Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi: Tunawashikilia wanne Chaso Mbeya, yataja sababu

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Chadema (Chaso) Mkoa wa Mbeya, Noah Mwalwange. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Chadema (Chaso) Mkoa wa Mbeya, Noah Mwalwange; Katibu wake, Gwamaka Mboka; Mwenyekiti wa mtandao huo tawi la CUOM, Agustino Wasinyo; na mwanafunzi wa CUOM, Rojas Mpwani.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata watu wanne, wakiwemo viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha vurugu na uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Chadema (Chaso) Mkoa wa Mbeya, Noah Mwalwange; Katibu wake, Gwamaka Mboka; Mwenyekiti wa mtandao huo tawi la CUOM, Agustino Wasinyo; na mwanafunzi wa CUOM, Rojas Mpwani.

Taarifa ya polisi inakuja saa chache baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya, kutoa taarifa ya kutoweka kwa wanne hao, akisema walikuwa katika ofisi za Chadema.


Taarifa ya Bavicha

Katika taarifa yake, Bavicha mkoani Mbeya imesema wanne hao walikamatwa jana, Jumamosi, Julai 4, na watu waliojitambulisha kuwa askari polisi waliovalia kiraia.

“Askari hao walikuwa na gari aina ya Toyota Hilux nyeupe,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Bavicha imelitaka Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kueleza sababu za kushikiliwa kwa viongozi hao na kituo walichopo.

“Sisi vijana hatuamini katika uonevu na ubaguzi kama njia za kulinda na kutunza utulivu na amani ya nchi yetu,” imeeleza.


Jeshi la Polisi

Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya leo Jumapili, Julai 5, 2026 limesema linawashikilia watu hao kwa tuhuma za kukutwa wakipanga na kuhamasisha watu kufanya vurugu na uhalifu mwingine katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.

“Watuhumiwa hawa walikamatwa Julai 4, 2026 saa 10 jioni katika eneo la Mafiati lililopo Kata ya Maanga, Jiji la Mbeya,” amesema.

Amesema ushahidi unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuatwe dhidi yao.

Aidha, jeshi hilo limetoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha kujiingiza katika vitendo vya kupanga na kuhamasisha uhalifu katika Jiji la Mbeya, kwani hatua kali kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa dhidi yao.