Prime
Usaili unapogeuka kilio kwa walimu wasio na ajira

Muktasari:
- Utaratibu wa sasa wa Serikali ni kuwafanyia usaili walimu wanaoomba ajira katika Utumishi wa Umma, hatua iliyozua mjadala kwa baadhi ya watu.
Adonis Byemelwa
Wiki mbili zilizopita nilipita mitaa ya Kwa Magimba, Kata ya Chamazi, jijini Dar es Salaam, nikakutana na kijana niliyemfundisha kidato cha sita miaka saba iliyopita.
Alinikumbuka na kunisabahi kwa heshima, nilimuona kachakaa, aliegesha pikipiki yake pembeni, huku akiwa amejaa vumbi la unga.
Akaniuliza kama namkumbuka, ukweli sikuweza kumkumbuka kutokana na hali yake au pengine miaka mingi kwani walimu hufundisha wanafunzi wengi na hivyo kuwa ngumu kuwaweka wote kichwani.
Huyu ni mhitimu wa shahada ya ualimu kutoka chuo kimoja maarufu nchini akiwa amebobea kwenye masomo ya kemia na biolojia.
Hajishughulishi na kazi aliyosomea, anachofanya sasa ni kusambaza unga kwenye maduka mbalimbali mitaa ya Mbagala, Mbande na Chamazi. Alinieleza kuwa kwa miaka kadhaa amekuwa akiomba nafasi za ualimu pasipo mafanikio.
“Niliamua kujiajiri kwenye hiki kibarua mwalimu. Ukitaka unga nakuletea mara moja. Hii pikipiki nia ya kaka yangu anayemiliki mashine mbili za kusaga hapo Mbande,’’ alisema na kuongeza:
‘’Kazi yangu imekuwa ni kusambaza unga. Nina mtoto mmoja na mke, maisha yanasonga. Nimekata tamaa na ajira hizi za ualimu; kila nikiomba sipati kazi.’’
Simulizi yake inafanana na ya Mwanamambo Kabobe, mwanafunzi wangu mwingine mhitimu wa ualimu, ambaye kwa miaka takribani saba sasa amekuwa akikatisha tiketi. Alianza kituo kikuu cha mabasi Ubungo na sasa yuko Magufuli pale Mbezi.
Huyu kasomea ualimu wa shule ya msingi Daraja A, hajawahi kupata ajira, amekuwa mtaani kipindi kirefu mpaka pale alipobahatisha kibarua cha kukatisha tiketi.
Hadithi hizi mbili hapo juu zinasawiri hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliyoitoa bungeni hivi karibuni akisisitiza kuwa ni lazima walimu wapya waajiriwe kupitia mfumo wa usaili.
Alisema kuwa Serikali imegundua kuwa kuna haja ya kuwekeza kwa walimu bora na hivyo imelazimika kuwafanyia mchujo mkali.
“Mimi niseme wazi kwamba ni lazima walimu wote wapiti usaili, kwasababu wametoka vyuoni wakiwa na uwezo tofauti. Nimekuwa nikipata maswali mengi kwamba tuajiri kwa kuangalia aliyekaa mtaani miaka kumi ama tuangalie ubora wao kupitia usaili, maana hawa wamehitimu vyuoni na najua walikuwa na uwezo tofauti,’’ alisema msomi huyo bobezi wa uchumi nchini.
Aliongeza: ‘’Niseme kwa mfano somo la Kiingereza, unamsaili mwalimu hawezi kujieleza sawasawa. Sasa huyu tumpe kazi kwa kigezo cha yeye kukaa mtaani bila kazi miaka kumi?’’
Mjadala
Hoja ya Profesa Mkenda imezua mawazo mseto kwa wadau wa elimu, huku wengi wakihoji ubora wa usaili huo na ni kwa namna gani mwalimu bora anaweza kupimwa kupitia maswali tu yanayoandaliwa kwa siku moja?
Wadau wengine wanahoji inawezekanaje walimu waliokaa mtaani kwa miaka zaidi ya kumi wakifanya shughuli za kukatisha tiketi na kusambaza unga wakumbuke baadhi ya misingi ya ufundishaji?
Wengine wanahoji inakuwaje walimu wanaonekana hawatoshi shuleni, ilhali wengi wako mtaani kwa miaka yote hiyo?
Profesa Mkenda anatetea utaratibu wa usaili kwamba ulichelewa sana katika kada ya ualimu nchini Tanzania, huku akitoa mfano wa nchi kama Ghana na Japan, kwamba zimekuwa zikitumia utaratibu huu kwa miaka mingi na kuwawezesha kupata walimu bora.
Wadau wa elimu wanahoji kama usaili huu unalenga kupata walimu bora ama ni mchujo maalumu wa kuweza kupunguza waombaji wa kazi ambao wamejaa mtaani wakifanya shughuli nyingine nje ya taaluma walizosomea.
Takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) (2022) zinaonesha kuwa Tanzania huzalisha takribani wahitimu 100,000 kila mwaka, huku asilimia chini ya 20 ndio wanaofanikiwa kupenya kwenye soko la ajira.
Timsiime Innocent, ni mhitimu wa shahada ya ualimu katika historia na Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino tangu mwaka 2018. Amekuwa akifanya kazi kituo cha mafuta jijini Mwanza na ameomba kazi ya ualimu serikalini kwa zaidi ya mara tano bila mafanikio.
“Mimi nilienda kwenye huo usaili tukaambiwa turudi siku nyingine baada ya kuonekana mtandao unasumbua. Tuliporudi nilikuata maswali ya usaili yakiwa na mitazamo tofauti; mengine niliyaona ya kawaida lakini mengine ni magumu. Nahisi ugumu huo unatokana na kuwa nimesahau kwani ni kipindi kirefu sana tangu nimalize chuo,’’ anaeleza.
‘’Nimekuwa najishughulisha na kazi tofauti na taaluma yangu na kipato ni kidogo mno, maana inafika kipindi unakaa nyumbani hadi unaona ufanye kazi yoyote inayojitokeza,” anaongeza kusema mhitimu huyo kwa uchungu.
Takwimu zinaonesha kuwa kwenye usaili wa somo la historia, walimu 15,136 walijitokeza na waliopitishwa kufanya usaili wa mdomo (oral interview) kwa awamu ya pili ni 1123, huku wanaohitajika ikielezwa kuwa ni walimu 500.
Usaili ni shida
Kwa msingi huo, usaili umekuwa si rafiki kwa waombaji japo wadau wengine wa elimu wanaona njia hiyo ni sahihi.
Wanaona huko ni kuipa heshima kazi ya ualimu ambayo hapo awali ilidharaulika kana kwamba ni taaluma inayoweza kufanywa na yeyote, ilhali kada nyingine kama utabibu na sheria zikihitaji mchujo wa hali ya juu.
“Ikitokea kijana kwa sasa anataka kusomea ualimu na amekwishaona kaka au dada yake amejaribu kufanya usaili kupata kazi hiyo mara tatu mfululizo bila mafanikio, lazima atakapoanza masomo atie bidii kwasababu tayari ni shuhuda wa ugumu wa kufikia viwango vya ubora wa kazi hiyo,’’ anasema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam, Dk Mohammed Ngunguti na kuongeza:
‘’Mwanzo itaumiza wengi lakini kwa baadaye itaheshimisha walimu na kuwanusuru wanetu wasifundishwe na walimu wasio na weledi wa kazi hiyo.”
Mhadhiri huyo anaongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, isiishie kuwabana wajiriwa wapya tu bali iiingie tena shuleni kuwasaili hata walio kazini na watakoshindwa kufikia vigezo warudie mpaka watakapofuzu.
Dk Ngunguti anaongeza kuwa watakaoshindwa kifikia vigezo wasifukuzwe ila wapewe fursa ya kujinoa na kufanya tena na tena usaili hadi wafaulu hata kwa mara kumi.
Lakini Prof Mkenda katika uwasilishaji wake bungeni aliwataka walimu wazidi kujinoa, akiwa na maana kwamba hata kama mhitimu anauza unga ama anafanya kazi kituo cha mafuta saa 24, atafute muda wa ziada kujifua juu ya masuala ya taaluma yake ili akidhi vigezo pale atakapohitajika kufanya usaili.
Mwalimu Amosi Elias wa jijini Dodoma, anasema kuna kozi ambazo mhitimu akifuzu humwezesha kuhawilisha maarifa yake bila shida, huku akitolea mfano wa mwanafunzi aliyefuzu masomo ya kupanga na kusimamia miradi.
Anasema mtu wa aina hii hata kama atakaa mtaani akingoja ajira, bado anaweza kuushughulisha ubongo wake kupitia yale aliyosoma kinadharia chuoni tofauti na kada nyingine kama ualimu.
“Mimi nahisi kuna haja ya kuwafundisha walimu ujasiriamali kwa kuwanoa wafungue shule ama vituo vya kulea watoto ili watumie taaluma zao; tofauti na sasa ambapo kuna kila sababu ya walimu wengi kusahau sayansi za ufundishaji kwani baadhi yao wamekuwa mtaani muda mrefu wakifanya kazi tofauti na taaluma zao,” anasema mwalimu Amosi.