Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tapa yatwishwa zigo la mmomonyoko wa maadili

New Content Item (1)

Washiriki na Wanachama wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA) wakiendelea kujadililiana masuala mbalimbali ya kisaikolojia katika Kongamano la 2 la Kisayansi na Mkutano wa 9 wa TAPA, linalofanyika katika ukumbi wa Gentle Hills, mkoani Iringa.

Muktasari:

  • Mmomonyoko huo umetajwa kuwa chanzo kikuu cha kushuka kwa tija ya kitaifa, migogoro ya kifamilia, udhaifu katika uongozi, pamoja na ongezeko la msongo wa mawazo miongoni mwa wananchi.

Iringa. Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa) kimetakiwa kuchukua hatua za haraka na za kisayansi katika kuimarisha afya ya akili ya wananchi, kama njia muhimu ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kushamiri nchini.

Mmomonyoko huo umetajwa kuwa chanzo kikuu cha kushuka kwa tija ya kitaifa, migogoro ya kifamilia, udhaifu katika uongozi, pamoja na ongezeko la msongo wa mawazo miongoni mwa wananchi.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Juni 12, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Nuru Sovellah wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Kisayansi na Mkutano wa tisa wa Tapa unaofanyika katika ukumbi wa Gentle Hills, mkoani Iringa.

Sovellah amesema hali ya sasa inaonesha namna matatizo ya kisaikolojia yanavyoharibu mwenendo wa jamii na kuchochea kuporomoka kwa misingi ya maadili.

Amesema ni wajibu wa wanasaikolojia wa Tanzania kuibuka na mbinu mpya za kisayansi zitakazosaidia kurejesha misingi ya utulivu, uwajibikaji na uzalendo katika jamii.

“Jamii yenye afya bora ya akili ndiyo msingi wa maadili, mshikamano na maendeleo ya kweli. Tapa mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha elimu ya afya ya akili inamfikia kila Mtanzania kuanzia shuleni hadi kazini,” amesisitiza Sovellah.

Aidha, ameipongeza Tapa kwa juhudi kubwa ya kutoa elimu kwa umma kuhusu afya ya akili na mchango wake katika kukuza taaluma ya saikolojia nchini.

Rais wa Tapa, Magolanga Shagembe amesema  kongamano hilo lina lengo la kubadilishana maarifa ya kitaaluma na kuimarisha uwezo wa wanasaikolojia nchini kukabili changamoto za sasa, hasa zile zinazoathiri maadili na afya ya akili kwa jamii.

New Content Item (1)

Washiriki na Wanachama wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA) wakiendelea kujadililiana masuala mbalimbali ya kisaikolojia katika Kongamano la 2 la Kisayansi na Mkutano wa 9 wa TAPA, linalofanyika katika ukumbi wa Gentle Hills, mkoani Iringa.

Shagembe amesema kwa mara ya kwanza, kongamano hilo linafanyika katika Kanda ya Kusini, mkoani Iringa na linafanyika kwa siku mbili.

“Huu ni mwanzo wa mageuzi makubwa kwenye fani ya saikolojia nchini. Tunatarajia kutoka na maazimio yatakayoweka dira ya kitaifa kuhusu afya ya akili,” amesema Shagembe.

Kongamano hilo pia linaangazia mchango wa wanasaikolojia katika kusaidia waathirika wa majanga.

Katibu Mkuu wa Tapa, Barnabas Nkinga amesema tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2009, kimekuwa kikitoa huduma za kisaikolojia kwa jamii, kusaidia waathirika wa matatizo ya afya ya akili na kushiriki katika tafiti mbalimbali za kuboresha ustawi wa jamii.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa Maofisa Ustawi wa Jamii Tanzania Bara, Martin Chuwa amesema hali ya afya ya akili nchini inatia wasiwasi, akibainisha kuwa baadhi ya watu wamepoteza uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa kutokana na matatizo ya kisaikolojia.

Hivyo amewasihi wanasaikolojia kufanya tafiti za kina kuhusu masuala ya afya ya akili, kuvunjika kwa ndoa, kuporomoka kwa maadili na changamoto nyingine ili kusaidia Serikali kupanga mikakati madhubuti ya ustawi wa jamii.

Akizungumzia suala la ‘machawa wa kisasa’, Shagembe amesema changamoto kama hizo zinachochewa zaidi na ukosefu wa utambuzi wa mtu binafsi kuhusu malengo yake ya maisha.

Naye Mhadhiri wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki amesema matatizo mengi ya kisaikolojia yanasababishwa na shinikizo la kutaka mafanikio ya haraka bila kuzingatia misingi halali.

Amehimiza jamii kufundishwa kuhusu uvumilivu, nidhamu ya akili na ujasiri kama misingi ya ustawi wa kisaikolojia.

Katika mjadala huo, wanachama wa Tapa wameelezea mafanikio ya chama hicho katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, walimu na wazazi juu ya namna ya kutambua viashiria vya matatizo ya afya ya akili na kuchukua hatua mapema.