Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Kinyaiya atia neno kupumzika Dk Mpango

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akisalimiana na Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Wilbroad Kibozi (kulia) wakati wa adhimisho la sadaka ya  misa takatifu ya daraja la  ya upadri  kwa mashemasi watatu katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Lodochowska jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Januari 18, 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kukubali ombi la Dk Mpango kupumzika.

Dodoma. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya amesema alichofanya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuamua kupumzika si cha kawaida kwa kuwa wengine wanang’ang’ania nafasi za uongozi.

Januari 18, 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kukubali ombi la Dk Mpango kupumzika. Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi alipitishwa kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.

Askofu Kinyaiya amesema hayo leo Julai 5, 2025 wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya daraja ya upadre kwa mashemasi, Sajilo Mark SJ, Damian Mtanduzi na Joseph Ibrahim linalofanyika katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, jijini Dodoma.

Amesema pamoja na Watanzania kumpenda Dk Mpango na wangependa aendelee lakini ameamua kupumzika.

“Kwa kweli ninamsifu kwa ujasiri huo, si kawaida watu wanang’ang’ania yeye anaachia. Sasa kwa sababu sidhani kama atapata nafasi nyingine ya kuwa na jimbo zima nitampa nafasi kwa speech (hotuba) kwa sababu anastahili na tunaona fahari ya kuwa na Mkristu mwenzetu,” amesema.

Askofu Kinyaiya amewataka Watanzania kushiriki katika uchaguzi ili kuwachagua viongozi wanaowataka.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akizindua jengo la katekesi katika Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska jimbo kuu la Dodoma, (kushoto) Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma Beatus Kinyaiya.

 “Mwaka huu ni wa uchaguzi Oktoba, niwaombe Watanzania twende tukapige kura, kwa sababu usipopiga kura watakuchagulia ambaye humtaki ndiyo maana yake. Ukifikiri nikae nyumbani ndiyo mwisho, imekula kwako kwa hiyo ninaomba twende tukapige kura,” amesema.

Amewataka kwenda kupiga kura na kumchagua mtu ambaye anaweza na si aliyekupa kitu chochote.

Pia ametoa wito kwa wazazi kuwaachia watoto wao waende seminari ili wawe mapadri na kuwatumikia Watanzania.

Askofu Kinyaiya, kama Mkurugenzi wa Benki ya Mkombozi, amesema benki hiyo inafanya vizuri na mwaka jana ilipata faida kubwa, hivyo mwaka huu wote walioweka hisa watapata gawio.

“Wote wenye hisa ndani ya Mkombozi Benki mkae mkao wa kula hela inakuja na tunatoa gawio kwa kiasi ambacho hakuna benki imewahi kutoa nadhani benki moja tu kubwa,” amesema Askofu Kinyaiya.

Akizungumza na waumini, Dk Mpango amewaomba mapadri, watawa na waumini kuliombea Taifa wakati linaingia katika uchaguzi mkuu.

“Ninaomba sana sala za kila mmoja ili Taifa letu lipite salama nchi yetu ibaki na umoja na amani lakini pia tutimize wajibu wetu wa kuchagua viongozi ambao wana hofu ya Mungu katika kuwatumikia Watanzania,” amesema na kuongeza:

“Kwa wana Kiwanja cha Ndege mimi nitabaki ni mwana K|Ndege, nimemuiga kaka yangu mheshimiwa Mizengo Pinda (Waziri Mkuu Mstaafu) yeye yuko Zuzu (Dodoma) mimi nitakuwa Mayamaya (Dodoma).”

Kuhusu mapadri wapya, Askofu Kinyaiya amewataka kuweka mkazo katika malezi ya familia kwa sababu nyingi zimekuwa na matatizo na kuvunjika kwa kukosa mtu wa kuwasindikiza.

“Hata hao mnaowaona wakikimbia huko na huko kutafuta mahubiri kutafuta udongo ni kwa sababu hawana imani ya ndani, ndiyo mahangaiko hayo. Wasaidieni watu wapate amani watulie,” amesema.

Pia amewataka kuwasaidia vijana ambao watu wanalalamikia maadili kupinda na kwa Taifa zima.

Askofu Kinyaiya amesema kila mmoja ameitiwa utume wake, hivyo atimize wajibu wake kwenye eneo lake.