Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo haya yatakujenga kuwa mwanafunzi bora

Muktasari:

  • Je, unaamini kuwa wewe ni miongoni mwa wanafunzi bora? Naamini kuwa unaweza kufanya makubwa kupitia uwanja wa elimu.Yote haya yanaanza na imani.

Uwezo wa kufanya jambo kubwa au dogo ni matokeo ya fikra inayoanzia ndani.

Kama alivyowahi kusema Henry Ford: "Ukiamini kuwa unaweza au ukiamini kuwa hauwezi uko sahihi."

Suala la msingi ni je,unaamini kuwa unaweza kupata unachotaka. Je, unaamini kuwa una akili kama walivyo wanafunzi wenye akili?

Je, unaamini kuwa wewe ni miongoni mwa wanafunzi bora? Naamini kuwa unaweza kufanya makubwa kupitia uwanja wa elimu.Yote haya yanaanza na imani.

Watu kama mwanasayansi, Albert Einstein na daktari wa binadamu, Dk Ben Carson ni watu ambao historia zao za utotoni hazikuwa nzuri kitaaluma lakini waliendelea kuamini kuwa wanaweza na ipo siku watafanya vizuri.

Leo hakuna mwanataaluma yeyote duniani asiyewajua hawa weheshimiwa, kwa sababu waliamini kuwa wanaweza na ipo siku watafanya makubwa zaidi.

Ukitaka kufanya makubwa katika uwanja wa elimu kama mwanafunzi, fanya mambo haya sita:

Moja, weka malengo. Kuwa na ndoto itakayokuwezesha kufikiri kila siku kuwa utafikaje pale. Kuna ndoto ya usiku na ndoto ya mafanikio. Ndoto ya usiku ni ile unayoota baada ya kulala ila ndoto ya mafanikio ni ile inayokufanya ukose usingizi kwa kufikiria kuwa utafikaje pale.

Ukiwa huna ndoto, wewe bado huna mbawa japo unatamani kupaa.Ndoto ndiyo inayotengeneza mbawa na kukufanya upae kifikra.

Pili, shirikiana na wanafunzi wenye malengo sawa na yako au wanaokuzidi. Ukitaka kukuza akili yako na uelewa wako, shirikiana na wanafunzi waliokuzidi katika eneo fulani ili wakupe changamoto ya kukufanya usome zaidi na kujua vile ambavyo ulikuwa huvijui.

Ukizungukwa na watu uliowazidi,siku zote utajiona kuwa unaweza au unajua kumbe unajua katika kundi la wasiojua.Kujua ni kujua katika kundi la wanaojua.

Tatu, kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Watu wote waliofanikiwa duniani ni wale wenye nidhamu ya hali ya juu kwenye kila kitu- nidhamu ya muda, nidhamu kwa wote waliokuzidi kiumri na wale waliochini yako.

Jifunze kufanya vitu kama vile kuna mtu anakutazama hali ya kuwa uko peke yako, hiyo ndiyo nidhamu ya kweli na siyo kuwa na nidhamu kwa sababu kuna watu wanakuangalia au wanakusimamia.

Nne, jaribu vitu mbalimbali hili uweze kujua uwezo wako. Shiriki katika michezo, shiriki katika uandishi wa insha na vitabu, shiriki katika makongamano ya kitaalamu haya yote yatakufanya ujue kipaji chako na uwezo wako ulipo na hivyo itakuwa rahisi kukiendeleza hicho kipaji ulichokigundua.

Tano, kuwa mfanyaji mzuri wa ibada kwani Mungu huwasaidia wenye jitihada na wenye kumcha yeye (wenye kumtegemea yeye tu).

Mungu huwasaidia wenye kumkumbuka yeye mara kwa mara.Siri ya mafanikio iko katika ibada na jitihada.

Sita, kuwa na kiigizo na mlezi madhubuti. Ikiwa unataka kuendelea, kuwa na mtu ambaye utakuwa unamuiga katika kile anachofanya.

Ila kumbuka, iga baadhi ya vitu, usiige vyote kwani upekee wako utakosekana endapo utaiga kila kitu.

Dunia inataka upekee wako wa uwezo na haiba yako ili na wewe baadaye uwe kiigizo chema kwa watu au katika jamii yako.