Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapya yaibuka zuio la mikutano ya hadhara



Dar es Salaam/Dodoma. Wakati Serikali imetangaza kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vyote vya siasa nchini kutokana na kile ilichodai ni viashiria vya uvunjifu wa amani kuelekea maadhimisho ya Sabasaba, wadau wa siasa na sheria wameukosoa uamuzi huo wakisema unakiuka sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zuio hilo limetangazwa leo, Juni 26, 2026, bungeni Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi,alipokuwa akijibu mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Paschal Chinyele.

Hii ni mara ya pili Serikali kuweka zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Mara ya kwanza lilitangazwa mwaka 2016 chini ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, kabla ya kuondolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 3, 2023.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa zuio la mwaka 2016, uamuzi wa sasa umekosolewa na wadau wa siasa na sheria, wakisema unakwenda kinyume na Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatoa haki kwa kila mtu kukutana kwa amani na watu wengine, kutoa maoni hadharani na kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika kwa hiari yake.

Ibara hiyo inasema: "Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au masilahi yake au masilahi mengineyo."


Yaliyojiri bungeni

Katika mwongozo huo, Chinyele aliomba kufahamu kama Serikali inafahamu kuhusu kuwepo kwa tetesi za maandamano zinazosababisha taharuki miongoni mwa wananchi.

Mbunge huyo, pia, alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuwahakikishia Watanzania usalama wao na mali zao.

Spika wa Bunge, Mussa Zungu alimsimamisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Katambi, akimtaka kujibu mwongozo huo.

Akijibu mwongozo huo, Katambi amesema ni kweli kuna taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikisema kutakuwa na maandamano, japo hakuna sababu zinazotajwa kwenye taarifa hizo.

Amesema wapo wanaosema kutakuwa na maandamano lakini sababu hazitajwi, hata wale waliojaribu kutaja sababu, ni zile ambazo Serikali imezitolea suluhisho, mojawapo ni suala la Katiba mpya, ambalo lipo kwenye ilani ya CCM na hatua mbalimbali zimepangwa za kiserikali katika namna ya kuliendea.

Waziri Katambi amesema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama, na tayari wameanza kufuatilia viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, kwa yeyote anayepanga kuivuruga kupitia mitandao ya kijamii au moja kwa moja.

“Namwagiza IGP Camilius Wambura, atoe maelekezo kwa ma-RPC wote nchini, ambayo yatashuka kwa wakuu wa Polisi Wilaya mpaka kwenye Polisi Kata kuanza kufanya uratibu wa mipango ya kiusalama na kuiimarisha zaidi,” amesema Katambi.

Amesema hivi karibuni Tanzania inatarajia kuwa na ugeni katika Maonyesho ya Sabasaba ambapo inatarajia kupata wageni kutoka mataifa mbalimbali na kipindi hicho ndicho kinasaidia kujijumuisha katika kujenga uchumi wa nchi.

Hivyo, Waziri Katambi ameongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho kuna chokochoko hizi, hawataweza kumvumilia mtu yeyote ambaye atafanya vurugu za aina yoyote kwani ni kipindi ambacho wanatarajia shughuli zote za kiuchumi ziendelee.

“Namwelekeza IGP Wambura asitoe vibali kwa kazi zozote zitakazokuwa zinahusiana na kufanya mikutano ya hadhara katika kipindi hiki, kwa chama chochote, iwe Chama cha Mapinduzi, iwe chama chochote kile, kwa kipindi hiki.

“Ni vizuri tukarudi katika kuruhusu wananchi kujenga uchumi wa nchi yao. Ni katika kipindi ambacho tunahitaji kufanya kazi kuhakikisha kila Mtanzania, wafanyabiashara na wawekezaji wanafanya kazi zao kwa utulivu,” amesema.

Katambi amesema kuanzia kesho  Juni 27, 2026 wataanza kuwahoji watu tofauti ambao wamekuwa waziwazi, kwa ushahidi na vielelezo, wakichochea uvunjaji wa amani katika taifa hili, kufanya vurugu na wanazo video ambazo wamezungumza kwenye majukwaa mbalimbali.


Kinyume cha Katiba

Kufuatia uamuzi huo wa Serikali, Wakili Maduhu William amesema mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba inayolindwa na Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema haki hiyo pia inatambuliwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, ambazo zinaweka utaratibu wa vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.

Maduhu amesema inashangaza pia kauli ya Katambi kupiga marufuku mikutano ya hadhara imetolewa bungeni, mahali ambapo wabunge hulindwa na kinga ya kikatiba dhidi ya hatua za kisheria kwa kauli wanazotoa wakati wa mijadala ya Bunge.

“Licha ya kuamini kuwa katazo hilo linakinzana na Katiba na sheria nyingine za nchi, limetolewa ndani ya Bunge ambako ni vigumu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtoa kauli kutokana na kinga ya Bunge. Hata hivyo, sababu zilizotolewa kuhalalisha katazo hilo zinahitaji kuchunguzwa kwa kina,” amesema.

Amesema miongoni mwa hoja zilizotolewa ni kuwepo kwa vitisho vya kiusalama, jukumu la kukabiliana na vitisho hivyo ni la vyombo vya dola, si la kuzuia shughuli halali za vyama vya siasa.

“Kama kuna tishio la kiusalama, Serikali ina vyombo vya ulinzi na usalama vyenye wajibu wa kuzuia na kushughulikia uhalifu, haijaelezwa kuwa vyama vya siasa ndivyo vinavyohusika na vitisho hivyo; kilichotajwa ni uwepo wa watu wasiojulikana. Kwa hiyo, hatua zinapaswa kuelekezwa kwa wahusika badala ya kuathiri haki za vyama vya siasa vinavyotambuliwa kisheria,” amesema.

Aidha, Wakili huyo amehoji sababu ya kuwepo kwa hofu kuhusu maandamano wakati sheria tayari imeweka utaratibu wa jinsi yanavyopaswa kufanyika.

Maoni ya wakili huyo hayako mbali na mtazamo wa Wakili mwingine Jebra Kambole aliyesema katazo la Waziri Katambi halina uhalali wa kisheria.

“Hakuna kifungu chochote cha sheria kinachompa Waziri mamlaka ya kuzuia au kupiga marufuku mikutano ya hadhara. Aidha, sababu alizozitoa kuhalalisha katazo hilo si za kweli.

“Mbona watu wanakusanyika kwenye harusi, mikutano ya dini au maeneo kama Kariakoo ambako huwa na msongamano mkubwa wa watu, lakini hakuna anayepiga marufuku mikusanyiko hiyo?

“Hawawezi kudhani kuwa wahalifu hupatikana kwenye mikutano ya kisiasa pekee, hivyo katazo hili halina uhalali wa kisheria,” amesema.

Wakili Jebra amesema hakuna sharti lolote la kisheria linalovilazimisha vyama vya siasa kuomba kibali ili kufanya mikutano ya hadhara.

Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linaweza kuzuia mkutano wa hadhara endapo litapokea taarifa au maombi ya mkutano huo, kisha likafanya tathmini ya hali ya usalama na kujiridhisha kuwa kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.

Akinukuu vifungu vya 43 hadi 47 vya Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, amesema sheria hiyo imeweka wazi utaratibu wa uendeshaji wa mikutano ya vyama vya siasa, hivyo hatua iliyochukuliwa ya kuweka katazo la jumla si sahihi kisheria.

Anailenga Chadema

Akizungumza na Mwananchi baada ya katazo hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Bara, John Heche amesema uamuzi huo unakilenga moja kwa moja chama hicho.

“Hakuna chama chochote bana, wanasitisha Chadema isifanye mikutano, ila ni kinyume cha sheria na Katiba kwa sababu Waziri hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa,” amesema Heche.

Kiongozi huyo amesisitiza kwamba agizo hilo linamaanisha kwamba nchi haifuati tena sheria, mambo yanafanyika kiholela bila kufuata Katiba wala sheria za nchi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf amesema Taifa lipo katika kipindi kigumu ambacho kinahitaji busara kwa pande zote za wadau wa siasa nchini.

“Tupo katika kipindi cha mtikisiko unaogusa amani yetu ya nchi, tunahitaji busara ili tuvuke salama. Tukifanya makosa katika kipindi hiki tutarudi nyuma tulikotoka,” amesema Mirambo.

Mirambo amesema mikutano ya hadhara ni haki ya vyama vya siasa na kuzuia shughuli hizo ni kosa, kinachotakiwa ni kujua wanaozungumza hawakiuki utaratibu ikiwemo kutoongea uchochezi.

Amesema Tanzania kuna busara ambayo ilikuwapo kabla na mwanzoni wa mfumo wa vyama vingi ambapo mikutano ya hadhara ilitumika kutuliza nchi.

Kwa upande wake Salum Mwalimu, katibu mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali si sahihi na akahoji ametumia sheria ipi kuchukua uamuzi huo.

“Ni vyema akatueleza sheria ipi au utaratibu upi ameutumia, kama kuna tishio lolote sidhani kama ni sawa kusema vibali visitolewe katika kipindi bila kueleza taharuki hiyo ni aina gani au zuio hilo ni kwa muda gani,” amesema.

Amesema Serikali isiposema zuio hilo ni kwa muda gani, itasababisha taharuki nyingine au sintofahamu kwa Watanzania.

Waziri Kivuli wa Ulinzi, Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia wa ACT Wazalendo, Rashid Habib Ali amesema wanalaani vikali agizo hilo haramu kw kuwa ni jaribio la kuisukuma nchi katika giza.

“Agizo hili pia ni mwendelezo wa watalawa kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 20(1) na Sheria ya Vyama vya siasa Ibara ya 23(1) (a) na (b) zinazotoa uhuru wa vyama vyenye usajili wa kudumu kufanya mikutano ya hadhara,” amesema.


Imeandikwa na Habel Chidawali, Peter Sekela, Baraka Loshilaa na Bakari Kiango.