Prime
Yajue matarajio manne yanayowaumiza wapenzi

Muktasari:
- Kwenye tasnia ya saikolojia tunasema kitendo cha kuwa na matarajio makubwa ni chanzo kikubwa sana cha msongo wa mawazo.
Dar es Salaam. Bahati mbaya watu wengi leo hulalamika sana kuwa uhusiano na mapenzi, vimekuwa chanzo cha maumivu na masononeko tofauti na ilivyotarajiwa.
Inajulikana kwamba uhusiano ni sehemu ya watu kufurahia, kuwa na vicheko na amani wakati wote.
Pamoja na ukweli huu, bado pia tafiti zinaonyesha kwamba baadhi ya mazingira yanayosababisha maumivu na migongano kwenye uhusiano ni ile hali ya mmoja au wote kuwa na matarajio zaidi kuliko uhalisia.
Kwenye tasnia ya saikolojia tunasema kitendo cha kuwa na matarajio makubwa ni chanzo kikubwa sana cha msongo wa mawazo.
Katika makala haya nina kwenda kukuchambulia kwa kifupi matarajio manne ambayo yameonekana kuwaumiza wapenzi wengi.
Kutegemea au kutarajia mtu mwingine kukupa furaha
Kwa bahati mbaya wengi wetu hatuandaliwi ipasavyo na kufundishwa kuhusu uhusiano kabla hatujaingia huko. Elimu na hata mazungumzo ya uhusiano katika jamii za Kiafrika havipewi kipaumbele sana kwahiyo wengi tunaingia kwenye uhusiano hatufahamu kwa undani baadhi ya vitu muhimu.
Kitu kimojawapo muhimu ambacho wengi wanaoingia kwenye uhusiano hawakifahamu ni mmoja kutarajia au kudhania kwamba anapoingia kwenye uhusiano, ni wajibu wa mwenzake kuhakikisha ana furaha.
Hapa namaanisha, mwanamke anaingia kwenye uhusiano akitarajia kwamba ni jukumu la mwanaume kuhakikisha mpenzi wake ana furaha. Sasa pale ambapo mwanaume huyu anashindwa kuyafikia matarajio haya, ugomvi unaanza.
Kamwe usitarajie kabisa kwamba ni jukumu la mwenzako kuhakikisha una furaha. Ukweli ni kwamba ni jukumu lako kabisa kuhakikisha unaweka furaha kwenye penzi lenu na unajitafutia furaha wewe mwenyewe kwanza. Mapenzi ni muunganiko wa watu wawili wenye furaha walioamua kufanyia kazi ili kuziongeza furaha zao na sio mmoja kutegemea kupewa furaha na mwingine.
Kudhania wengine wanafahamu unachowaza
Unapokuwa kwenye uhusiano unahitajika sana kuwa kuwasiliana kwa ubora. Unahitaji sana kuwasiliana katika hali ya juu maana uhusiano unaokosa mawasiliano mazuri, una shida.
Kuwasiliana maana yake kuyaweka bayana yote unayotaka mwenzako ayafahamu. Hautakiwi kuhisi au kudhania kwamba mwenzako ataelewa tu kwamba umekasirika, kwamba hajafurahia maneno yake, la hasha.
Usitarajie tu kwamba anafahamu ninachowaza, yeye sio malaika aweze kuingia akilini mwako au nafsini mwako aweze kuijua hasira yako au furaha yako.
Mwambie napenda hiki na hiki kifanyike na sipendi hiki au kile, kama umefurahi weka wazi na kama umesononeka pia weka bayana. Wako wengi ambao ndani yao wameumizwa lakini hawasemi chochote lakini ndani yao wanatamani sana kuambiwa samahani au pole.
Wanadhani mpenzi wake anajua tu kuwa ameumia, usifanye hivyo maana utaendelea kuumia na kuteseka wakati suluhisho unalo wewe mwenyewe.
Kutarajia kwamba kila mmoja atakubaliana na mawazo yako
Haiwezekani kamwe kila unachoongea au kila wazo unalolitoa basi kila mtu atakubaliana nalo. Kwa kutarajia hivyo basi unajiwekea mazingira makubwa ya kuumiza hisia zako na hata ugomvi baina yako na mpenzi wako.
Wako watu ambao wao huamini kila walisemalo au wazo wanalolitoa ni sahihi ingawa wao wanaweza kabisa kupinga mawazo ya wengine. Hii ni imani mbaya na watu wa jinsi hii wanashida sana kuishi kwenye uhusiano na wapenzi wao au hata na jamii inayowazunguka. Lazima ufahamu kwamba hakuna aliye mkamilifu hata mmoja, hatujakamilika kuanzia tukiwa kwa wazazi wetu, shuleni na hata tunapoingia katika uhusiano, sasa unawezaje kuwa na matarajio kwamba unaloliongea au kulipendekeza halitopingwa na yeyote?
Kwanini unawaza kwamba mawazo yako ni lazima yakubaliwe na wote? Kuwaza au kuamini hivyo maana yake ni kwamba wengine au huyo mpenzi wako mawazo yake wakati wote ni madogo au yasiyo tija, labda hilo ndilo linakupa uhakika huo.
Kutarajia kwamba unaweza kumbadili mtu
Bahati mbaya sana wako watu huingia kwenye uhusiano huku wanajua fika kuwa kuna tabia walizonazo wenza wao ambazo hawazipendi kabisa na kwasababu wako kwenye penzi, huwa hawawezi kuzikomalia tabia hizo kwahiyo wanajifanya kama wanazifumbia macho, wakiamini kwamba watazishughulikia hukosiku za mbele.
Wako wanaoamini kwamba huyu mtu atabadilika akipata watoto, wako wanaoamini kwamba atabadilika akishakuwa na majukumu ya mume au mke au familia, wako wanaoamini kuwa nikiingia kwenye ndoa nitahakikisha nambadilisha aache hiyo tabia yake.
Kwa bahati mbaya sana wengi wenye mawazo kama haya wameumia na kukatishwa tamaa pale walipokuja kugundua kwamba ni ngumu sana kumbadilisha mtu tabia yake aliyoizoea labda yeye mwenyewe aamue kubadilika.
Mabinti na wanawake wengi wameumizwa hisia zao baada ya kuona tabia za wanaume wao zinaendelea vile vile.Mbaya zaidi sasa hivi mtu huyu ndio kashakuwa mume na sio tu rafiki au “boyfriend” na yumkini wana watoto.
Ushauri wangu ni kwamba, bora uhakikishe unayaona hayo mabadiliko katika kiwango kinachokuridhisha wewe na sio usubirie ukitegemea eti atabadilika.
Punguza matarajio yasiyokuwa halisi katika uhusiano, itakusaidia kupunguza maumivu na kuongeza furaha.