Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walichozungumza Dk Mpango, Ho Duc Phoc wa Vietnam

Muktasari:

  • Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango yupo nchini Hispania kushiriki Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Ho Duc Phoc, yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika jijini Sevilla nchini Hispania.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano ulipo baina yake na Vietnam ambao umedumu kwa miaka 60 sasa. Amesema Vietnam ni kati ya nchi za kwanza kufungua ubalozi baada ya uhuru na kushirikiana na Tanzania kupitia Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wananchi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Julai 1, 2025 na Ofisi ya Makamu wa Rais, imemnukuu Dk Mpango akisema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo na Vietnam ikiwemo kuunga mkono kwenye masuala yenye masilahi ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa.

Makamu wa Rais amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanznia na Vietnam unapaswa kuongezwa zaidi katika uwekezaji, kilimo, biashara masuala ya ulinzi na kushirikiana pia katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Ameishukuru Serikali ya Vietnam kwa kuridhia soko la bidhaa mbalimbali za Tanzania kama vile korosho na bidhaa za misitu.

Makamu wa Rais ameipongeza Vietnam kwa kuandaa Tume ya Kwanza ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC) mwaka 2014 na kuihakikishia kwamba Tanzania itaandaa Tume ya Pili ya Pamoja ya Ushirikiano mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ameikaribisha Vietnam kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kama vile kilimo, viwanda vya nguo na vingine vya uzalishaji.

Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Ho Duc Phoc ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Vietnam katika majukwaa ya kimataifa na hivyo kudumisha ushirikiano mzuri uliopo.

Amesema ushirikiano wa kiuchumi unaendelea kuimarika ambapo Tanzania inatumia soko la Vietnam kuuza korosho na bidhaa za misitu na kila mwaka mauzo ya biashara hizo hufikia dola milioni 150.

Amesema uchumi wa mataifa hayo mawili unaendelea kutegemeana kwa kuwa Vietnam inazalisha bidhaa zinazouzwa nchini Tanzania ikiwemo mavazi na chakula.

Ameongeza kwamba ni vema kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi kwa kuwa bado yapo maeneo ambayo yanaweza kuwekezwa zaidi kupitia mashirika mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji ya Vietnam.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo wa Denmark, Elsebeth Søndergaard Krone, yaliyolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimaendeleo baina ya nchi hizo mbili.

Makamu wa Rais ameishukuru Denmark kwa mchango iliotoa katika maendeleo ya Tanzania kwenye  sekta mbalimbali za uchumi ambazo zimebadili maisha ya Watanzania ikiwemo miundombinu, sekta ya fedha, afya, maji na mengineyo.

Mazungumzo hayo yamesisitiza ushirikiano wa kimkakati zaidi katika biashara na uwekezaji na sekta zingine zenye manufaa kwa pande zote mbili ikiwemo nishati, mazingira, kilimo janja, miundombinu na kuiwezesha sekta binafsi.

Halikadhalika, Makamu wa Rais ameshiriki mkutano wa pembezoni wa nchi zinazoendelea (LDCs) ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Nepal,  Kadga Sharma  na kuhudhuriwa na mataifa rafiki yaliyoendelea. Mkutano huo umejadili tathimini ya utekelezaji wa azimio la mkutano wa tano wa nchi hizo uliofanyika Doha nchini Qatar mwaka 2023.

Aidha Mkutano huo umelenga kupanga mikakati katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza tangu azimio la Doha hususan masuala ya ufadhili pamoja na kuweka msisitizo katika kuongeza jitihada za kukusanya mapato ya ndani, ili kufikia lengo la asilimia 13 ya pato la Taifa.