Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekretarieti ya ajira yajitosa usaili wa walimu

Muktasari:

  • Usaili wa kada za ualimu kujaza nafasi 14,648 zilizotolewa na  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini,  ulianza tarehe 14 Januari, 2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Februari, 2025 Tanzania Bara na Zanzibar.

Februari 19, 2025 Sekretarieti ya ajira ilitoa ufafanuzi kuhusu mjadala wa usaili kwa walimu unaoendelea mtandaoni.

Taarifa ya ufafanuzi iliyotolewa na Lynn Chawala, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, ilieleza yafuatayo:

‘’ Usaili wa kada za ualimu kujaza nafasi 14,648 zilizotolewa na  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini,  ulianza tarehe 14 Januari, 2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 24 Februari, 2025 Tanzania Bara na Zanzibar.

Hadi tarehe 18 Februari, 2025, jumla ya walimu 6,055 waliofanya usaili na kufaulu wamepangiwa vituo vya kazi katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kukamilika kwa mchakato wa ajira zao.

 Ili kutekeleza dhana ya uwazi, usaili wa kada za ualimu unasimamiwa kwa ushirikiano wa viongozi kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma; Ofisi ya Rais (UTUMISHI); Ofisi ya Rais (Tamisemi); Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Tume ya Utumishi wa Walimu; taasisi nyingine za umma pamoja na ofisi za wakuu wa mikoa kote nchini.

Aidha, wataalam wanaohusika na usahihishaji wa mitihani ya usaili pamoja na wale wanaoshiriki kwenye majopo ya usaili wameratibiwa na Katibu wa Sekretareti ya Ajira kupitia ofisi za wakuu wa mikoa chini ya uratibu wa makatibu tawala wa mikoa. Matokeo ya usaili wa kada za ualimu yamekuwa yakiingizwa kwenye mfumo wa kidigitali wa ‘Ajira Portal’ mara baada ya usaili kukamilika kwenye vituo husika katika mikoa yote nchini.

Jukumu hili husimamiwa na timu za viongozi kutoka makao makuu-Dodoma na ofisi za wakuu wa mikoa. Wasailiwa waliofanya vizuri katika usaili huu wamepata fursa ya kuajiriwa na waliofaulu na kukosa nafasi katika usaili majina yao yataendelea kuhifadhiwa katika kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa msingi huu, Serikali ikitoa vibali vya ajira au nafasi za ajira zikipatikana kutokana na sababu mbalimbali watapangiwa vituo vya kazi bila kulazimika kurudia kufanya usaili.

Hivyo, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inapenda kuwakumbusha wale wote wanaotoa taarifa za kupotosha kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea nchini kote kuacha upotoshaji huo. Vilevile, tunawaomba wadau wote kupuuza upotoshaji huo kwani lengo la utaratibu huu ni kupata nguvu kazi ya walimu wenye uwezo na weledi watakaochangia katika kuifikisha nchi yetu katika malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

 Pia ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Toleo la 2 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023.

Tunawasihi wote wanaotafuta fursa za ajira katika Utumishi wa Umma wenye sifa stahiki wakiwemo walimu, kujiandaa vizuri kabla ya usaili, kujiamini na kushiriki katika usaili ili waweze kufaulu na kupangiwa vituo vya kazi kadiri nafasi za ajira zinapojitokeza.

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawahakikishia waombaji fursa za ajira kuwa mchakato wa ajira chini ya ofisi hii unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi bila ya rushwa wala upendeleo wowote.