Kinachowasibu wazazi malezi bora kwa watoto

Muktasari:
- Wazazi wengi hujikuta wakifanya kazi kwa muda mrefu ili kukidhi mahitaji muhimu ya familia na kusahau suala zima la malezi kwa watoto wao.
Katika ulimwengu wa kisasa unaoendeshwa na maendeleo ya teknolojia na utandawazi, wazazi wengi wanakumbana na changamoto zinazobadilisha mbinu zao za malezi.
Hali hii inawafanya baadhi kuonekana kama wameacha majukumu yao ya msingi.
Ni muhimu basi kuchunguza chanzo cha hali hii na nini kifanyike ili kukabiliana nayo.
Hivi karibuni nikiwa kwenye mihangaiko yangu nilikuta na Sabina Mrindoko, mtaalamu wa malezi na saikolojia ya watoto.
Miongoni mwa mambo tuliyozungumza ni pamoja na hili jambo.
Mrindoko aliniambia kuwa mara nyingi wazazi wengi hujikuta wakifanya kazi kwa muda mrefu ili kukidhi mahitaji muhimu ya familia na kusahau suala zima la malezi kwa watoto wao.
Anasema hali hiyo sasa huwafanya wazazi wengi kuwa na muda mfupi wa kushughulika na malezi.
Sasa hilo likanikumbusha namna wazazi ambao ni waajiriwa wanavyotoa kipaumbele cha kazi za ofisi badala ya familia.
Hili halina ubishi, kila mmoja anashuhudia kwamba kazi nyingi za ofisini zinaweza kuwa kikwazo kingine kinachowazuia wazazi kuwa karibu na watoto wao.
Upungufu huu wa muda unawapa watoto nafasi kubwa ya kupata taarifa mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, ambazo wakati mwingine zinaweza kuwa na maudhui yasiyofaa au yenye upotoshaji bila wazazi kujua.
Sambamba na hilo, wazazi wengi hutumia muda mwingi kwenye simu na mitandao ya kijamii.
Katika hili, Mrindoko pia aliniambia hali hiyo nayo inapunguza mawasiliano ya ana kwa ana na watoto, jambo ambalo linadhoofisha uhusiano wao.
Pia, wazazi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu athari za teknolojia na utandawazi kwa watoto wao. Kutokana na pengo hili la ufahamu, wanashindwa kupanga mikakati thabiti ya malezi inayolingana na mazingira ya sasa.
Na wanapojaribu kukabiliana na mazingira tofauti na yale waliyokulia, mara nyingi wanashindwa kuchagua mbinu bora za malezi.
Lakini pia tukumbuke kuwa utandawazi umeleta tamaduni mpya ambazo zinawafanya baadhi ya wazazi kuona njia za malezi za kitamaduni kuwa zimepitwa na wakati, hivyo kuamua kuiga mitindo ya malezi ya mataifa mengine ambayo wakati mwingine hayafai katika mazingira ya Tanzania.
Wazazi wengine wameamua kukabidhi jukumu la malezi kwa walimu, wafanyakazi wa nyumbani au vifaa vya teknolojia kama runinga na kompyuta.
Hii nayo inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza nafasi yao ya kuwa karibu na watoto wao na kudhibiti tabia mbaya wanazojifunza nje ya familia.
Hata hivyo, bado kuna nafasi ya kubadilisha hali hii, kwa sababu wazazi wanaweza kuanza kwa kujipangia ratiba itakayowawezesha kuwa na muda wa kutosha wa kukaa na watoto wao.
Ni muhimu pia kujifunza kuhusu athari za matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto na kuweka mipaka inayofaa.
Hii itawasaidia kujua mbinu bora za malezi zinazoendana na teknolojia kwa ustawi wa watoto.
Teknolojia ni sehemu muhimu ya ulimwengu kwa sasa, hivyo wazazi wanapaswa kujiongeza kwa kuzuia mianya ambayo watoto wanaweza kujifunza mambo yasiyofaa.
Ili kudhibiti hili, ni muhimu kupanga muda maalumu kwa watoto kutumia vifaa vya kidijitali na kuhakikisha kuwa maudhui wanayoyapata yanafaa kwa umri wao.
Hii itasaidia kuwalinda dhidi ya maudhui yanayoweza kuharibu maadili yao.
Zaidi ya yote, ni muhimu kuzingatia umuhimu wa kuenzi na kuwafundisha watoto maadili ya kitamaduni ambayo yanawajenga kuwa raia wema. Hali hii itawasaidia kuwa na nidhamu, kuwajali wengine na kuwa na msimamo bora na hata wanapokumbana na changamoto za kimtandao au kijamii.
Changamoto za malezi katika enzi hizi za utandawazi na teknolojia zinahitaji ufahamu na mbinu mpya kutoka kwa wazazi kila mara.