndipo taifa litapoteza mwelekeo kwa sababu viongozi na wanaoongozwa kila mmoja atajihami na kupigania uwepo wake; viongozi wataendelea kulinda madaraka na wananchi watajaribu kurejesha misingi ya haki, utu, kujitawala na demokrasia. Vita ya makundi haya mawili haitaliacha taifa salama, litaparaganyika kila mmoja akijaribu kulinda cha kwake.

Ndiyo maana hoja ya kupigania ukatiba kwanza inayoungwa mkono na rafiki yangu Polepole ni hoja mfu na mufilisi. Tanzania ya sasa inahitaji Katiba mpya kwa udi na uvumba, na rais wa sasa anapaswa kuongoza mchakato wa kupata Katiba ile ya maoni ya wananchi yaliyokusanywa na kina Polepole kwenye tume ya Jaji Warioba.

Rais wa sasa anapaswa kuongoza nchi walau kupitia katiba inayorejesha hadhi ya mihimili yote ya dola, inayolinda nguvu na mamlaka ya umma katika demokrasia na iliyojengwa juu ya misingi ya haki, utu na usawa.

Ukatiba lazima ufuate baada ya katiba kuwepo, na tena lazima ukatiba wenyewe ujengwe juu ya taasisi zinazolinda ukuu wa Katiba ikiwamo kukubaliana kuwa wananchi ndiyo wenye mamlaka ya mwisho ya mustakabali wa nchi yao.

Taasisi hizi zikifanya kazi vizuri na wananchi na wanaoongoza wakafuata misingi tuliyokubaliana kwenye katiba pamoja na mipaka ya viongozi na wanaoongozwa kwenye kila wanachokifanya – tutajenga taifa la maana na la mfano.

Nakumbusha kuwa Marekani kila mara walipokuwa wanaondoka katika zama moja kwenda nyingine walibadilisha Katiba yao, walipokuwa wanaondokana na ubaguzi wa rangi kujenga taifa la watu wote walijenga hali hiyo kwenye Katiba kwanza kisha wakaweka mifumo ya kulinda hadhi hiyo mpya. Afrika Kusini wakati walipokuwa wanaachana na ubaguzi wa rangi na kuunda taifa jipya walibadilisha katiba yao na kuweka misingi muhimu wanayoifuata hadi leo. Tanzania ya leo inayojaribu kujinasua kutoka kwenye matatizo lukuki ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii yanayosababishwa na watu wachache, inapaswa kuweka misingi hiyo kwenye Katiba yake na kisha kuweka taasisi zitakazojenga ukatiba miongoni mwa wananchi.

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])