Prime
Hizi ndizo aina za waume, uko kundi gani?

Muktasari:
- Mara nyingi kwenye ndoa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanawake walioolewa “wake”, na malalamiko haya yanaelekezwa kwenye namna waume zao wanavyoishi au wanavyofanya
Dar es Salaam. Mara nyingi kwenye ndoa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanawake walioolewa “wake”, na malalamiko haya yanaelekezwa kwenye namna waume zao wanavyoishi au wanavyofanya.
Huyu analalamika mume wangu yuko hivi, na yule naye anasema mume wangu yuko vile. Mmoja anasema mume wangu anafanya hivi na mwingine analia mume wangu hafanyi vile.
Huu mkanganyiko umekuwa mkubwa sana na unasababisha maumivu kwa wake zetu. Ndio maana nimeamua kuna na makala haya itakayo kusaidia kufahamu kuwa wanaume pamoja na kwamba wanafanana kijinsi, lakini kwenye tabia zao katika ndoa wanatofautiana sana.
Labda kwa kuisoma makala haya utajigundua kuwa wewe ni mume wa aina gani (kama wewe ni mume) na labda pia utamgundua mume wako yuko kundi gani kwa kuangalia namna tabia yake ilivyowakilishwa, Nakutakia usomaji mwema na wa kuelewa.
Mume bachela
Mume wa aina hii anapenda sana kufanya mambo kivyake pasipo kumshirikisha mke wake. Anapenda sana kuvinjari na kuwa na marafiki zake sana na sio mke wake, anaweza akashinda baa akajisahau kabisa kama ana mke na watoto, akiwa na rafiki zake anajisikia furaha zaidi kuliko anapokuwa na mkewe au watoto wake. Hata wakipanga kwenda ‘mtoko’ na mkewe basi lazima atawaita na rafiki zake kadhaa wajumuike naye.
Mkikaa pamoja na yeye na marafiki zake basi mke fahamu ndio umetengwa kabisa, wataanza kuongea mambo ya ligi ya Uingereza, warudi ligi ya Tanzania halafu wakichoka mpira wahamie siasa, mpaka hapo kichwa kimeshakuuma unatamani kwenda ukajikunyate na watoto wako nyumbani.
Wanaume wa hivi kwa kweli hawamaanishi sana kwenye masuala ya ndoa. Wao ndoa huichukulia kirahisirahisi tu. Mara zote ni watu wasiionyesha kupevuka au kukua kwenye mambo yanayohusiana na ndoa au familia.
Mume tindikali
Yeye anachemka kama tindikali kila wakati. Mkali hatari. Ana fujo hatari. Ngumi mkononi. Ukimjibu tu kidogo umeisha.
Ukinyamaza anasema kwanini hutaki kujibu anachoongea, kwahiyo anaweza kukuadhibu kwa kumdharau.
Kila mara ni mbabe kwenye kila jambo. Kiufupi ni mume hatari sana na wa kumwogopa wakati wowote ule maana hujui ataamka na kipi
Mume mtumwa
Waume wa namna hii kila mara kiu yao ni kutaka wafanyiwe na kuheshimiwa kama wafalme ila wao wanawafanya wake zao kama watumwa. Kila mara huwahimiza sana wake zao kufanya mambo ya mila na tamaduni za zamani katika kuonyesha heshima kwao, hata kitu ambacho anaweza kufanya yeye atataka mke afanye maana ni kazi ya mwanamke.
Akiangusha kitu mke ndio aje aokote. Hawa ndio wale mara nyingine wanataka mke amsalimie shikamoo baba nanihii, au shikamoo mume wangu. Huwezi kumsalimia mume wako bila ya kupiga goti au kuinama maana ni dhambi.
Mara nyingine waume wa aina hii hawapendi kabisa kuitwa kwa majina yao ya kwanza, wanapenda kuitwa kwa majina ya ukoo au ya watoto wao, ukimwita jina lake anaona ni dharau kubwa sana.
Mume wa jumla
Mwanaume wa hivi ni mume wa kila mwanamke. Utaona anawajali wanawake wengine kuliko anavyomjali mke wake. Atawasifia wanawake wengine walivyopendeza na walivyo wazuri wakati mke wake wala hajawahi kusikia sentensi kama hizo kwenye kinywa cha mumewe.
Hata kama hana uhusiano na hao wanawake lakini utaona anapenda sana kuwasaidia hususani kuwapa pesa wakati hata siku moja hawezi mpa pesa mkewe.
Ukiwachunguza marafiki zao wengi ni wanawake kuliko wanaume. Ni mkarimu sana kwa wanawake wengine lakini sio kwa mkewe. Anaweza kuwa rafiki sana kwa marafiki wa mke wake kuliko alivyo rafiki kwa mke wake.
Mume mkavu
Mume huyu hujui saa ngapi ana furaha na saa ngapi kabadilika. Ni ngumu sana kuzielewa hisia zake.
Unaweza kufikiri ana furaha maana alikuwa anacheka ghafla ukimgeukia unaona kashanuna. Wabakhili sana wanaume wa hivi. Hawajali kabisa hisia za wake zao.
Anaweza kusema neno kavu na chungu mkewe akaumia hata kutoa chozi lakini yeye bado tu anaendelea kubwabwaja maneno bila kujali kuwa amemuumiza mwenzake kihisia. Wanaume wa hivi hawana muda wowote kwenye kuweka jitihada katika uhusiano wao ili penzi linoge.
Wao wanadhani uhusiano mzuri unakuja tu wenyewe, mkikosana, wewe ndio utahangaika sana kwenye kutafuta suluhu yeye yupo tu wala hana habari. Kiufupi ni kwamba waume wa aina hii, hawana utu.
Mume panadol
Hawa mara zote huwatumia wake zao kama mashine za kutatua matatizo yao. Wanawapenda wake zao pale ambapo mume anapohitaji kitu fulani na akishafanikiwa kupata ufumbuzi wa hitaji lake basi mke yule hafai tena.
Waume wa jinsi hii ni wenye akili sana na wajanja, wanajua kila udhaifu wa wake zao na wanatumia udhaifu huo kupata wanachokitaka kutoka kwa wake zao. Mumeo yuko kundi gani?