Prime
Misingi mitano ya upendo imara kwenye ndoa

Muktasari:
- Ndoa ni sawa na jengo, ili liwe imara unahitaji kuwa na msingi madhubuti. Ni ipi hiyo?
Dar es Salaam.Unataka kuwa na ndoa imara na unayoweza kudumu ndanimwe kwa miaka nenda rudi?
Safu hii leo inakuangazia baadhi ya mambo unayoweza kufanya ili kujenga ndoa imara maishani mwako.
Mosi, heshima. Upendo hustawi katika nyumba yenye heshima. Mtoto hushikamana na wazazi wake akitumaini kwamba watatimiza mahitaji yake, lakini uamuzi wa kupenda daima unaanzia na heshima. Tunapochagua rafiki au mpenzi, kwanza tunawatambua kwa sababu tunawapenda, ama kwa kuwa wana sifa fulani ambayo tungependa kuwa nayo. Tunawaheshimu kwa sababu fulani hata ingawa sababu hiyo haiko wazi katika akili zetu.
Pili, urafiki . Baada ya heshima kinachofuata ni urafiki. Urafiki ni muhimu katika kila aina ya upendo. Hata katika uhusiano wa kimahaba urafiki ni muhimu.
Baadhi ya watu wanaamini kwamba urafiki katika ndoa na uhusiano wa muda mrefu ni muhimu zaidi hata kuliko upendo wenyewe. Huenda ni kwa sababu urafiki ni kiungo muhimu katika msingi wa upendo. Pasipo urafiki haiwezekani kuwa na upendo.
Tatu, uelewa ama huruma kama tunavyopenda kuuita ni muhimu sana ili kutokeza upendo. Mara nyingi katika uhusiano wa muda mrefu, sifa hii inaanza kupotea kwa sababu ya kukazia fikra upande usiofaa wa uhusiano.
Nne, mawasiliano. Mawasiliano ndio msingi wa upendo, ni msingi wa mawasiliano ya aina yote na uhusiano katika maisha yako.
Bosi, wafanyakazi, wauza maduka wote wanahitaji kuwa na mawasiliano mazuri. Kiuhalisia, upendo unajengwa na mawasiliano. Licha ya mawasiliano ya kila siku, mtu anapaswa kuwasiliana kwa upendo na watu wengine.
Ikiwa hili haliwezekani, basi hakuna ushirika au uhusiano wenye nguvu, kitu ambacho ni muhimu ili kuwasilisha upendo kwa kila mtu.
Tano, ushirikiano. Ushirikiano ni zaidi ya urafiki wa kawaida. Ushirikiano unaonyesha uhusiano kamili, ukaribu, na hata mfungamano wa maisha. Hata hivyo, unaonyesha uhuru kwa kiasi fulani.
Unaruhusu mwenza wako aishi maisha yake. Rafiki ni mtu unayewasiliana naye kuhusu kila kitu, lakini mshirika wako ni mtu ambaye anakusaidia, lakini unamruhusu afanye uamuzi wake mwenyewe wa kumsaidia. Sasa umeona ni kwa nini upendo wa kweli unachochea urafiki na ushirikiano kwa pamoja!
Ikiwa una sifa hizi, basi upendo wako una msingi imara. Uhusiano haupaswi kuwa kama fremu mbili tu.
Haupaswi kuwa ni kuishi na mtu unayefahamiana naye au mtu ambaye uliishi naye tu kwa miaka mingi, uhusiano unapaswa kuwa ni kuishi na mtu ambaye unampenda.
Msingi wa upendo katika uhusiano wako ukoje? Hujachelewa sana kuanza kujenga uhusiano wako katika misingi hii.
Mawasiliano bora na yenye ufanisi
Mawasiliano bora ni muhimu sana kwa mafanikio yetu katika nyanja mbalimbali. Kama hatuna mawasiliano yaliyo bora au hatuwezi kuwasiliana inavyotakiwa, itakuwa ngumu kwa watu wengine kutusaidia katika kile tunachokihitaji. Mawasiliano yasiyo bora au kushindwa kuwasiliana vema kunadumaza na mara nyingine kuua kabisa uhusiano baina yetu na wengine.
Kwa maana hii basi hauna budi kuzingatia sana maelezo na ushauri kutoka katika mada hii na kuyaweka maelezo haya katika matendo ili yakusaidie maishani.
Vitu vya kuzingatia. Yatazame au yachukulie mazungumzo yako na wale unaohusiana nao kama majadiliano ya kawaida tu na sio mashindano.
Hii itakusaidia kuwa na uhusiano na mawasiliano bora na wengine hususani pale utakapoyaona yale mnayozungumza mara kwa mara kama majadiliano na siyo mashindano.
Majadiliano ni mazungumzo yenye kusudi la kufikia suluhisho au mwafaka fulani. Ni mazungumzo ambayo yanapotumika nia yake siyo kumuumiza, kumuumbua mtu bali kutoa nafasi kwa pande zote kufikia matokeo bora.
Mazungumzo yenye ushindani ni yale yenye nia ya kuumiza, kuumbua, kuaibisha, na kudharaulisha, na ambayo nia yake ni kumuonyesha mshindi na aliyeshindwa mwishoni mwa mazungumzo hayo.
Wale wenye tabia ya kuzungumza kiushindani huyachukulia mazungumzo kama nafasi ya kuonyesha ubabe au kunyanyasa wengine.
Hata kama yule mnayezungumza naye ana nia ya mashindano, wewe fanya majadiliano ya kawaida ili taratibu uweze kumbadilisha mtazamo wake.
Kuwa msikilizaji makini na hitaji kusikilizwa pia. Kati ya alama za kuonyesha kuwa wewe ni mwenye mawasiliano bora ni pamoja na uwezo wa kuwa msikilizaji mzuri.
Wako watu ambao hupenda kuongea tu na sio kusikiliza. Sambamba na hilo, unatakiwa kuomba na wewe pia usikilizwe vizuri.
Muombe yule anayekusikiliza akuache umalize kuongea ndio na yeye aanze kuongea. Kamwe hamtafikia mwafaka wowote ikiwa wote wawili mnaongea kwa wakati mmoja.
Yafuatayo yatakuwezesha kuwa msikilizaji mzuri: msikilize yule anayeongea kwanza na kumuelewa; fahamu fika kile kinachozungumzwa elewa nia na madhumuni ya majadiliano; uliza swali pale unapodhani hujaelewa ili uweze kuelewa vema nia ya mzungumzaji.
Jaribu kuweka kwa kifupi au kwa muhtasari kile kilichozungumzwa, mweleze anayezungumza unavyojihisi juu ya alichokuwa akikieleza, na hakikisha ulimuelewa vema. Eleza unavyofikiri wewe. Mweleze aliyekuwa anazungumza kama umekubaliana naye au la, toa sababu za kukubaliana au kutokukubaliana.